Header Ads

WANAHABARI TUJITAZAME UPYA


Na Happiness Katabazi

WIKI iliyopita Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari(MCT), Kajubi Mkajanga alinukuliwa na vyombo vya habari akikemea tabia ya baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuchapisha na kutangaza habari ambazo zinaleta misuguano ya viongozi wa dini na taasisi hizo.


Kajubi pamoja na mambo mengi alikemea pia taabia ya wanahabari kushindwa kusimama kwenye maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na matokeo yake wamekuwa wakitangaza na kuchapisha habari ambazo zinaleta madhara katika baadhi ya taasisi za kidini, wananchi na jamii kwa ujumla hali iliyodai haipo kwenye utamaduni wa nchi yetu.

Fukuto la Jamii linaunga mkono hoja ya Mkajanga ambaye naye pia ni mwanahabari kitaaluma kwamba hivi sasa umezuka uandishi wa kuleta uchochezi wa kijaami.Lakini kwa wale wanaomfahamu Mkajanga kufuatilia matamko yake watakubaliana nami yeye ni miongoni mwa wanahabari wa zamani ambao wamekuwa wakitoa matamko ya kukemea aina ya uandishi unapofanywa hivi sasa na wanahabari na waandishi wa kizazi hiki ambao kwa kiasi fulani usipodhibitiwa mwisho wa siku unaweza kulitumbukiza taifa shimoni.

Mkajanga kupitia Baraza la Habari (MCT) kila kukicha wamekuwa wakikemea hali hiyo lakini cha kusikitisha baraza hilo Fukuto la Jamii leo linadiriki kutamka bayana baraza hilo halina meno na linaitaji kupatiwa meno hili liweze kung’ata vyombo ya habari ambavyo vinatangaza au kuchapisha habari ambazo zinakwenda kinyume na miiko ya taaluma.

Baraza hilo kila kukicha kulalamika mbele ya jamii au kuwaita wahariri ambao vyombo vyao vimechapisha habari zisizo na maadili au kufanyakazi za usuluhishi,haitoshi kabisa.Tunataka Baraza hilo ama liiambie serikali au limweleze mfadhili wake kwamba wakati umefika sasa wakuifanyia mabadiliko ya muundo na sera ya baraza hilo ili kipengele cha kuweza kuvibana vyombo vya habari na kutoa adhabu kali kwa mhariri,chombo na mwandishi waliohusika kuandika habari zisizokidhi viwango vya kitaaluma.

Mbona taaluma zingine kama mawakili, madaktari,wahandisi wana mabaraza yao na Kamati za Maadili ambapo pindi mwanataaluma wake anapokiuka miiko ya taaluma yake uweza kumshughulikia kikamilifu?Kwanini sisi wanahabari hatuna chombo chenye meno cha kuweza kutushughulikia hadi tumsubiri Waziri wa Habari ndiyo atoe amri ya kufungia gazeti?

Hiyo ni sura moja ya mada ya leo ,sura ya pili ya makala ya leo inajumuisha waandishi wa habari,wahariri, yombo vya upelelezi, mahakama na wananchi wenyewe.

Dhima nzima ya ujumla ya makala ya leo ninazungumzia aina ya uhandishi wa habari na jinsi ya wananchi wengi wakati mwingine wasiyofahamu ajenda iliyopo kwenye hizo habari au makala wanazosishabikia.Kila siku binafsi napenda kuipongeza serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwani katika utawala wake uhuru wa wananchi kujieleza na vyombo vya habari umekuwa ukikua kila kukicha na katika hili katika maisha yangu yote nitaikumbuka serikali ya awamu ya nne.

Lakini pia nitaendelea kuilaumu serikali inayoongozwa na rais Kikwete kwa kushindwa kuchukua hatua kwa baadhi ya vyombo vya habari ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikichapisha habari kiushabiki, za uongo na za kuleta uchochezi wazi wazi.Na mifano hayo ninayoisema ni mingi lakini Idara ya Habari ,Vyombo vya Upelelezi, Mahakama,mahakama vipo kwenye lindi la usingi mzito sana kana kwamba hawazisomi habari hizo.

