Header Ads

KESI YA MAHALU:MKAPA AKUNJUA MAKUCHA


.UTETEZI WAKE WAMGUSA RAIS KIKWETE
.AUWASILISHA RASMI MAHAKAMANI DAR

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE utetezi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, umetua rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam.


Mkapa ambaye ni shahidi wa pili wa kesi hiyo alitoa utetezi huo ambao unaweza kuandika historia mpya katika mwenendo wa kesi nchini, kupitia kiapo chake ambacho kimewasilishwa mahakamani na wakili wa mshtakiwa huyo, Mabere Marando.

Katika moja ya vipengele 13 vya kiapo hicho, pasipo kutaja jina, maelezo ya kiongozi huyo mstaafu yanamgusa Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati Mkapa akiwa madarakani alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Hiyo inakuwa ni mara ya kwanza kwa rais mstaafu, kutoa utetezi mahakamani kwa kesi inayomgusa mmoja wa waliokuwa wateule wake wakati akiwa madarakani.

Kesi hiyo Namba 1/2007 ambayo Mahalu anashtakiwa pamoja na Grace Martin inasikilizwa na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilivin Mugeta.

Katika kesi hiyo, Mahalu na Martin wanatuhumiwa kwa wizi wa shilingi bilioni tatu katika ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome.

Katika hati ya kiapo chake cha Machi 31 mwaka huu, ambayo imeandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Nyaraka (The Registration of Documents Act, Cap. 117 of 2002), Mkapa anaeleza kuwa kila kilichofanywa na Mahalu kilikuwa sahihi na kilikuwa na baraka ya serikali aliyokuwa akiingoza toka mwaka 1995-2005.

Ushahidi huo wa rais Mkapa ambao Tanzania Daima inayo nakala yake, umeorodhesha maelezo yake yaliyoainishwa katika vipengele 13.

Mkapa katika utetezi wake huo anadai kuwa mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi lililoko katika mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Rome ulizingatia sera ya serikali ya upatikanaji au ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi na makazi na kwamba ulizingatia maslahi ya taifa.

Hati hiyo ya kiapo ambayo tayari wakili Marando amesema ameishaiwasilisha pia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Eliezer Feleshi, inaanza kwa kusema, “Mimi Benjamin Mkapa, mtu mzima, Mkristo, mkazi wa Dar es Salaam, ninaapa kama ifuatavyo, ’nilikuwa Rais mtendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viliwili mwaka 1995-2005 na nina uhakika wa yote haya nitakayosema ndani ya kiapo hiki.’

Katika kiapo hicho Mkapa anadai pia kuwa alifahamishwa na watendaji wa serikali aliyokuwa akiingoza jinsi mchakato uliofanyika na ripoti za uthamini wa serikali zilizotumika katika kufikia hatua ya kununua jengo hilo la ubalozi.

Anadai kuwa tathmini ya jengo hilo ambalo Mahalu anadaiwa kufanya udanganyifu na wizi kwa kulipa fedha kinyume na ilivyotajwa katika mkataba ambayo ilifanywa na serikali ya awamu ya tatu kupitia wizara mbili tofauti, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Ardhi na Maendeleo Mijini.

Anaendelea kudai kuwa, anatambua kuwa ripoti ya serikali ya uthamini wa jengo hilo iliandaliwa na Wizara ya Ujenzi kwa kiwango cha dola za Marekani milioni tatu na Wizara ya Ardhi kwa thamani ya euro milioni 5.5.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa wa aina mbili, mmoja ni rasmi na mwingine wa kibiashara na kuongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu ya serikali ya Italia na kuwa hilo lilifanyika kwa baraka za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Utaratibu kama huo wa mikataba miwili ushawahi kufanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ambapo ilionekana haja kwa kuzingatia maslahi ya taifa kwanza....na kuwa ni mimi ndiye niliyezindua jengo hilo la ubalozi Februari 23 mwaka 2003,” anadai Mkapa.

Shahidi huyo wa Mahalu anadai pia kuwa kwa mujibu wa kiapo chake anakumbuka vyema taarifa ya serikali iliyotolewa bungeni Agosti 3 mwaka 2004 iliyosema na kuthibitisha kuwa taratibu zote zinazohusiana na manunuzi ya jengo kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, zilifuatwa na kwamba muuzaji wa jengo hiilo alilipwa fedha zote.

