Header Ads

HONGERA OFISI YA DDP,POLE MARANDA,FARIJALA


Na Happiness Katabazi

MEI 23 mwaka huu serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Eliezer Feleshi iliandika historia mpya ya ushindi wa kesi moja kati ya jumla ya kesi 12 za wizi wa mabilioni ya Fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania .

Historia hiyo ya ushindi ilitokana na jopo la Mahakimu wakazi watatu lililokuwa likiongozwa na Saul Kinemela,Phocus Bambikya na Elvin Mugeta kutoa hukumu katika kesi ya jinai Na.1161/2008 iliyokuwa ikimkabili Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda na Binamu yake Farijala Hussein ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi wizi wa shilingi bilioni 1.8 kwa kutumia kampuni yao hewa ya Kiloloma &Brothers kuonyesha kampuni hiyo imepewa idhini ya kudai deni la Kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India katika BoT ,huku wakijua si kweli.

Ambapo Hakimu Mugeta ambaye ndiye alikuwa akisoma hukumu hiyo alisema washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa nane lakini mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kuwatia hatiani kwa jumla ya makosa sita ya kughushi nyaraka mbalimbali na kisha kujipatia kiasi hicho cha fedha na kusema kuwa inawafutia makosa mawili ya kula njama na wizi kwasababu jamhuri ilishindwa kuthibitisha makosa hayo.Hali iliyosababisha siku hiyo mahakama hiyo kuzizima kwa vilio huku baadhi ya wananchi wakifurahia hukumu hiyo.

Kabla sijaendelea na mada ya leo, Fukuto la Jamii litawakumbusha wasomaji wake jinsi kesi hii ilitolewa hukumu ilivyokwenda hatua kwa hatua kwani mwandishi wa Fukuto la Jamii ni miongoni mwa waandishi wa habari za mahakamani na nimiongoni mwa waandishi wa habari wachache nchini ambao wameiripoti kesi hiyo na kesi nyingine tangu zilizofunguliwa hadi kutolewa hukumu.

Novemba 4 mwaka 2008, ndiyo siku ya kwanza ambayo nayo itabaki kuandikwa kwenye historia kuwa ndio siku ambayo DDP- Feleshi iliwaburuza mahakamani watuhumiwa wa wizi katika akaunti ya EPA, baada ya skendo ya wizi kuibuliwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoo, kelele za wananchi na wafadhili, hali iliyosababisha Rais Kikwete kuunda Tume ya uchunguzi wa wizi huo ambayo ilimshirikisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP-Said Mwema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dk. Edward Hosea na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa sasa amestaafu, Johnson Mwanyika.Tume hiyo iliwahoji watuhumiwa na hatimaye kuwafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbali na kesi hiyo Na.1161/2008 ambayo Mei 23 mwaka huu ndiyo ilitolewa hukumu, Maranda na Farijala pia wanakabiliwa na kesi nyingine tatu za EPA ambazo nazozimefikia katika hatua ya kusikilizwa, kufanywa majumuisho ya wanakesi ya kujibu au la na kujitetea.Kesi ya pili ni jinai Na.1162/2008 inamkabili tena Farijala ,Maranda ambao wa kwasasa wanatamikia kifungo chao katika Gereza la Ukonga, maofisa wa BoT ambao ni Iman Mwakosya,Ester Komu na Bosco Kimela ambapo upande wa Jamhuri wanadai washtakiwa hao waalighushi nyaraka kwa kutumia kampuni hewa ya hewa ya Rashaz T Ltd kuchota sh milioni 207 katika akaunti ya EPA.

Kesi ya tatu ni Na.1163/2008 ambayo inamkabili Maranda na Farijala ambapo walitumia kampuni yao hewa ya Money Planner kuchota fedha katika EPA.Ambapo kesi hii tayari Jamhuri imeshafunga ushahidi wake na mahakama kilichobaki sasa ni pande zote kuwasilisha mahakamani majumuisho ya kesi hiyo ambayo wataiomba mahakama iowaone washtakiwa hao wanakesi ya kujibu au la.

