Header Ads

HUKUMU KESI YA EPA :YAMETIMIA


.MARANDA,FARIJALA JELA MIAKA MITANO
.WASHTAKIWA WENGINE WA EPA MATUMBO MOTO
.HUKUMU YAWALIZA NDUGU,JAMAA
Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilitoa hukumu ya kwanza katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 zilizochotwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu (BoT).


Hukumu hiyo ilizusha vilio na kuifanya mahakama hiyo kuzizima kwa muda baada ya Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Rajab Maranda na binamu yake Farijala Hussein kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Katika kesi hiyo, ndugu hao makada wa CCM wanadaiwa kughushu nyaraka na kujipatia sh bilioni 1.8 isivyo halali kutoka kwenye akaunti hiyo. Hiyo ni miongoni mwa kesi 14 za EPA zilizopo mahakamani.

Jopo la mahakimu wakazi likiongozwa Saul Kinemela lilianza kusoma hukumu hiyo kwa saa moja ndani ya ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo.

Mahakimu wengine ni Phocus Bambikya Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Elvin Mugeta, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akisoma kwa kujiamini Hakimu Mugeta alisema kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Novemba 4, 2008 ambapo jumla ya mashahidi tisa upande wa Jamuhuri walitoa ushahidi wao.

Hakimu Mugeta aliikumbusha mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walikabiliwa na makosa nane ambayo ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa, wizi wa sh bilioni 1.8 na kughushi hati ya kuhamisha deni (deed of asssigment) inayoonyesha kampuni hewa ya Kiloloma & Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai ya India.

Makosa mengine ni kughushi hati ya jina la biashara la kampuni hiyo inayoonyesha imetolewa na Msajili wa Makampuni (BRELA), kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa BoT, kuwasilisha nyaraka hizo kwenye Benki ya Afrika (BOA), kufungua akaunti na kujipatia ingizo la kiasi cha sh 1,864,949,294.45 isivyo halali.

“Baada ya kupitia hati ya makosa hayo, kupitia ushahidi na utetezi uliotolewa na pande zote mbili, jopo hili limefikia uamuzi wa kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa la pili, tatu, nne, tano, sita na saba.

“Na kwamba mahakama imeshindwa kuwatia hatiani kwa kosa la kwanza ambalo ni kula njama na kosa la nane ambalo ni wizi kwa sababu upande wa jamuhuri umeshindwa kuthibitisha kwamba washtakiwa hao walikula njama na kuiba katika BoT,” alisema Hakimu Mugeta huku ndugu na jamaa wakijifuta machozi ndani ya chumba cha mahakama.

Hakimu huyo alisema jopo hilo linakubalina na ushahidi wa jamuhuri kuwa washtakiwa hao walighushi nyaraka hizo kwa sababu mashahidi watatu ambao ni Ofisa wa Polisi Salum Kisai, Mkurugenzi Mtendaji wa BRELA, Esteriano Mahingira, na Neema Kitambi Ofisa wa Benki ya BOA.

Katika ushahidi wao, waliithibitishia mahakama hiyo kuwa nyaraka na saini iliyokuwa kwenye hati hiyo na jina la biashara ya Kampuni ya Kiloloma&Brothers vilighushiwa.
“Kwa mujibu wa utetezi wa Maranda na Farijala, nyaraka hizo hazikuandaliwa na wao bali ziliandaliwa na Charles Issack Kissa… sasa mahakama hii imejiuliza kwa nini washtakiwa hao wasingemleta huyo Kissa kama shahidi wao ili awatetee?

“Kwa kuwa hawakumleta Kissa mahakama hii inakubaliana na upande wa jamuhuri kuwa huyo ni mtu wa kufikirika na kwamba Kissa ndiyo Farijala aliyeghushi nyaraka hizo,” alisema Hakimu Mugeta aliyekuwa anavuta pumzi kwa kunywa maji.

Akiendelea kuichambua hukumu hiyo, Mugeta alisema katika utetezi wao washtakiwa walikiri kwa hiyari yao ni wamiliki wa kampuni ya Kiloloma & Brothers na kwamba walifungua akaunti ya pamoja katika Benki ya Afrika na kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka BoT.