Kumbukumbu ambazo gazeti hili linazo zinaonyesha kwamba, Agosti 3, 2004, Kikwete alitoa maelezo bungeni kuhusu utata uliokuwapo awali kuhusu ununuzi wa jengo hilo la ubalozi.

Kikwete katika maelezo yake hayo ambayo yako pia katika kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) anaeleza, “Mheshimiwa Naibu Spika mwaka 2001/02 wizara ilinunua jengo la ubalozi counsel katika ubalozi wa Rome katika jitihada za kuondokana na tatizo la kupanga majumba ya watu huko nje na pia kupunguza gharama za kuendelea kulipa pango la nyumba kila mwaka.

“Ununuzi wa jengo hili ulifuata taratibu zote za manunuzi ya majengo ya serikali kwa kuzishirikisha wizara za ujenzi, ardhi na maendeleo ya makazi pamoja na Wizara ya Fedha.

“...Jengo lilifanyiwa tathmini na wataalamu wetu na kukubaliana na ununuzi wa Euro 3,098,781.40 tarehe 6 Machi 2002 fedha za awamu ya kwanza katika ubalozi wa Rome zilipelekwa nazo zilikuwa shilingi 700,000,000 tarehe 28 Juni 2002 zilipelekwa shilingi 120, 000,000.

“Mwishoni mwa tarehe 26 Agosti mwaka 2002 zilipelekwa shilingi 1,000,000,000 jumla ya fedha zilizokuwa zimepelekwa zikafikia shilingi 2,900,000,000 na baada ya hapo ubalozi wetu ulitekeleza taratibu zote za ununuzi wa jengo na kumlipa mwenye nyuma kiasi hicho cha fedha,” alieleza Kikwete.

Akimwelezea Mahalu katika utetezi wake, Mkapa alidai katika kipindi chote alichokuwa rais wa nchi alifanya kazi na mshtakiwa huyo katika nyadhifa mbalimbali za utumishi wa umma na kwamba mshtakiwa huyo ni mtu wa tabia njema, mkweli, mwaminifu na mchapaji kazi.

Mkapa anahitimisha utetezi wake kwa kueleza kuwa, kutokana na mwenendo huo wa kutukuka, Rais wa Italia alimpatia moja ya tuzo za heshima yenye hadhi ya juu kabisa ya taifa hilo Profesa Mahalu, muda mrefu baada ya balozi huyo kuwa ameshaondoka nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha mahakamani ushahidi huo wa Mkapa jana, wakili Marando alisema mteja wake anakusudia kupeleka jumla ya mashahidi 10.

Mashahidi hao ni mteja wake (Mahalu), Mkapa, Rais Jakaya Kikwete, kwani wakati akinunua jengo hilo ndiye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ndiye alimpa mteja wake nguvu ya kisheria ya kuendelea na ununuzi wa jengo hilo, aliyekuwa waziri wa Ujenzi wa John Magufuli na mashahidi wengine na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba ambaye pia anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bil. 11.7.

Kuwasilishwa kwa hati ya kiapo cha Mkapa mahakamani hapo, kumekuja baada ya Hakimu Mkuu Mfawidhi Ilvin Mugeta kusema kuwa yeye ndiye amejipangia kusikiliza utetezi wa washtakiwa hao Aprili 28 mwaka huu.

Hatua ya Hakimu Mugeta kusikiliza utetezi huo inakuja baada ya Machi 28 mwaka huu, Jaji Sivangilwa Mwangesi ambaye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo tangu awali kujitoa baada ya mawakili wa washtakiwa kuwasilisha sababu sita za kumwomba ajitoe kwa sababu kukosa imani naye Machi 25 mwaka huu.

Mapema mwaka 2007, Jamhuri kupitia mawakili wake toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln na Ponsian Lukosi iliwafikisha mahakamani hapo kwa mara ya kwanza washtakiwa hao kwa makosa ya uhujumu uchumi, wizi wa zaidi ya euro milioni mbili wakati wakisimamia ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome nchini Italia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 6 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.