MAHAKAMA,KESI ZA EPA ZIMEWAKINAI?
Na Happiness Katabazi
NOVEMBA 4, 2008, serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, iliandika historia ya kuwafikisha watuhumiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya Feleshi kufungua kesi 14 za EPA kwa watuhumiwa ambao wengine ni maofisa wa BoT na wafanyabiashara maarufu nchini, ilitokana na tuhuma hizo kuibuliwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kelele za wananchi na wafadhili kupitia vyombo vya habari ambazo zilisababisha Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa wizi huo ambayo ilimshirikisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Dk. Edward Hosea na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.
Tume hiyo iliwahoji watuhumiwa na hatimaye ikaridhia watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani.
Binafsi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache hapa nchini ambao tumekuwa tukiziripoti kesi hizo tangu zilizofunguliwa hadi leo hii tunaendelea kuzifuatlia pale Mahakama ya Kisutu.
Nimejifunza mengi kutokana na ushahidi uliokwishatolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri na washitakiwa. Hivyo wakati kesi hizo zinafunguliwa kwa mpigo na kishindo mahakamani hapo Novemba 4, 2008, zilikuwa zinapangiwa kwa mahakimu wakazi wa mahakama hiyo katika hatua za awali.
Ilipofika hatua ya Jamhuri kuieleza mahakama upelelezi wa kesi hizo kuwa umekamilika, uongozi wa mahakama nchini enzi hizo ukiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Agustino Ramadhani uliweka utaratibu wa kuziendesha tofauti na kesi nyingine.
Uongozi ulieleza kuwa kesi zote za EPA zitasikilizwa kwa mtindo wa jopo ambapo jopo hilo linaundwa na mahakimu wakazi watatu. Na hilo lilifanyika kwani majopo yalipangwa na kesi hizo hadi sasa zinaendelea kusikilizwa kwa mtindo wa majopo na ikitokea hakimu mmoja katika jopo fulani hayupo, basi siku hiyo kesi haitaendelea kwa sababu jopo halijatimia.
Na ikitokea wakili wa mshitakiwa fulani akamwombea ruhusa mteja wake ili atoke nje ya Dar es Salaam, kama jopo halijatimia basi mahakimu hao hukataa kutoa ruhusa hiyo kwa maelezo kuwa hawawezi kutoa ruhusa au kutoa maamuzi mbalimbali katika kesi husika bila idadi ya jopo kutimia.
Si idadi ya jopo kutotimia kulisababisha kesi za EPA kuahirishwa, pia katizo la umeme lilisababisha, kwa sababu uongozi wa mahakama uliweka utaratibu mpya ambapo walitafutwa wataalamu wa kompyuta kutoka Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, ambao walikuwa wakija na kompyuta zao na kufunga vipaza sauti kurekodi mwenendo mzima wa kesi hizo.
Kwa kweli hilo lilikuwa likifanyika na mara kadhaa mahakama pia ilikuwa ikilazimika kuahirisha kesi hizo kwa sababu ya katizo la umeme kwani kompyuta nazo zilikuwa zikitumia umeme kurekodi mienendo ya kesi hizo 14 za EPA.
Wafanyakazi wa muda mrefu wa mhimili wa mahakama ambao si wasemaji walinieleza huo ni utaratibu mpya kufanyika katika Mahakama ya Kisutu tangu ilipoanza na wengine walidiriki kusema kuwa utumiaji wa teknolojia ya kompyuta kurekodi kesi hizo ulikuwa ni wa gharama na kwamba hautadumu kwa muda mrefu.
Kweli siku chache baadaye waandishi wa habari za mahakama tunaoweka kambi siku tano za jumaa mahakamani hapo tukaanza kuona kesi za EPA zinaendelea kusikilizwa bila ya teknolojia hiyo ya kompyuta kuwepo, na mashahidi wakawa wanafika kutoa ushahidi wao, hadi miaka inakatika sasa.
Binafsi nilijipa jukumu la kufanya uchunguzi wangu kujua kulikoni. Nilielezwa kuwa teknolojia hiyo haitakuwepo tena kwenye kesi hizo kwani ina gharama na kwamba hata upatikaji wa fedha wa kuprinti mwenendo wa kesi hizo uliokuwa ukirekodiwa kwa teknolijia hiyo hapo awali ulikuwa wa shida. Nikaishia kucheka.
Kwa mbwembwe hizo za mahakama na zile zilizokuwa zikionyeshwa na mahakimu wanaounda hayo majopo kwa sisi tuliobahatika kuzishuhudia tulisema kama kweli majopo hayo yataendelea na moyo huo, tulibashiri huenda kesi hizo zitachukua muda mfupi kumalizika.