Kesi ya nne ni Na.1164/2008 inamkabili Farijala,Maranda,Iman Mwakosya,Ester Komu,Sophia Lalila na Ajay Somani ambao jamhuri inadai washtakiwa walikula njama,kushushi nyaraka za jina usajili, hati ya kuamisha deni,kujipatia ingizo kwa kutumia kampuni feki ya Mibale Farm kuonyesha imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Raksh Mills Textile Co.Ltd ya nchini India na kisha kujipatia ingizo la shilinigi bilioni 3.8 toka kwenye akaunti ya EPA.

Kesi hii imefikia hatua ya mshtakiwa wa pili (Maranda) Juni 2 mwaka huu, kupanda kizimbani kujitetea baada ya Mei 5 mwaka huu, mshtakiwa wa kwanza Farijala Hussein kumaliza kutoa utetezi mbele ya jopo la mahakimu wakazi Sam Karua,Elvin Mugeta na Jaji Beatrice Mutungi. Tukiachana na kesi hizo tatu zinazowakabili fungwa hao.

Pia kuna kesi nyingine zinawakabili washtakiwa mbalimbali wa wizi wa EPA, na miongoni mwa kesi hizo ambayo jumla yake ni 12, kesi nne zinamkabili Mfanyabiashara maarufu nchini JayantKumar Chandubai Patel maarufu “Jeetu Patel’ na wenzake, ambapo ukilinganisha na kesi zote za EPA zilizopo mahakamani hapo kesi hizo nne za EPA ambazo nazo zilifunguliwa Novemba 4 mwaka 2008 zipo hatua ya chini kabisa yaani hata kesi moja moja ya msingi haijaanza kusikilizwa kwasababu mshtakiwa huyo na wenzake waliwasilisha maombi ya kuomba kesi zote zisiendelee kusikilizwa kwasababu amefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania, ya kuomba kesi zote nne zinazomkabili katika Mahakama ya Hakimu MKazi Kisutu zifutwe kwasababu Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi alimuhukumu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ wakati kesi anazokabiliwa nazo hazijaamliwa na mahakama na mahakama ya Kisutu ikakubali ombi lake la kusimamisha kesi hizo.

Baada Lakini hata hivyo mwaka juzi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage aliitisha majarada la kesi hizo za Jeetu ofisini kwake na kupitia amri zilizotolewa na majopo ya mahakimu wakazi ya kusimamisha usikilizwaji wa kesi hizo ambapo Jaji Kaijage baada ya kuyapitia alitoa amri kwa mahakama ya kisutu kuendelea kusikiliza kesi hizo lakini hata hivyo mawakili wa Jeetu, Martin Matunda na Mabere Marando hakukubaliana na amri ya Jaji Kaijage kuamua kuwasilisha maombi ya mapitio ya uamuzi wa Jaji Kaijage katika katika Mahakama ya Rufaani nchini ambapo mahakama ya rufani nchini wiki mbili zilizopita ilisikiliza maombi hayo ya mawakili wa Jeetu na muda wowote kuanzia sasa itatoa uamuzi wake.

Juni 11 mwaka 2009, Kiongozi wa Jopo la Mahakimu wakazi lililokuwa likiongozwa na Cypiriana Willam ambaye kwasasa amaestaafu kwa mujibu wa sheria na nafasi yake katika kesi hiyo kuchukuliwa na Mugeta ambao alikuwa akisaidiwa na Bambikya na Kinemela walimuona Farijala na Maranda wana kesi ya kujibu katika kesi Na.1161/2008 ambayo ilitolewa hukumu Jumatatu iliyopita ambapo mwanzo mwisho upande wa Jamhuri kesi hii ulikuwa ukiwakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface akisaidiwa na Timon Vitalis, Frederick Manyanda na Shadrack Kimaro kwasababu upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yao.