Mfano mzuri ni miongoni mwa waandishi wa habari za mahakama,kuna wenzetu ambao kwa ujinga wao hawataki kujifunza wala kuuliza maofisa wa mahakama,kusoma majalada ya kesi ili kufahamu kilichoandikwa kwenye jarada hilo wamekuwa wakiandika habari kuhusu kesi fulani zikiwa na makosa makubwa na upotoshaji.

Mfano hakimu ametoa uamuzi(ruling)- mwandishi anasema hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Flora Mushi ametoa hukumu(Judgment),hakimu ameifuta kesi ya kuvunja na kuiba katika ghala Kampuni inayozalisha kinywaji cha Konyagi,Tanzania Distillers Limited ,inayowa wakabili walinzi wa Kampuni ya KK Security,chini ya kifungu cha 225 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Waandishi wengine walioripoti kufutwa kwa kesi hiyo bila woga waliliropiti kuwa hakimu huyo ametumia kifungu cha 225 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Huku ukweli ni kwamba kifungu hicho kipo ndani ya Sheria ya Makosa ya Jinai ambacho kinampa mamkala hakimu hakimu kuifuta kesi isipokuwa kesi ya kughushi na kinataka ndani ya siku 60 upelelezi wa kesi uwe umekamilika.

Sasa upotoshwaji wa aina hiyo tena wa mwenendo wa kesi za mahakama unaofanywa na baadhi ya waandishi tena waandamizi wasiotaka kuuliza, kujifunza na matokeo yake mwisho wa siku heshima ya gazeti ndiyo inayoporoka mbele ya wasomi wa sheria na wale wanaofahamu kifungu cha 225 cha Sheria ya makosa ya jinai, kinasema nini na kwamba kifungu hicho si cha Katiba.

Wakati uongo na ujuha huo ukiendelea kufanywa na baadhi ya wanahabari ambao unasababisha jamii kukaririshwa na kuaminishwa vitu vya uongo,hatujasikia uaongozi wa mahakama au hakimu husika anayeendesha kesi kukemea upotoshwaji huo wazi na mwisho wa siku baadhi ya wanahabari wasiyo makini wanaendelea na mchezo huo kwa kuzipotosha habari za kimahakama.

Kuhusu habari za kisiasa, baadhi ya wanahabari ambao hivi sasa wengi wao wameanza kushindwa kudhibiti mihemko yao kuhusu mapenzi yao na vyama fulani au ushabiki wa wanasiasa fulani,miongoni mwao wamekuwa wakiandika habari ambazo kwa maslahi yao binafsi na siyo ya taifa wamekuwa wakiandika habari ama wakiwanukuu au kuficha majina ya wanasiasa wanaowapenda wao au chama wanachokipenda wao ambazo mwisho wa siku zimekuwa zikileta misuguano baina ya vyama na jamii.

Baadhi ya vyombo vya habari wakati mwingine vimejikuta vinachapisha habari ambazo zinaisu taasisi fulani au mtu fulani bila hata ya kutoa nafasi kwa mhusika aliyetuhumiwa na taarifa hizo ambazo wakati mwingine hazionyeshi chanzo cha taarifa hizo ni nini, kujieleza.

Na baadhi ya wananchi hao wanaokumbwa na kadhia hiyo ya habari zinazowahusu kuchapishwa bila wao kupewa fursa ya kueleza anachokijua, wamekuwa wakikimbilia mahakamani kufungua kesi za kudai fidia za kashfa dhidi ya baadhi ya magazeti na wengi wao wamekuwa wakishinda kesi hizo lakini cha kusikitisha mwandishi wa habari za mahakama ambao uzipata nakala za hukumu za wananchi hao walioshinda kesi hizo unapofika kwenye chumba cha habari na kumweleza mwariri wako kuwa kuna mwananchi mmoja ameshinda kesi dhidi ya gazeti fulani,baadhi wahariri ukataa habari hiyo isichapishwe kwa kigezo kuwa wahariri walishafanya makubaliano yao ya siri ambayo yanakataza gazeti jingine lisiandike habari kuhusu gazeti jingine ambalo limetiwa hatiani na mahakama kwa kuchapisha habari fulani ya uongo.

