Header Ads

HEKO SPIKA MAKINDA,NDUGAI,DK.KASHILILAH


Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni Spika wa Bunge Anne Makinda, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah na Naibu Spika Job Ndugai kwa wakati tofauti waliviambia vyombo vya habari kuwa wabunge wengi kutofahamu kanuni za uendeshaji wa Bunge ndiyo ilikuwa chanzo cha mivutano katika kikao cha 10 cha Bunge.


Wameyasema hayo kutokana na wananchi mbalimbali pamoja na taasisi za kiraia kujitokeza kukosoa mambo yaliyofanyika katika kikao cha Bunge lililopita.
Dk. Kashililah anasema uwepo wa wabunge vijana kumelifanya Bunge hilo kuonekana kama ni la wanafunzi.

Katika Bunge hilo, baadhi ya wabunge walionekana kwenda kinyume na kanuni za Bunge na kuzusha malumbano na kurushiana vijembe bila kuheshimu nyadhifa zao.
Baadhi ya wabunge hao walikwenda mbali na kutaka milango ya ukumbi ifungwe ili waweze kuchapana makonde.

Kwa upande wake Makinda ambaye amefiwa na mama yake mzazi na Fukuto la Jamii linampa pole kwa kuondokewa na mama yake, aliunga mkono hoja ya Kashililah kuwa wabunge wengi hawajui kanuni.

Anasema Bunge limeshatenga muda fulani katika Bunge lijalo kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wabunge hao ili waweze kuzifahamu kanuni za Bunge.

Naye Naibu Spika, Job Ndugai, anasema kuna baadhi ya wabunge wanawake wanavaa nguo fupi, zisizoendana na utamaduni wa Bunge hilo.

Naamini hilo likifanyika la kuwapatia mafunzo wabunge matatizo hayo yatakwisha.

Binafsi nilibahatika kuzunguka Mikoa yote nchini na Zanzibar kwaajili ya kampeni.
Awali kulikuwa na lundo la tuhuma kutoka kwa baadhi ya wananchi na wanachama wa chama alichotoka mbunge husika kuwa amepitishwa kwenye kura za maoni na chama chake kwa mbinu chafu.

Leo Fukuto la Jamii linapenda kutoa pongezi kwa Spika Makinda na Katibu wa Bunge Dk. Kashililah kwa ujasiri wao wa kuzungumza kile kilichomo ndani ya akili na mioyo yao kwamba wabunge ambao tumewachagua wakatuwakilishe bungeni na wakatutungie sheria, wengi wao hawataki kujisomea.

Na kwamba viongozi hao wa Bunge wanawaongoza baadhi ya wabunge ambao hawafahamu kanuni ingawa walishapewa. Ni aibu sana.

Nasema hawataki kujisomea, kwa sababu tumeambiwa na Dk. Kashililah kwamba muda mrefu Ofisi ya Bunge ilishawapatia wabunge kanuni za Bunge ili wazisome na wazielewe.

Lakini tulichokishuhudia katika kikao cha 10 ni wazi kabisa baadhi ya wabunge hawana ule utamaduni wa kupenda kujisomea na kuelewa kanuni au taratibu zinazopaswa ziwaongoze wao katika shughuli za kibunge.

Ushahidi wa hilo ni vile vitendo vya ubwatukaji ovyo na kutoa kauli za kuchochoea uvunjifu wa amani bungeni, vitu vilivyokuwa vikitolewa na baadhi yao.
Siku zote viongozi wetu na wasomi wamekuwa wakieleza jamii kuwa elimu haina mwisho na binafsi nakubaliana na msemo huo.

Sasa inapotokea Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye hajui kanuni za kumuongoza yeye akiwa bungeni na jinsi Bunge linavyoongozwa, hivi ataweza kusimama mbele ya wapiga kura wake na kuwataka wasome kwa bidii kwa sababu elimu haina mwisho?
Ndiyo maana Fukuto la Jamii linatoa pongezi kwa Spika Makinda na Dk. Kashililah kwa kutueleza ukweli kwamba wale wabunge wanaowaongoza wengi hawafahamu kanuni.

Ni nadra sana kwa viongozi wa taasisi fulani kuandika udhaifu wa wafanyakazi wao au watu wanaowaongoza lakini viongozi hao wamekuwa wakweli.

Hivi ndivyo viongozi wa taasisi nyingine wanatakiwa wawe pindi wanapobaini watendaji wao wana udhaifu katika eneo fulani na kisha kutafuta njia ya kuweza kuutokomeza udhaifu huo.

Kwa sisi waumini wa fani ya sheria tumekuwa tukijiuliza maswali mara kwa mara, ni kwanini huu utaratibu wa kuwaruhusu wabunge wetu ambao wengi hawajasoma sheria kutunga sheria?