Bado nakumbuka siku moja tukiwa mahakamani hapo, jopo moja linalounda kesi moja ya EPA inayomkabili mshitakiwa Farijala Hussein, lilikataa ombi la Farijala liloomba kesi hiyo iarishwe ili aende nyumbani kupumzika kwakuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa figo na hivyo amemeza dawa zinazomsababishia aende chooni mara kwa mara kujisaidia haja ndogo.
Jopo hilo liliendelea kupokea ushahidi wa shahidi wakati Farijala akiwa kizimbani na mara kwa mara alikuwa akinyoosha kidole juu kuliomba jopo hilo limruhusu ende kujisahidia haja ndogo na kisha kurejea kizimbani.
Hakuna ubishi kwamba upande wa Jamhuri katika kesi za EPA umejitahidi kadiri ya uwezo wake kuhakikisha unawaleta mashahidi wake bila kuchoka ukilinganisha na kesi nyingine ambapo upande wa Jamhuri umekuwa ushindwa kuwaleta mashahidi wake kwa wakati.
Na katika kesi za EPA nitakuwa sijautendea haki upande wa Jamhuri kama sitaupa pongezi kwa kuweza kuwaleta mashahidi wao bila visingizio na Jamhuri ingekuwa ikifanya hivyo hata kesi zake katika mahakama zote nchini, wananchi tusingekuwa tukiilaumu.
Kwa muktadha huo hapo juu basi leo Fukuto la Jamii, limesukumwa kuueleza umma na kuuliza uongozi wa mahakama kwamba kulikoni ile kasi ya baadhi ya mahakimu wanaounda kesi za EPA ya kufika mahakamani bila kukosa hata kama kesi hizo zimekuwa zikija kwaajili kusikilizwa au kujatwa, kupungua? Au kesi za EPA zimewakinai?
Haya ninayoaandika sio nimesimuliwa, ninayashuhudia kila kukicha na ndio maana leo nimelazimika kuandika makala hii kwa umma na mahakimu wao ili waweze kutueleza kuwa huenda kesi za EPA zimewakinani ndiyo maana siku hizi hata kesi hizo wakizipangia tarehe, itakuja kwaajili ya upande wa Jamhuri au utetezi kuwasilisha majumuisho ya washitakiwa wana kesi ya kujibu na mashahidi kuendelea kutoa ushahidi wao, huku baadhi ya mahakimu wanaounda majopo wakiwa hawaonekani.
Na matokeo yake waandishi wa habari za mahakama siku hizi tumekuwa tukishuhudia hakimu mwingine kabisa ambaye hata kwenye yale majopo 14 yanayosikiliza kesi 14 za EPA hayupo, akifika ndani ya chumba cha mahakama huku akitabasamu anaanza kueleza kuwa amepata taarifa kutoka kwa wana jopo (mahakimu wakazi) wanaosikiliza kesi husika kwamba hawapo hivyo yeye amekuja kuiahirisha kesi hiyo na kupanga tarehe nyingine.
Na ushahidi mmoja wapo unaounga mkono hoja yangu hiyo ni lile tukio lililotokea Aprili 29 mwaka huu. Ahadi iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu Januari 26 mwaka huu, kuwa Aprili 29 ingetolewa hukumu ya kesi ya wizi wa fedha za EPA inayomkabili Mweka Hazina wa (CCM), Rajabu Maranda (53) na mpwa wake, Farijala Hussein, ilishindwa kutekelezwa kwa vitendo.
Jopo la mahakimu wakazi linaloundwa na Saul Kinemela, Focus Bambikya na Ilvin Mugeta, ambalo ndilo lilikuwa likisikiliza kesi hiyo ya jinai namnba 1161/2008 hawakuweza kutokea mahakamani.
Hivyo Mahakama ya Kisutu ililamizimika kumtuma Hakimu Mkazi Musthapher Siyani, ambaye hajawahi kusikiliza kesi za EPA zilizofunguliwa na serikali, kuja kuahirisha hukumu pamoja na kesi nyingine tano za EPA zinazowakabili watuhumiwa hao na wengine ambao ni Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel ‘na wenzake. Akitoa sababu ya kushindwa kusomwa kwa hukumu hiyo, Hakimu Siyani alisema amepata taarifa kuwa kiongozi wa jopo hilo Saul Kinemela yupo nje ya Dar es Salaam.
Na kweli baada ya uchunguzi wa Fukuto la Jamii ulibaini Kinemela alifuatana na Waziri wa Kazi na Ajira Gaudensia Kabaka mkoani Songea kwa ajili ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Usalama Mahala pa Kazi.
