Header Ads

KESI YA SAMAKI WA MAGUFURI YAZIDI KUUNGURUMA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa 10 wa Upande wa Jamhuri katika kesi ya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi katika kina kirefu cha Ukanda wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayowakabili raia 36 wa kigeni maarufu kama ‘kesi ya samaki wa Magufuli’, Mwanaidi Mndolwa ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,walipokagua Meli ya Tawariq 1 waliwakuta samaki wakiwa hawana vichwa.


Mndolwa ambaye ni Mtaalamu wa Uchakataji wa Samaki toka Wizara ya Maendeleo na Uvuvi ambaye pia ndiyo alikuwa ni miongoni mwa timu ya maofisa wa serikali na Jeshi la Polisi ambao ndiyo walipewa jukumu ya kuipekuwa meli ya Tawariq 1 ambayo ndiyo ilikamatwa ikivua samaki na kuaribu mazingira katika ukanda huo wa bahari ya Hindi, alitoa maelezo hayo wakati akiongozwa na wakili mwandamizi wa serikali Biswalo Mganga,Prosper Mwangamila na Mango kutoa ushahidi wake jana mbele ya Jaji Agustine Mwarija.

Mndolwa aliieleza mahakama kuwa zoezi upekuzi na upakuaji samaki toka ndani ya meli kuja kwenye majokofu lilichukua siku tisa ambapo samaki walianza kupakuliwa Machi 10-18 mwaka 2009 na wakati wanapekuwa Keptaini wa meli hiyo ambaye naye ni miongoni mwa washtakiwa alikuwepo ambapo walifanikiwa kupakua jumla ya makontena 19 na kila kontena moja lilikuwa kiifadhi zaidi ya samaki 900 na hivyo kufanya uzito huo kuwa ni wa tani 55.

“Na kufuatia upekuzi na upakuaji tuliwakuta samaki ndani ya meli hiyo ya Tawariq 1 ambao hawana vichwa na kitaalamu kutambua samaki aliyekwisha ondolewa vichwa kuwa wamevuliwa lini , huwezi kujua na samaki ambao tayari wameishaondolewa vichwa kitaalamu uweza kuishi bila kuaribika ndani ya miezi 18”alidai Mndolwa.

Mndolwa aliendelea kudai kuwa upekuzi wao ndani ya meli hiyo ulibaini meli hiyo ilikuwa na sehemu kwaajili ya kuifadhi utumbo,vichwa, mikia na kuongeza kuwa kwa mujibu wa kitaalamu meli ya uvuvi inatakiwa kuwa na eneo la kutunzia utumbo,mikia na kwamba walikuja majokofu yote yalikuwa yameifadhiwa samaki ambao wengi wao walikuwa ni aina ya Jodari, changu,vibua na ngisi na kwamba hawakukuta majokofu yaliyokuwa yameifadhi uchafu wa samaki hao.

Jaji Mwarija aliairisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri atapanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi.Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mfululizo hadi Mei 31 mwaka huu.

Machi 9 mwaka 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uvivu haramu katika kina kirefu cha habahari ya Hindi Ukanda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuharibu mazingira ya ukanda huo.Hadi sasa washtakiwa wanaendelea kusota rumande kwa kukosa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.