Juni 6 mwaka 2009, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Boniface aliwasilisha majumuisho ya kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wote yaani Farijala na Maranda wana kesi ya kujibu, kwani Jamhuri imeweza kuthibitisha kesi hiyo.

Aidha, Aprili 29 mwaka 2010, Rajabu Maranda alipanda kizimbani kutoa utetezi wake katika kesi hiyo ambayo leo inatolewa hukumu ambapo aliieleza mahakama hiyo kuwa alichokuwa akikizingatia katika mchakato wa kudai deni katika (EPA) ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.Na Mei 23 mwaka huu, ndiyo hukumu ya kesi hiyo ilitolewa na kufanya kesi hiyo moja ya EPA kumalizika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wahstakiwa hao kupitia wakili wao Majura Magafu wamesema hawakubaliani na hukumu hiyo na tayari wameishawasilisha katika Mahakama ya Kisutu hati ya nia ya kukataa rufaa Mahakama Kuu.

Kwa mtiririko wa kumbukumbu wa kesi ya kesi hiyo iliyokwishatolewa hukumu na kesi nyingine ambazo bado hazijatolewa hukumu zipo kwenye hatua za kusikilizwa na nyingine nne za Jeetu ambazo bado hazijaanza kusikilizwa ninaimani wasomaji wa Fukuto la Jamii mtakuwa mkielewa nini kinachooendelea katika kesi hizo.

Sasa Fukuto la Jamii linapenda kukumbusha baadhi ya matamko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kupitia vyombo vya habari, baadhi ya wanachama wa CCM wanajifahamu ambao walikuwa wanakebeki kesi chini chini,baadhi ya makala za waandishi wenzangu na baadhi ya wananchi ambao siwafahamu ambao kwa muda walikuwa wakinitumia mimi binafsi ujumbe mfupi wa kunitaka niache kufuatilia kesi hizo kwasababu mwisho wa siku nitamaliza soli za vitu bure kwasababu kesi hizo za EPA ni usanii wa serikali na mwisho wa siku kesi zote zitafutwa na kwamba hakuna hata mshitakiwa mmoja atakayetiwa hatiani.

Mengi yalisemwa kuhusu kesi hizo kuwa ni kesi za usanii tena hata baadhi ya mawakili walidiriki kusema hayo lakini Jumatatu ya wiki iliyopita pale katika Mahakama ya Kisutu baada ya hukumu hiyo kusomwa wale wale mawakili ambao miongoni mwao wanawatetea washtakiwa wengine wa EPA, majina yao nayaifadhi walinileza kuanzia siku hiyo wanafuta kauli yao kuwa kesi hizo ni za usanii na kwamba hukumu hiyo tayari imetoa ishara mbaya kwa kesi nyingine za EPA zinazowakabili wateja wao.Nilicheka sana.

Na mawakili wengine walidiriki kunieleza kuwa upande wa Jamhuri katika kesi za EPA zimejitahidi sana kukusanya ushahidi wa kutosha katika kesi hizo ila wanachokifanya ni kutumia mbinu chafu ya kuwasilisha mapigamizi yasiyokuwa na kichwa wa miguu mahakamani ili kasi ya usikilizwaji na umalizikaji wa kesi za EPA uchelewe ili wateja wao waendelee kubaki uraiani.

Na baadhi ya mawakili wanaofanya mchezo huo ambao majina yao nayaifadhi yalinieleza kuwa serikali imeishabaini hujuma hizo wanazozifanya kuchelewesha kesi hizo na wamekuwa wakiitwa na kuonywa na mamlaka husika na mawakili hao hivi sasa wamesema wanaachana na mchezo huo kwani mwisho wa siku wanaweza wakajikuta wananyang’anywa leseni ya uwakili kwaajili ya kesi moja tu ya kupita wakati leseni hiyo ndiyo inamfanya aendeshe maisha yake.