Hata hivyo kuahirishwa kwa hukumu hiyo si siri kumeacha maswali mengi kwa baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakamani hapo wakishangazwa na kitendo cha mahakimu wote watatu wanaounda jopo na wanaosikiliza kesi nyingine tano kushindwa kutokea mahakamani hadi kufikia hatua ya kuahirisha kesi zao licha ya kuwa kesi moja namba 1163/2008 inayomkabili Maranda na Farijala kuja kwa ajili ya kufanyiwa majumuisho ya washitakiwa hao kama wana kesi ya kujibu au la.
Swali ambalo tumekuwa tukijiuliza wananchi, je, wakati jopo hilo linapanga tarehe ya hukumu kiongozi huyo wa jopo Kinemela hakuwa akijua tarehe hiyo ya hukumu ni siku ya maadhimisho hayo?
Kama kweli hukumu imeishaandaliwa ni kwanini isitolewe idhini ya kusomwa hukumu hiyo na wana jopo wenzake bila ya yeye kuwepo? Sasa kama ikitokea tena hakimu mwingine anayeunda jopo hilo Mei 23 mwaka huu ambapo kesi hiyo imepangwa kusomwa, akiwa amesafiri, hukumu hiyo haitasomwa tena kwa sababu mwanajopo mmoja amesafiri?
Ni hukumu ngapi zinaandaliwa na mahakimu wengine lakini kutokana na hakimu aliyeiandaa hayupo anatoa idhini hukumu hiyo isomwe na hakimu mwingine na kweli hukumu hiyo inasomwa?
Na ushahidi wa hukumu zilizoandaliwa na majaji wengine na kusomwa na msajili ni pamoja na hukumu ya rufaa ya mwanamuziki wa dansi, Nguza Vicking na wanawawe ambayo ilisikilizwa na hukumu hiyo kuandikwa na jopo la majaji watatu, Nataria Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk wa Mahakama ya Rufani nchini, ambapo hukumu hiyo ilikuja kusomwa na Msajili Neema Chusi kwa niaba ya jopo hilo.
Hukumu nyingine iliyosomwa bila idadi ya jopo kutimia ni hukumu ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Mahalu, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2008, ambapo Oktoba 4 mwaka jana, Jopo la majaji watatu lililokuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakhi Jundu, Agustine Mwarija na Projest Rugazia lilisoma hukumu yake bila Jaji Rugazia kuwepo mahakamani ambapo Mahakama Kuu ilisema inakubaliana na Mahalu kuwa kifungu cha 36 (4)(e) Sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002, kinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Na mahakama katika hukumu hiyo ilitoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku hiyo ambayo hukumu ilitolewa Oktoba 4 mwaka 2010 iwe imekifanyia marekebisho kifungu hicho cha sheria.
Kwa hiyo mahakimu wanaosikiliza kesi za EPA na kesi nyingine kama za matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara watambue kuwa wananchi kupitia vyombo vya habari watu wanazifuatilia kwa karibu kesi hizo ili waweze kujua hatima yake kwa kuwa uchunguzi wa kesi za EPA uliwekewa utaratibu wa aina yake tofauti na kesi nyingine.
Fedha nyingi za walipa kodi zilitumika katika ile tume iliyoundwa na rais hivyo wananchi hao ambao kodi zao zilitumika wana haki ya kufuatilia hatima ya kesi hizo.
Sasa inapotokea matukio kama haya ya baadhi ya mahakimu wanaounda kesi hizo kupunguza kasi ya kuudhuria kesi hizo na vyombo vya habari vikaripoti matukio hayo, itasababisha Watanzania kutanguliza hisia mbaya kuhusiana na kesi hizo ya EPA hata kama ushahidi wa hisia hizo walizonazo hawana.
Mahakimu wanaosikiliza kesi hizo warejeshe ile kasi yao ya zamani ya kuhudhuria kesi hizo na waachane na kasumba ya kuwatuma mahakimu wasiosikiliza kesi hizo kuja kuahirisha kesi zao, licha ya kwamba hakuna sheria inayokataza hilo.
Kama uongozi wa mahakama nchini hautasimama vema kuhakikisha majopo hayo yanahudhuria kesi zao bila kukosa, basi kuanzia sasa tuanze kuliwekea mashaka lile tamko la Jaji Kiongozi Fakhi Jundu, kwa umma kwamba kesi za kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 zimewekewa utaratibu wa kusikilizwa na majaji kutoka mikoani na kwamba zitakuwa zimemalizika ndani ya miaka miwili tangu zilipofunguliwa.
Kesi hizo za uchaguzi ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka jana zimekuwa zikisikilizwa na kuamuliwa na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kinyume na tamko hilo kwamba majaji watakaosikiliza kesi hizo watatoka mikoani.
Na katika kesi hizo, hakuna hata kesi iliyofikiwa ya shahidi hata mmoja kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake.Tusubiri tuone.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716-774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Mei 3 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment