Header Ads

KESI YA JERRY MURRO YAPATA HAKIMU MPYA


Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC1,Jerry Murro na wenzake kwa mara nyingine tena jana alishindwa kuanza kujitetea katika kesi inayowakabili ya kula njama,kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 10 toka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage kwasababu kesi hiyo imepata hakimu mkazi mpya aitwaye Frank Leonard Moshi.


Hakimu Mkazi Frank Moshi ambaye ni hakimu mgeni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, alisema jana asubuhi ndiyo uongozi wa mahakama hiyo umempatia jalada la kesi hiyo ambalo linaonyesha kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya washtakiwa wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Majura Magafu ambapo upande wa Jamhuri unawakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP),Stanslaus Boniface kuanza kujitetea.

“Kesi hii tangu awali ilikuwa ikisilizwa na hakimu mwingine lakini leo uongozi wa mahakama hii ndiyo umenipatia jalada la kesi hii ambalo linaonyesha kweli leo(jana) inakuja kwaajili ya washtakiwa kuanza kujitetea …..sasa basi kwa kuwa leo ndiyo nimepewa jalada na mimi ndiye nitaendelea kusikiliza kesi hii naomba mnipatie muda nilisome kilichokuwa kikiandikwa na hakimu mwenzangu tangu kesi hii ilipoanza ili nielewe kwahiyo washtakiwa hawataanza leo kujitetea kwakuwa sijalisoma jalada na hivyo naiarisha hadi Juni 7 mwaka huu, ambapo washtakiwa wataanza kujitetea”alisema Hakimu Frank Moshi.

Machi 29 mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe kesi hiyo ilikuja kwaajili ya Murro na wenzake kuanza kujitetea lakini hawakuweza kuanza kujitetea kwasababu mshtakiwa wa kwanza Murro alikuwa safarini mkoani Kilimanjaro kwaajili ya kuudhuria msiba wa baba yake mdogo.

Machi nane mwaka huu,hakimu Mirumbe alitoa uamuzi wa kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu katika kesi hiyo ikiwa ni dakika chache ya shahidi wa sita wa Jamhuri D/C Koplo Lugano Mwampeta kumaliza kutoa ushahidi wake na Naibu Mkurugenzi wa Mashataka Stanslaus Boniface kuiambia mahakama kuwa huyo ndiye alikuwa shahidi wao wa mwisho na kwamba upande wa Jamhuri unatangaza kufunga ushahidi kwa upande wao.

Hakimu Mkazi Mirumbe ambaye ndiye aliyeanza kusikiliza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo na Jamhuri Februali 15 mwaka jana, dhidi ya Murro, Edmund Kapama na Deogratius Mugasa ambao Januari mwaka jana washtakiwa hao walitenda makosa ya kula njama,kushawishi na kuomba rushwa ya shillingi milioni 10 kutoka kwa Wage.Kati ya mashtaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashtaka mawili,ameamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwaajili ya kupangiwa kazi nyingine.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 3 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.