Kwa upande wake Maranda alikiri pia kuhusika na mchakato wa kudai deni hilo na kweli alipewa idhini na kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India kudai deni hilo kwa kuwa alichokizingatia ni fedha, sio uhalali wa nyaraka zilizotumika kupata fedha hizo.

Hakimu huyo alisema jopo hilo limeukataa utetezi wa washtakiwa kwa kuwa hauna msingi hivyo Mahakama inakubalina na upande wa Jamuhuri kwamba washtakiwa hao na watu wengine wasiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam mwaka 2005 walighushi nyaraka hizo na kujipatia mabilioni ya fedha.

Baada ya kuwatia hatiani washtakiwa hao, jopo hilo lilitoa fursa kwa upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface wakati upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili wa kujitegemea Majura Magafu, kusema lolote kabla ya adhabu kutolewa.

Wakili Boniface aliyekuwa akisaidiwa na Wakili Shadrack Kimaro, aliieleza Mahakama kuwa kwa kumbukumbu zinaonyesha hii ni mara ya kwanza kwa washtakiwa hao kutiwa hatiani hivyo ione haja ya kuwapa adhabu kali kwa kuzingatia kiasi kikubwa cha fedha kilichopotea.

Aidha, aliiomba mahakama kutumia kifungu cha 358 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ili itoe amri kwa washtakiwa kurejesha kiasi hicho cha fedha kwa mwenye mali ambaye ni serikali ama wafilisiwe mali zao.

Kwa upande wake wakili Magafu aliiomba mahakama kuwaonea huruma washtakiwa kwa kuwa ni mara ya kwanza kutiwa hatiani, pia ni wagonjwa wa figo, wanategemewa na familia zao na kwamba makosa mengine waliyatenda bila kujua au kutoelekezwa vema na taasisi husika.

Magafu pia aliiomba mahakama kutumia kifungu cha 38 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 kinachoeleza kuwa pamoja na mahakama kumtia hatiani mshtakiwa, inaweza kumwachilia huru kwa masharti hivyo kuliomba jopo hilo kuzingatia kifungu hicho litakapotoa adhabu.

Akisoma adhabu baada ya kusikiliza maombi ya mawakili wa pande zote, Hakimu Mugeta alisema jopo hilo limezingatia maombi yao mawakili na uzito wa makosa hivyo limewatia hatiani katika kosa la pili ambalo washtakiwa wote watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, kosa la tatu ambalo washtakiwa wote wametiwa hatiani kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitano jela wakati kosa la nne washtakiwa hao watatumikia miaka mitano jela.

Aidha, katika kosa la tano Maranda amepatikana na hatia hivyo atatumikia miaka miwili jela huku kosa la sita ambalo washtakiwa wote wametiwa hatiani, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na shtaka la saba lililowatia hatiani wote, watatumikia kifungo cha miaka miatatu jela.

Hivyo watuhumiwa hao walihukumiwa kifungo cha miaka 21 adhabu itakayokwenda kwa pamoja ambapo watatumikia miaka mitano jela.

Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo jopo la mahakimu liliondoka na kufanya ndugu, jamaa na marafiki wa watuhumiwa hao wakiangua vilio kwa sauti ya juu kisha askari polisi waliwatoa kizimbani washtakiwa hao na kuwapeleka mahabusu ya mahakama hiyo kusubiri taratibu za kiutawala ili wapelekwe kuishi makazi mapya katika Gereza la Ukonga.

Tangu saa 5:22 asubuhi washtakiwa hao walihifadhiwa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo huku Tanzania Daima ikishuhudia jamaa zao wakihaha huku na kule na wengine kununua maji, dawa za miswaki, sabuni na maziwa kwa ajili ya wafungwa hao ambao waliondolewa mahakamani hapo saa 9:30 alasiri kwa gari aina ya Toyota Land Cruser lenye namba za usajili SCN 9008K mali ya Jeshi la Polisi.

Wakati Farijala na Maranda wanaondolewa katika eneo la mahakama hiyo, askari kanzu na waliovalia sare wakiwa na silaha kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na wafungwa hao walipandishwa kwenye gari la wazi na kuketi nyuma mithili ya ‘maharusi’ huku wakiwapungia mikono watu waliofurika mahakamani hapo.

Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao walisema adhabu hiyo ni ndogo ikilinganishwa na kiasi cha fedha kilichochukuliwa na kuipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kazi nzuri ya kutoa ushahidi ulioiwezesha mahakama kuwatia hatiani wafanyabiashara hao.

Kwa mwingine baadhi ya mawakili wa kesi nyingine za EPA walisema hukumu hiyo ni ishara mbaya kwa wateja wao na kwamba kesi hizo sio usanii kama ilivyokuwa ikidhaniwa na wengi.

Jumla ya kesi 14 za EPA zilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Eliezer Feleshi, Novemba 4, 2008 dhidi ya washtakiwa mbalimbali wakiwemo mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel na wenzake na baadhi ya maofisa wa BoT ambao kesi zao zinaendelea mahakamani hapo.

Jumla ya kesi 14 za EPA zilifunguliwa na DDP- Feleshi kwa kishindo kwa mara ya kwanza Novemba 4 mwaka 2008 dhidi ya washtakiwa mbalimbali wakiwemo mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel na wenzake na baadhi ya maofisa wa BoT ambao bado kesi zao zinaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

Mbali na kesi hiyo Na.1161/2008 ambayo jana ilitolewa hukumu, Maranda na Farijala pia wanakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa Sh milioni 207 ambapo anashtakiwa yeye na maofisa wa BoT, Mkuu wa Idara ya EPA, Iman Mwakosya na Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo Ester Komu, na Katibu wa Benki Bosco Kimela.

Katika kesi hiyo ya wizi Maranda anadaiwa kutumia nyaraka za kughushi kuonyesha kampuni yake ya Rashaz Tanzania kuwa imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Rashaz T Ltd na kisha kujipatia ingizo hilo la Sh milioni 207 huku akijua si kweli.

Kesi ya tatu ya jinai ni kesi Na. 1164/2008 ya wizi wa shilingi bilioni 3.8 katika akaunti hiyo ambayo inasikilizwa mbele ya jaji Beatrice Mutungi, Hakimu Mkazi Samwel Karua na Elvin Mugeta. Katika kesi hiyo, washitakiwa Farijala, Maranda, Iman Mwakosya, Ester Komu, Ajay Somani na Sophia Lalika walitumia kampuni ya Mibale Farm kuonyesha imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Lakshmi Textile Mills co. Limited ya India huku wakijua si kweli.

Juni 11 mwaka 2009, mahakama hiyo ilimuona Maranda na Farijala ambao wanakabiliwa na jumla ya kesi nne za wizi katika EPA, kuwa wana kesi ya kujibu katika kesi Na.1161/2008 ambayo ilitolewa hukumu jana na kwamba upande wa Jamhuri unaowakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface aliyekuwa anasaidiwa na Timon Vitalis, Frederick Manyanda na Shadrack Kimaro umeweza kuthibitisha kesi yao.

Juni 6 mwaka 2009, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Boniface aliwasilisha majumuisho ya kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wote hao wana kesi ya kujibu, kwani Jamhuri imeweza kuthibitisha kesi hiyo na kwa hiyo washtakiwa hao wana kila sababu ya kujibu kesi inayowakabili.

Aidha, Aprili 29 mwaka 2010, Rajabu Maranda alipanda kizimbani kutoa utetezi wake katika kesi hiyo ambayo leo inatolewa hukumu ambapo aliieleza mahakama hiyo kuwa alichokuwa akikizingatia katika mchakato wa kudai deni katika (EPA) ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.

Itakumbukwa kuwa serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) Feleshi iliwaburuza mahakamani watuhumiwa wa wizi katika akaunti ya EPA, baada ya tuhuma kuibuliwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoo, kelele za wananchi na wafadhili, hali iliyosababisha Rais Kikwete kuunda Tume ya uchunguzi wa wizi huo ambayo ilimshirikisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP-Said Mwema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dk. Edward Hosea na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa sasa amestaafu, Johnson Mwanyika.Tume hiyo iliwahoji watuhumiwa na hatimaye kuwafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.