WATANZANIA TUSITUHUMIANE HOVYO,TUFUATE SHERIA
Na Happiness Katabazi
KIFUNGU cha 7(1)(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002; kinasema ni wajibu wa kila mwananchi anayefahamu taarifa za kutendeka au kuna mtu anania ya kutenda uhalifu au mauji,analazimika kutoa taarifa hizo kwenye mamlaka husika za dola.
Na endapo mtu huyo atashindwa kutimiza waibu huo anaweza kushtakiwa kwa kosa la kusaidia kutendeka kwa kosa kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code R:E;2002).
Kifungu cha 99(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ,kina mruhusu hakimu kutoa kibali kwa mwananchi aliyeomba mahakama impatie kibali cha kuendesha kesi binafsi si bali kuhusisha waendesha mashtaka wa serikali.
Na kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la Pili iliyochapishwa na Oxford Universty Press, inatoa maana ya neno Fisadi .Ina sema Fisadi maana yake ni “Mtu mbaya ,mtongozaji,mharibifu,mpotevu,mwasherati;-guberi”.
Fukuto la Jamii limelazimika kuanza kwa kunukuu vifungu hivyo vya sheria na Kamusi hiyo ni kwasababu limeona kadri siku zinavyozidi kwenda hapa nchini baadhi ya wanasiasa,vyombo vya habari,viongozi wa dini na wananchi wamekuwa wakirushiana maneno kuwa huyu,yule ni fisadi.
Hivi sasa hapa nchini kumekuwa na upumbavu miongoni mwa pande mbili za baadhi ya wanasiasa wa chama tawala na wale wa vyama vya upinzani,baadhi ya vyombo vya habari, viongozi wa dini ambao wamekuwa wakionyesha dhahiri kuegemea upande mmoja katika pande hizo mbili.
Upumbavu huo ni ule wa miongoni mwao wa kumhukumu mwanasiasa fulani kuwa ni fisadi wakati kumbe naye huyo anayemhukumu kwa maneno mwanasiasa mwenzie kumbe naye ana ananukia halufu ya ufisadi.
Hadi sasa hakuna hata kundi moja hapo juu lililokwenda mahakamani kumfungulia mwanasiasa mmoja anayemtuhumu kufanya ubadhirifu wa rasilimali za taifa au kwenda kituo chochote cha polisi kutoa taarifa za mwanasiasa au ofisa yoyote wa serikali kuomba achunguzwe kwani ana ushahidi mkononi unaonyesha mwanasiasa au ofisa wa serikali ni mbadhilifu(fisadi) wa mali za umma ,chama na amegushi vyeti(fisadi wa elimu) ndiyo maana amekuwa akimtaja kwa jina mwanasiasa huyo majukwaani kuwa ni fisadi na siyo mtuhumiwa wa ufisadi.
Tunachokishuhudia sasa ni kwa baadhi ya wanasiasa au wafanyabiashara kumfungulia kesi mwanasiasa fulani au mfanyabiashara fulani kuwa amemkashfu binafsi mbele ya jamii kwa kumuita yeye ni fisadi.Na mfano wa hili ni zile kesi za madai ya kashfa zilizowahi kufunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Reginald Mengi na ile kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyofunguliwa na Yusuf Manji na Reginald Mengi ambapo mahakama hiyo imetoa amri ya kuzuia vyombo vya habari visiripoti kesi hiyo.
Inashangaza sana kuona ni sisi wananchi tumekuwa na ujasiri na wepesi sana wa kuwakamata wale tunaowatuhumu kuwa wametuibia simu,pochi,mikufu, majumbani kwetu na kuwapiga,kuwachoma moto au kuwapeleka vituo vya polisi ili sheria zichukue mkondo wake lakini siku za hivi karibuni nimekuwa nikijiuliza ni kwanini ni sisi wananchi tunaojitapa kuwa tunachukia ufisadi na tuna uchungu wa mali ya umma tumekuwa vinara wa kusimama majukwaani na kwenye vyombo vya habari kuwataja fulani na fulani tena kwa majina kuwa wanafuja rasilimali za nchi lakini tunashindwa kwenda vituo vya polisi vilivyopo karibu yetu kutoa taarifa hizo za wale mliowahukumu kwenye majukwaa kuwa wamekuwa wakifuja rasilimali za taifa ili polisi waweze kuzifanyia kazi?
Mbona tumekuwa taifa la watu wanaopenda kuzungumza sana,majungu,kuchafuana kuliko kuchukua hatua?Kusema fulani ana mali nyingi basi ni fisadi wakati wewe uliyeanzisha tuhuma hizo hadharani unashindwa kuisaidia polisi kuwa mali za mtu huyo ni zake kweli?Mali hizo zipo maeneo gani?Kweli amezipata kwa haramu?
Kwani hapa nchini hatuna kipimo kinachoonyesha mwenye mali kiasi hiki ni tajiri au bilionea na wala hakuna sheria inayomkataza mtu kumiliki mali.
Hakika huo ni udhaifu mwingine wa wajenga hoja wanaowatuhumu wenzao kuwa wana mali nyingi.Mwisho wa siku hata hilo jeshi la polisi au Takukuru zitapata wakati mgumu wa kuanzia uchunguzi wao dhidi ya mtu huyo.
Lakini ikumbukwe kuwa nao hao mnaowataja hadharani kuwa ni mafisadi kuwa wana mbinu sana tena kuliko hata nyie mnaowataja.Na hili ninalolisema hata IGP-Said Mwema, Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU),Dk.Edward Hosea walishawahi kukiri kwenye vyombo vya habari kuwa mafisadi ni watu wenye mbinu sana.
Wewe raia mwema ambaye kweli unadai una uchungu sana na rasilimali za taifa hili na mnawachukia mafisadi wa mali za umma mnatamba kuwa mna mnataarifa za uhakika kuwa mwanasiasa,ofisa wa serikali ni mbadhilifu fulani wabadhilifu, sasa ni kwa nini mnashindwa kupeleka taarifa hizo kwenye vyombo vya dola ili muweze kusaidiana na vyombo hivyo ili hizo taarifa za ubadhilifu ziweze kufanyiwa kazi?
Kama tulivyokwisha elezwa na IGP-Mwema, Dk.Hosea kuwa mafisadi wana mbinu sana, hamuoni mnavyowaanika majukwaani ndiyo nao wanaibuka na mbinu nyingine mbadala tena kimya kimya za kuvuruga ushahidi wa hizo tuhuma mnazozielekeza kwao.?
Sasa kwa muktadha huo nyie mliojipa jukumu la kuwasema wenzenu ni mafisadi mtakuwa hamuisaidii serikali badala yake mtakuwa mnazidi kuwapa mbinu hao mnaowahukumu kuwa ni mafisadi kubuni mbinu mpya za kuiba, kubadilisha umiliki wa mali wanazozimiliki, kuhamisha fedha kwenye akaunti zao na kwenda kuzihifadhi kwenye akaunti zenye majina ya watu wengine na mwisho wa siku vyombo vya upelelezi vitajikuta vinashindwa kukusanya ushahidi mathubutu dhidi ya wao na hivyo kujikuta wanashindwa kuwafikisha mahakamani?
Kuna watanzania wengi sana wenye mapenzi ya kweli na taifa lao tena wala hawana mpango wa kujikomba ili wapatiwe madaraka,wala hawabwatuki majukwaani pindi wapatapo taarifa za kutendeka au kuna watu wanataka kutenda uhalifu wamekuwa wakienda kimya kimya kwenye mamlaka husika kutoa taarifa na taarifa hizo zimekuwa zikifanyiwa kazi na mwisho wa siku waliohusika vitendo hivyo wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani?
Lakini hilo miongoni mwa wanasiasa wetu tena wa pande mbili yaani wa chama tawala na upinzani hilo la kwenda kutoa taarifa katika taasisi husika kuhusu ubadhilifu mkubwa kutendeka limewashinda kabisa matokeo yake hivi sasa wamegeuza hilo la kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola za kuhusu kutendeka kwa uhalifu kuwa ni ngazi ya kupandia kupata umaarufu wa ‘chee’ katika jamii yetu lakini Uchaguzi mkuu unapofika wananchi wale wale waliokuwa wakimshangilia mwanasiasa huyo aliyejipa jukumu la kuwahukumu wenzao kuwa ni mafisadi, wanamnyima kura za ndiyo wanampatia kura za ndiyo yule aliyehukumiwa majukwaani kuwa ni fisadi.
