Header Ads

MSHTAKIWA RICHMOND ALIGUSHI SAINI-SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

MTAALAMU wa maandishi toka Jeshi la Polisi, Hamad Hamad ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa kuwa hati ya nguvu ya kisheria (Power of Attoney) iliyotolewa na mshtakiwa wa kesi ya kutoa taarifa za uongo kwa Bodi ya Shirika la Umeme Tanesco kuhusu Kampuni Richmond LLC ya Marekani, Naeem Gile ilikuwa
imegushiwa.


Hamad ambaye ni shahidi wa sita wa upande wa Jamhuri ambaye alikuwa akiongozwa na Wakili Kiongozi wa Serikali Fredrick Manyanda aliyekuwa akisaidiwa Shadrack Kimaro kutoa ushahidi wake alieleza kuwa Novemba 3 mwaka 2008 alipokea hadi hiyo ya nguvu ya kisheria na barua nyingine mbili ambazo zilikuwa hazibishaniwi ili aweze kuzifanyiakazi ya kitaalamu ambayo itatoa majibu ya nyaraka ipi kati yake ilikuwa imegushiwa.

Hamad alidai kuwa nyaraka hizo mbili zilikuwa zimesainiwa katika nyakati tofauti na Mkurugenzi wa Kampuni ya Richmond LLC, Mohamed Gire anayeishi nchini Marekani na hati ya nguvu ya kisheria (Power of Attoney) ilikuwa inaonyesha kusainiwa naye hiyo yeye kama mtaalamu wa maandishi aliletewa ili aweze kuzilinganisha saini hizo mbili zilizokuwa zimesainiwa kwenye barua hizo mbili ambazo zilikuwa zimesainiwa na mtu mmoja.

Alidai kwa kuangalia tu kwa macho aligundua tofauti kati ya saini iliyokuwa kwenye barua hizo mbili na ile iliyopo kwenye hati ya nguvu ya kisheria, na alipokagua kwa kutumia kifaa maalumu ,kifaa hicho kilitoa matokeo ambayo saini hizo zilizosainiwa kwenye nyaraka hizo mbili hazikuwa zimesainiwa na mtu mmoja.

Mshitakiwa Naeem katika kesi hiyo anadaiwa pia, akifahamu na kwa ulaghai,alitoa taarifa za uongo kuhusu kampuni hiyo ya kufua umeme kwa Bodi ya Shirika la Umeme la Tanesco kuwa inauwezo wa kuzalisha umeme hapa nchini hivyo apewe tenda na kwamba alikuwa amepewa nguvu ya kisheria ya kuendesha kampuni hiyo hapa nchini na Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC,Mohamed Gire ,inayoonyesha hati hiyo ya nguvu ya kisheria ambayo inaonyesha ilitolewa Machi 3, mwaka 2006,huku akijua si kweli.

Mshitakiwa anadaiwa Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme megawati 100 ili apewe tenda hiyo.

Kabla hakimu Walialwande Lema jana kuairisha kesi hiyo baada ya kuombwa na upande wa mashitaka kwa kuwa hawakuwa na shahidi mwingine, alionya kuwa jana alikuwa ametoa ahirisho la mwisho upande wa mashitaka walete mashahidi wao hivyo wajitahidi Juni 16 mashahidi hao wafike mahakamani

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 27 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.