Na ndiyo maana sheria nyingi zilizotungwa na Bunge, huku zikisainiwa na rais zimekuwa zikilalamikiwa kuwa ni sheria mbaya na baadhi ya vipengele vyake vinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Baadhi ya taasisi za kutetea haki za binadamu na wanaharakati wamekuwa wakilalamikia vipengele hivyo Mahakama Kuu, ambayo imekuwa ikivitengua.

Sasa tutegemee tutungiwe sheria zisizo kandamizi wakati tayari Spika Makinda na Katibu wa Bunge wameishatueleza kwamba wabunge wengi hawajui kanuni ingawa Bunge lilishawapa vitabu vya kanuni ili wajisomee?

Hivi wananchi watamsikiliza kweli mbunge huyo au watapuuza mafundisho yake? Wananchi wamewachagua wabunge wao wakawawakilishe bungeni kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na mambo mengi ya msingi lakini hakuna mpiga kura aliyempigia kura mbunge wake ili aende bungeni kwa ajili ya kwenda kubwatuka na kutaka milango ifungwe ili wapigane makonde.

Mbunge anayeshindwa kusema matatizo na kero za wananchi wake ndani ya Bunge ili serikali isikie kilio hicho na kisha iziweke kero hizo kwenye mpango wa kuzitatua, mbunge wa aina hiyo hafai tena kupewa kura na wananchi.
Bunge ni eneo linaloheshimiwa na wananchi, kwani sheria zote hutungwa na kurekebishwa huko.

Ifike mahala wapiga kura tujiulize, zile kero zote tulizowapatia waliokuwa wagombea ubunge kwenye majimbo yetu na sasa wabunge, wanaziwasilisha sehemu husika zitatuliwe?
Maana hivi sasa ninachokiona kuna fasheni mpya imeanza kutumiwa na baadhi ya wabunge wanaotaka umaarufu wa ‘chapuchapu’, wa kujitapa kuwa Bunge lijalo atawasilisha hoja binafsi au kuuliza swali kuhusu ufisadi wa mfano wa Kampuni ya Meremeta na Kagoda ambapo ukiitazama hiyo hoja haimo hata kwenye vipaumbele vyake.

Na maswali hayo ya kuhusu ufisadi wa kampuni hizo yalishatolewa majibu na serikali bungeni kuwa upelelezi bado unaendelea.

Sasa basi, mbunge huyo anaacha kuwasilisha kero za wananchi wake kwanza anapewa nafasi ya kuchangia na Spika, yeye anauliza swali kuhusu ufisadi huo, wakati mbunge huyo pia alikuwa ana nafasi kabla ya vikao vya Bunge kuanza mjini Dodoma au kumalizika kwenda kuonana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba au kumwandikia barua ya kumuuliza swali hilo na angejibiwa kwa sababu hivi sasa Jeshi la Polisi nchini lina mabadiliko makubwa ya kiutendaji, linaendeshwa kisomi na urasimu uliokuwapo unaendelea kutokomezwa.

Ni haki yao wabunge kuuliza maswali ya aina hiyo kuhusu kile wanachodai kuwa ni ufisadi mkubwa, lakini tunawaomba wakumbuke yale waliyoyaahidi wakati wa kampeni kwamba watahakikisha wanafikisha matatizo ya wapiga kura wao kama uhaba wa maji, kukosekana dawa hospitalini, matatizo ya walimu, huduma mbovu kwa wajawazito, ujenzi wa barabara na madaraja na maji.

Maana matatizo hayo ndiyo yamekuwa yakiwakabili wapiga kura lakini hivi sasa tunachokishuhudia baadhi ya wabunge utawasikia wakiuliza maswali ya nyongeza yasiyo na tija katika majimbo yao au kuwasilisha hoja binafsi ambazo binafsi nadiriki kusema hazina faida kabisa kwa wapiga kura wao ambao kura zao ndizo zilimfanya mbunge anayeuliza maswali ya aina hiyo kuingia bungeni.

Si dhamira yangu kutaka kuwafunga midomo wabunge wetu, la hasha! Napendekeza sasa hayo maswali kuhusu ufisadi katika kampuni fulani fulani wabunge mliochaguliwa na wananchi muwaachie wabunge walioteuliwa na rais au wabunge wa viti maalumu ambao hawana majimbo, wakijisikia waulize maswali ya aina hiyo na nyie wabunge mliochaguliwa na wananchi muwe mnauliza maswali yanayohusu majimbo yenu ili serikali iweze kusikia kwa mapana kero za wananchi na kuzitatua.

Binafsi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule wa mwaka 2010 nilibahatika kuzunguka majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, nilijifunza mengi na kujionea mengi lakini kikubwa nilichojifunza ni kwamba wabunge ambao mara kwa mara wamekuwa vinara ndani ya Bunge kuuliza maswali ambayo wakati mwingine hayahusu majimbo yao au kuwasilisha hoja ambazo hazina masilahi kwa taifa, majimbo yao yapo nyuma sana kimaendeleo.

