Header Ads

HUKUMU KESI YA EPA: MAHAKIMU WAINGIA MITINI

Na Happiness Katabazi

ILE ahadi iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ya Januari 26 mwaka huu, kwa umma kwamba jana ndiyo ingetoa hukumu katika kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania , inayomkabili Mweka Hazina wa (CCM) Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda (53) na mpwa wake Farijala Hussein imeshindwa kutekelezwa kwa vitendo.


Jopo la mahakimu wakazi mahakimu wakazi, Saul Kinemela, Focus Bambikya na Elvin Mgeta, ambalo lilikuwa likisikiliza kesi hiyo ya jinai Na 1161/2008 jana hawakuweza kutokea mahakamani.

Hivyo Mahakama ya Kisutu ililazimika kumtuma Hakimu Mkazi Musthapher Siyani, ambaye hajawahi kusikiliza kesi za EPA zilizofunguliwa na serikali, kuja kuahirisha hukumu hiyo pamoja na kesi nyingine tano za EPA zinazowakabili watuhumiwa hao wengine ambao ni Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel na wenzake.

Akitoa sababu ya kushindwa kusomwa kwa hukumu hiyo jana, Hakimu Siyani alisema amepata taarifa kuwa kiongozi wa jopo la mahakimu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo, Saul Kinemela yuko nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Hukumu hii leo haitaweza kusomwa kwa sababu kiongozi wa jopo Saul Kinemela aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo yuko nje ya jiji hili kwenye kazi nyingine hivyo naiahirisha kesi hii ambayo leo (jana) ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu hadi Mei 23 na mahakama hii imekubali ombi la washtakiwa hao kwenda mkoani Kigoma, ” alisema Hakimu Siyani.

Baada ya hakimu huyo kusema hayo, ndugu na jamaa wa washtakiwa hao ambao walifika mahakamani hapo kufuatilia hukumu hiyo walionekana kuwa na sura za furaha na kusalimiana na washtakiwa huku wapiga picha wakimzonga Maranda ili wampige picha ambapo alisimama kwa takriban dakika moja huku akionyesha sura yake kwa wapiga picha hao ambao walimpiga picha watakavyo na kisha aliwauliza kama wameishamaliza kumpiga picha nao wakamjibu tayari wamemaliza kazi yao hali iliyosababisha watu kuangua vicheko mahakamani.

Hata hivyo kuahirisha huko kwa kesi hiyo kumeacha maswali mengi kwa baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakamani hapo wakishangazwa na kitengo cha mahakimu wote watatu wanaounda jopo na pia wanaosikiliza kesi nyingine tano kushindwa kutokea mahakamani kuahirisha kesi hizo tano hadi Mei 27.

Novemba 24, 2008 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Eliezer Feleshi aliwafikisha mahakamani hapo Maranda na Farijala kwa kesi nne tofauti ikiwemo kesi hiyo ambayo ilipaswa itolewe hukumu jana kwamba washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka zilizoghushiwa Benki Kuu zilizoonyesha kampuni yao ya Kiloloma & Brothers ambayo hata hivyo haijawahi kusajiliwa kwa msajili wa makampuni nchini (BRELA), kwamba imepewa idhini na kudai deni la kampuni ya nje ya M/S BC Cars Export huku wakijua si kweli.

Itakumbukwa kuwa serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) Feleshi iliwaburuza mahakamani watuhumiwa wa wizi katika akaunti ya EPA, baada ya tuhuma hizo kuibuliwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoo.

Kelele za wananchi na wafadhili, zilisababisha Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa wizi huo ambayo ilimshirikisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP-Said Mwema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dk. Edward Hosea na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa sasa amestaafu, Johnson Mwanyika.

Tume hiyo iliwahoji watuhumiwa na hatimaye kuwafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosiu, Aprili 30 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.