Mfano huo hapo juu ni wa kweli na nimeushuhudia mimi binafsi.Na nina diriki kusema wazi kwamba kama kweli nyie wahariri wetu mliingia makubaliano hayo ya kifedhuli ambayo ni wazi kabisa yanakwenda kinyume na Ibara ya 18(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; ambayo inasema ‘kila mtu anayohaki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii;’.

Lakini kwa watu tunaotunza kumbukumbu kichwani ,tunajiuliza ni kwanini vyombo vingine vya habari vikifikishwa mahakamani,baadhi ya vyombo vingine ulipoti kesi hizo hadi zinapotolewa hukumu lakini ni kwanini vyombo vingine vinaripoti habari za kesi hizo tena hao hao wahariri wanaosema kuna azimio wamelipitisha la kutoandikana,wanaziruhusu habari za kesi hizo zichapishwe na gazeti analoliongoza?

Na kama hilo ni kweli wananchi tuwaulize hao wahariri wetu nani amewapa madaraka ya kuvunja ibara hiyo ya sheria?Kwa hiyo ni haki kwa vyombo vya habari kuchapisha habari zinazowashushia heshima na kuwaletea usumbufu baadhi ya wananchi zichapishwe lakini si haki kwa wananchi walioshuhiwa heshima habari zao za kulifungulia kesi gazeti kuchapishwa gazetini?

Sasa kumbe tunailaumu nini serikali kuwa inalindana wakati sisi vyombo vya habari ndiyo tunalindana katika kuficha makosa yetu ambayo tena mahakama ndiyo imeuanika udhahifu wetu kupitia hukumu mbalimbali?

Wakati baadhi ya vyombo vya habari vikichapisha na kutangaza habari ambazo hazina maadili,upotoshaji na uchochezi tunavishuhudia vyombo vya upelelezi vikishindwa kufurukuta kuvichukulia hatua vyombo hivyo ambavyo hali ilivyo hivi sasa wananchi wengi wamekuwa wakiamini kila kinachoandikwa na magazeti hata kama ni cha uongo kwani wazi hivi sasa watu wengi hawaudhulii mikutano ya adhara ya vyama vya siasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati vyama vingi vimeanzishwa hapa nchini na badala yake wamekuwa wakifuatia mikutano hiyo kupitia vyombo vya habari.

Sasa inapotokea na sisi vyombo vya habari tunashindwa kuripoti habari kwa usahihi bila kuweka ushabiki ,unakuta wananchi hao wakiamini habari hiyo.Lakini kwa sisi wajanja ambao tumeishang’amua uwendawazimu huo wa upotoshwaji unaofanywa na baaadhi ya wanataaluma wenzetu tena kwa maslahi binafisi, tumekuwa na utaratibu kuzichambua sana habari hizo na pia kuwauliza waandishi zaidi ya wanne walioudhulia ama mkutano huo ili kujua ukweli ni upi.

Ikumbukwe kuwa karibu nchi nyingi zilizowahi kukumbwa na machafuko ama ni wanasiasa au vyombo habari vilishiriki kikamilifu kuchochea machafuko hayo ambayo yalileta maafa.Na mfano mzuri ni machafuko yaliyotokea nchini Rwanda miaka ya 1990.Lakini baada ya vita kumalizika nchi hiyo ikapata kiongozi wa nchi ambaye ni Rais Paul Kagame ambaye aliahidi na akatekeleza kuwafikisha mahakamani waandishi,wanasiasa na wanajeshi waliohusika na machafuko hayo.

Na kweli tumeshuhudia wanajeshi ,waandishi wa habari waliochochea mauji ya Rwanda wakifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu dhidi ya Binadamu iliyopo mkoani Arusha wakipatikana na hatiani ya makosa ya uchochezi na hivi ninavyoandika makala hii wapo magerezani wanatumikia adhabu zao.Na kutokana na hukumu hizo ,inaelezwa waandishi wa Rwanda hivi sasa wanaheshimu na wanazingatia utaifa na maadili ya taaluma zao.

Hapa Tanzania bado hilo la vyombo vya habari vinavyochaposha habari za kichochezi kufikishwa kortini halijafanyika na siku likifanyika nitafurahi sana. Kwani hata Baba wa Taifa Hayati Julias Nyerere alishawahi kusema ; ‘ Uhuru bila nidhamu ni sawa na uwendawazimu na nidhamu bila uhuru ni sawa na utumwa’.

Nyerere hakuwa mpumbavu kutamka maneno hayo alikuwa anasema anachokimaanisha ambacho katika utawala huu wa Rais Kikwete ni kweli uhuru wa kutoa maoni,vyombo vya habari umepanuka lakini baadhi ya vyombo vya habari,wanasiasa na wananchi wameshindwa kabisa kuutumia uhuru huo kwa nidhamu na vyombo vya upelelezi, na taasisi nyingine za serikali zenye dhamana ya kukomesha hali hiyo vimelala usingizi wa pono hali inayosababisha taratibu baadhi ya vyombo vya habari na waandishi kujifanya vipo juu ya sheria.

Siku Jeshi la Polisi chini ya IGP-Said Mwema litakapashirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtka(DDP),Eliezer Feleshi kumfungulia kesi ya jinai mwandishi na mwariri kwa kosa la kuandika na kuchaposha habari za uchochezi mahakamani naamini na mwisho wa siku kama ushahidi wa jamhuri utaweza kuishawishi mahakama kuwatia hatiani watu hao, nafikiri ndiyo itakuwa mwanzo na mwisho wa wahariri,wanahabari wanaoandika habari za uchochezi ,uongo na zinaleta ,misuguano isiyoyalazima ndani ya jamii yetu.

Tunachokishuhudia sasa ni baadhi ya wananchi wanaodhani wamechafuliwa majina yao na vyombo vya habari ndiyo wamekuwa wakifungua wao wenyewe mahakamani kudai fidia.Hatua ambayo hivi sasa baadhi ya wahariri na waandishi hawaiogopi kabisa kwani wamekuwa wakisema mwisho wa siku mahakama ndiyo itaitia hatiani kampuni ,gazeti na mchapishaji na kuimaru imlipe fidia mlalamikaji huyo na siyo mwandishi aliyeandika habari iliyoleta madhara kwa mwananchi mwengine na ndiyo maana kila kukicha baadhi ya habari ambazo hazikidhi matakwa ya kitaaluma zimekuwa zikiendelea kuchapishwa na hakuna mamlaka ya serikali inayochukua hatua.

Fukuto la Jamii linapenda kuona Taifa la Tanzania linakuwa na wanataaluma wanaoheshimu taaluma zao na wanaofanyakazi zao kwa kuzingatia maadili na kanuni za taaluma zao.Hivyo sisi vyombo vya habari tuamke na kusimama kwenye misingi ya haki,ukweli na taaluma.Kwani tukae tukijua tunavyochapisha kwa makusudi habari ambazo hazijakidhi vigezo vya kitaaluma tunawaumiza wananchi wenzetu.

Tukumbuke viongozi wa madhebu ya dini zetu wamekuwa wakituasa kwa kutumia vitabu vya dini kwamba tutendeane yaliyomema na wengine hivi sasa wamekuwa wakituambia malipo ya matendo mema au mabaya tunayoyafanya tutalipwa hapa hapa duniani.Hivyo ni kheri mwenyezi mungu atulipe mema kutokana na matendo mema tunayowafanyia wenzetu.

Kwani kupitia habari zetu za uongo, majungu, fitna ambazo miongomini mwetu wamekuwa wakiziandika wakati mwingine zimekuwa zikisababisha watu kupoteza maisha, kufukuzwa kazi,kuamishwa vituo vya kazi ama kufukuzwa kazi hata kusambaratisha ndoa zao.

Kwa hiyo ni vyema na haki kila mwanahabari kwa nafasi yake akawa na hofu ya mungu, kuzingatia maadili ya taaluma yake, kuepuka kutumika na baadhi ya wanasiasa au maofisa wa seriakali ambao wamekuwa na magomvi binafsi maofisini kwao bila siye kujua sasa wanaona njia ya kumkomesha mbaya wake ni kwenye vyombo vya habari.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.