Na wale wabunge wenye hulka ya kukaa kimya bungeni majimbo yao yamepiga hatua za kimaendeleo.

Mfano mmoja wapo wa wabunge ambao hawana hulka ya kuzungumza bungeni ni Mbunge wa jimbo la Igunga (CCM), Rostam Aziz, lakini ukilizunguka jimbo lake utakubaliana nami kwamba licha ya kukaa kimya bungeni, lakini jimbo lake limeendelea sana kwa mawasiliano ya simu, nguzo za umeme ambazo zimetanda katika vijiji vingi; pamoja na kujengwa shule nyingi za msingi na sekondari, ukilinganisha na baadhi ya majimbo yanayoongozwa na wale wabunge wazungumzaji wazuri bungeni.

Ikumbukwe kuwa wapiga kura walivyowapigia kura wabunge wao walikuwa wana imani wabunge hao ndio watakwenda bungeni na sehemu nyingine kuwasemea matatizo yao.

Sasa inapotokea wabunge mnasahau mlichotumwa na wananchi wenu, matokeo yake mkajiingiza kwenye ile fasheni mpya ya kuomba Bunge liwaruhusu kuwasilisha hoja binafsi kuhusu ufisadi fulani ambao si kero ya wananchi, kwakweli inatia kichefuchefu na kutukera.

Msifikiri hatuwaoni mnayoyatenda huko bungeni, tunayajua na tunayaweka kwenye fikra zetu.
Hakika Uchaguzi Mkuu ujao sisi wananchi tutawahoji, ni kwanini mmeshindwa kutusemea kero zetu bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani.

Tunataka wabunge wa vitendo na wanaotanguliza masilahi ya wapiga kura wao mbele kuliko fasheni mpya ya kuomba kuwasilisha hoja binafsi kuhusu ufisadi.

Utakuta mbunge anauliza swali kuhusu uchunguzi wa ufisadi katika kampuni fulani kwamba umefikia wapi wakati mbunge huyo huyo katika kampeni zake za Uchaguzi Mkuu alitumia ufisadi wa kugawa rushwa na mbinu nyingine chafu hadi akashinda ubunge.

Na wabunge waliotumia mbinu chafu, dhalimu na dhuluma hadi wakafanikiwa kuupata ubunge tunawafahamu na tunasikia kichefuchefu kuwaona wakiwa ndani ya Bunge na kujigeuza vinara wa kuuliza maswali kuhusu ufisadi wakati naye anajua na wapiga debe wake wanajua vema walitumia mbinu chafu kuhakikisha mbunge wao anapata ubunge. Ina kera sana.

Nimalizie kwa kumtaka Spika Makinda atambue kuwa yeye ndiye mwanamke pekee tangu nchi hii ilipopata uhuru Desemba 9, 1961 kuteuliwa kuwa Naibu Spika na sasa Spika wa Bunge.
Kwa hiyo atambue wadhifa wake huo ni kielelezo kuwa wanawake wanaweza wakipewa nafasi.
Hivyo endapo atashindwa kuthibitishia umma na Afrika kuwa yeye ni Spika mwanamke na anaweza, ajue hiyo haitakuwa aibu yake bali itakuwa ni aibu kwa wanawake wote.

Spika Makinda anapaswa awe Spika anayesimamia sheria na kanuni za Bunge bila kutetereka, aachane na tabia ya kuwaona wabunge wakishindwa kusimamia kanuni na kutoa maneno yanayohatarisha amani ndani ya Bunge akaishia kusema: “Wabunge vitendo mnavyovifanya mjue mnajidhalilisha,” hii kauli hatutaki tena kuisikia.

Wabunge ni watu wa kupita, hivyo wanapotokea baadhi ya wabunge wanatoa maneno yasiyotakiwa bungeni, wanapaswa kuchukuliwa hatua ili liwe fundisho kwa wengine.

Wito kwa Spika Makinda ni kwamba tunaomba ulifanyie kazi tamko la Naibu Spika Ndugai, linalosema kuna baadhi ya wabunge wanawake wanavaa nguo fupi.
Madai hayo ni mazito, kwani inaonyesha wabunge wa kike wameshindwa kudhibitiwa kuhusiana na suala la kuvaa nguo fupi.

Hivyo baadhi ya wabunge wa kike wanaovaa nguo fupi ndani ya Bunge letu tukufu, Fukuto la Jamii linasema kama kazi ya ubunge imewashinda ni vema mjivue ubunge, kwani kamwe hatuwezi kukubali kuona Bunge letu heshima yake inaporomoshwa na baadhi ya wabunge wachache kwa mavazi yao.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Mei 10 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.