Header Ads

JAMHURI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA SAMAKI WA MAGUFURI

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya uvuvi haramu katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi maarufu kesi ya ‘Samaki wa Magufuri’ inayowakabili raia 36 wa kigeni umefunga ushahidi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Mganga anayesaidiwa na Prosper Mwangamila mbele ya Jaji Agustine Mwarija alieleza mahakama hiyo kuwa mashahidi wake 13 walifika mahakamani hapo kutoa ushahidi wameona ushahidi wao umetosha na hivyo wamefikia uamuzi huo wa kuifunga kesi yao.

‘Mheshimiwa jaji na mahakama yako tukufu leo tunayo furaha kuiarifu mahakama hii kuwa upane wa Jamhuri tumefunga rasmi kesi yetu kwani tumejiridhisha mashahidi 13 tuliwaleta mahakamani hapa kutoa ushahidi wanatosha kujenga kesi yetu hivyo tunaiachia mahakama iendelee na kazi yake”alisema Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Mganga.

Kwa upande wake Jaji Mwarija alisema anakubaliana na maelezo hayo na ana uamuru upande wa utetezi katika kesi hiyo unaowakilishwa na mawakili wa kujitegemea John Mapinduzi na Ibrahim Bendera kuwasilisha majumuisho ya kesi hiyo ya kuiomba mahakama iwaone wateja wao hawana kesi ya kujibu Juni 6 mwaka huu.

Aidha pia Jaji Mwarija aliuamuru upande wa Jamhuri nao uwasilishe majumuisho yao ya kuwaona washtakiwa wanakesi ya kujibu kwa njia yam domo Juni 9 mwaka huu.

Machi 2009 walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka makosa ya kukamatwa wakiwa kwenye meli ya Tawariq 1 wakifanya uvuvi katika kina kirefu bila leseni ya uvuvi na kisha kuchafua mazingira katika kina kirefu cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tangu kipindi hicho hadi leo washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwasababu mahakama kuu imewanyima dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 31 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.