Ikumbukwe kwamba nchi hii ni ya watanzania wote walio wanachama wa vyama vya siasa na siyo wanachama wa vyama vya siasa kwahiyo sote tuna uhuru wa kutoa taarifa za kutendeka au kutaka kutendeka kwa uhalibifu au ubadhirifu wa rasilimali za umma, kulinda rasilimali za nchi yetu kwa kushirikiana na serikali iliyopo madarakani kwa sasa.Sasa inapotokea kikundi cha watu fulani kikaanza kukwepa uhuru huo na majukumu hayo ambayo yameainishwa hata kwenye Katiba na sheria ya makosa ya Jinai ya mwaka 2002,inashangaza sana.
Pia ikumbukwe hata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)Elizer Feleshi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kufungua kesi mahakamani kabla ya kufungua kesi za jinai mahakamani anapaswa kukusanya na kujiridhisha na baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa kwake na pia ajiridhishe kwa kuona baadhi ya maelezo ya mashahidi ambao anatarajia kuwatumia kujenga kesi atakayoifungua mahakamani na siyo ‘blaa blaa’ zitolewazo na baadhi wanasiasa,wananchi na baadhi ya vyombo vya habari.
Na matokeo yake vikundi hivyo vya wanasiasa vikaamua kutumia njia inazozijua kusema serikali iliyopo maradakani imeshindwa kutimiza wajibu hivyo iondoke madarakani na wakati wakitoa madai hayo vikundi hivyo vinakwenda kuomba ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara na kuomba ulinzi kwa jeshi la Polisi ambalo jeshi la polisi linaongozwa na IGP-Mwema ambaye naye ameteuliwa kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete ambaye naye baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanamuita ni fisadi ,kwakweli huwanapata shida kuwaelewa wanasiasa wa aina hiyo ambao wanakataa kula nyama ya nguruwe lakini wanakunywa supu yake!
Mbona hatujawasikia hao wanasiasa vinara wa kuwasema wenzao ni mafisadi kwamba walishapeleka kituo chochote cha polisi,Takukuru au mamlaka nyingine za dola taarifa kuhusu watu kadhaa kutenda au kuwa nania ya kutenda uhalifu halafu taarifa hizo hazikufanyiwa kazi na mamlaka hizo?
Na mbona hatujawasikia hao wanasiasa vinara wa kuwahukumu wenzao kuwa ni mafisadi kwamba walishawahi kufika mahakamani na kuomba kibali cha mahakama cha kuendesha kesi binafsi bila kuwashirikisha mawakili wa serikali halafu mahakama ikawafukuza au kuwanyima kibali hicho?
Nadiriki kusema kwa sasa tulipofika hao baadhi ya wanasiasa toka CCM na vyama vya upinzani waliokuwa mstari wa mbele wa kuwataja wanasiasa wenzao kuwa ni mafisadi bila kupeleka taarifa na ushahidi wa tuhuma hizo katika mahakama husika, wanatuharibia nchi taratibu.
Leo hii makala hii itadharauliwa sana na majuha lakini nawataka wananchi tuamke na kuwahoji hao viongozi wetu wa siasa siku wakikosa kile wanachokiita kuibua ufisadi watatueleza nini sisi wapiga kura wao na wananchi kwa ujumla?
Maana ninachokiona hivi sasa na baadhi ya viongozi wa Chadema na CCM,baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kuwahukumu wenzao kuwa ni mafisadi, hakitofautiani sana na kile kilichokuwa kikifanywa Mbunge wa Vunjo(TLP),Agustine Mrema wakati akiwa Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi lakini mwisho wa siku alipoishiwa ajenda hizo tuna muona hivi sasa ameachana na mtindo huo na badala yake anafanyakazi zake vyema za kibunge.
Je tuwaulize hao vinara wa sasa siku watakapopata nyadhifa fulani kubwa kule serikalini kama alioupata yule mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa Zanzibar kwa chama cha (CUF) cha Makamu wa Pili wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad,ndiyo watapunguza kasi ya maandamano na mikutano ya hadhara na kusimama majukwaani kudai serikali iliyopo madarakani imeshindwa kazi?
Wanasiasa wengi tabia na hulka zao wengi zinaeleweka, kama hawajapata kile wanachokitaka wao binafsi huwa wana hulka ya kubwatabwata majukwaani lakini pindi wanapopata nyadhifa walizokuwa wakizinyemelea,huamua kuvisaliti hata vyama vyao na kuamua kusalimu amri katika kile ambacho awali walikuwa wakikiita ni mapambano dhidi wabadhilifu wa rasilimali za umma na serikali iliyopo madarakani.
Nina uzoefu na hili kwani Uchaguzi wa mwaka 1995 na 2000,2005 na 2010 nili bahatika kuzishuhudia chaguzi hizi.Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na 2005 ulitawaliwa na vurugu za hhapa na pale.Viongozi wa vyama upinzani wakati huo walikuwa wakiwatanguliza mstari wa mbele vijana kushiriki na kuongoza maandamano ambayo serikali ilikuwa imeyapiga marufuku na mwisho wa siku vijana hao wakajikuta wanaangukia kwenye mikono ya polisi kwa kupigwa na wengine kupoteza maisha yao na wengine kupata ulemavu wa kudumu huku wale viongozi wao waliokuwa wakiwatuma kukwepa vipigo na wengine hivi sasa wamerudi CCM tunawajua, ambao ndiyo walikuwa wakituhadaa sisi wananchi kuwa ni chama kilichochoka na wamepewa madaraka na wapo wengi tu.
Sasa ni rai yangu kwa wanasiasa na sisi wote tunao watuhumu wenzetu kwenye jamii kuwa ni vinara wa ufisadi ,tukasoma kwanza maana ya neno ‘Fisadi’ kisha kila mmoja kwa wakati wake ajiulize kimya kimya kuwa yeye siyo fisadi?
Maana kwa mujibu wa Kamusi hiyo inasema Fisadi ni ‘ Mtu mbaya, mtongozaji, mharibifu, mpotevu, mwasherati;-guberi”.Sasa nyie wanasiasa mnaowasema wenzenu ni mafisadi Je tuwaulize hakuna hata mmoja ambaye ajihusishi na vitendo vya uasherati? Je hakuna hata mmoja wenu ambaye hadi leo hii amewahi kuisaliti ndoa yake kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na vimada nje ya ndoa yake?.Miongoni mwenu nanyi mmekuwa mkituhumiwa kuwa ni vinara wa uasherati. Na uasherati umetajwa kwenye maana nzima ya neno fisadi.Je hamuoni na nyie mnapaswa kuitwa adharani ni mafisadi pia?
Na tukumbuke hao tunaowahukumu mbele za familia zao na jamii kuwa ni mafisadi wakati mwingine hakuna ushahidi wa madai hayo mkae mkijua wanafamilia na wana watoto, wanawasikia na watoto wao wanawatazama,wana chukia,wanakasirika na kuwaweka kwenye kumbukumbu zao na dhambi hiyo itawatafuna .Mwisho wa siku watoto hao watakuja kulipiza visasi tu.Sasa hatutaki kujenga taifa la vijana wenye visasi dhidi ya vijana ambao hapo nyuma baba zao waliwaumiza baba zao kwa kuwadhalilisha mbele ya umma na familia zao.Na huko ndipo taifa la Tanzania lilipo na linapoelekea.Tukomeshe upuuzi huu,haraka sana.
Tunataka kuwa na wanasiasa wa chama tawala,upinzani ambao wanatoa hotuba zinazotoa dira kwa taifa na kufundisha wananchi na siyo kama ilivyo hivi sasa kwa baadhi ya wanasiasa wengi kutoa matamko au hotuba zenye lengo la kuumbuana,kushushiana heshima na kuchafuana badala ya kutoa hotuba za kuwaelekeza wananchi na wanachama wao dira ya taifa na vyama vyao ni ipi.
Hayati Julias Nyerere,viongozi wengine wa kisiasa barani Afrika na wanasiasa makini hapa nchini kabla ya vyama vyao kushika hatamu na wakati ni viongozi wa kuu wa serikali wamekuwa na walikuwa wakitoa hotuba zenye kuonyesha dira na mwelekeo kwa wananchi na wanachama wao na hadi leo ukizitafuta hotuba zao na kuzisoma kuna mambo utajifunza kutokana na hotuba zao, lakini siyo kama ilivyosasa kwa baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani na baadhi ya CCM kutwa wamekuwa wakitoa matamko ambayo hata vizazi vyetu havitafaidika na hotuba hizo zaidi zaidi watakachoambulia ni kujivunza tabia mbaya ya kuzulia maneno na kupakana matope.Mmbadilike.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 17 mwaka 2011
No comments:
Post a Comment