Lakini kama ilivyoada ya watanzania wengi kuwa na hulka ya kudhika mambo fulani,kusema sema ovyo na kutoa hukumu hata kama hawana ushahidi na hayo mambo wanayoyasema.Hadi sasa wale wanasiasa wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wakisema kesi hizo ni usanii hata baada ya kesi hiyo moja kutolewa hukumu hadi sasa wameshindwa kujitokeza tena kwenye vyombo vya habari kufuta kauli zao na kuipongeza upande wa Jamhuri kwakushinda kesi hiyo.Lakini ingetokea upande wa Jamhuri kesi hiyo wangeshindwa ni wazi kabisa wanasiasa hao wangeibuka kutoka mafichoni na kutoa kauli za kuikebehi serikali na waendesha mashtaka wake.

Tabia hii binafsi uwa inanikera sana kwani tumekuwa taifa la wananchi tunaopenda sana kupakana matope,kuhukumiana na kushindwa kupongezana pale taasisi fulani au mtu fulani anapofanya jambo jema kwa maslahi ya nchi.Taasisi hizo zinapofanya vibaya tumekuwa vinara wakuwaramu lakini zinapofanya vizuri hatuzipongezi.Tuachane na utamaduni huo wa kijinga badala yake tujenge utamaduni wa serikali, vyama vya siasa, viongozi wetu ama wananchi wanapofanya jambo jema tuwapongeze na wanapokosea tuwakosoe kwa hoja na kuwaelekeza nini wafanye.

Na mfano wa hayo ninayo ya sema ni ile hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam(ACP),Abdallah Zombe na wenzake nane ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauji.Wananchi mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na mimi mwandishi wa Fukuto la Jamii, tuliwashambulia mawakili wa serikali kwa kushindwa kesi hiyo.

Na siyo kesi ya Zombe tu, hata mimi binafsi kupitia makala zangu hapo nyuma nilikuwa nikandika makala za kuwaandama mawakili wa serikali ambao walikuwa wakiziendesha baadhi ya kesi za EPA, kwani hapo awali walikuwa wakionekana kubabaika katika uandaaji wa hati za mashtaka hali iliyokuwa ikiwalazimu kuzibadilisha hati za mashtaka mara kwa mara hali iliyokuwa ikizusha hofu kwa wananchi kuwa uenda mawakili wa serikali hawapo makini katika uandaaji wa hati hizo hali licha kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, inauruhusu upande wa jamhuri kuifanyia hati ya mashtaka marekebisho(amendment of charge).

Lakini siku zote muungwana asifiwi ushenzi, kwakuwa ni kweli serikali ilishindwa kwenye kesi ya Zombe nikaandika makala ya kuisema , na Jumatatu ya wiki iliyopita serikali Iliweza kuibuka mshindi katika kesi ya EPA, leo nimelazimika kuandika makala ya kuipongeza serikali kwa kushinda kesi hiyo.Na huu ndiyo msimamo wangu kwamba serikali ikifanya vizuri nitaipongeza na ikivurunda nitaikosoa.

Kwahiyo Fukuto la Jamii kwanza kabisa linapenda kutoa pongezi za dhati kwa serikali kupitia ofisi ya DDP-Feleshi na timu yake ambayo ilikuwa ikiongozwa na mawakili mahiri wa serikali Stanslaus Boniface,Fredrick Manyanda kwa kuweza kuleta mahakamani vielelezo,mashahidi na kutumia mifano ya kesi mbalimbali na sheria mbalimbali mahakamani hali iliyokuwa ikiufanya upande wa washtakiwa mara kwa mara wakati kesi hiyo ikiendelea kushindwa kufurukuta na mwisho wa siku upande wa Jamhuri wakaibuka washindi katika kesi hiyo ambapo mahakama ilihukumu kifungo cha miaka mitano jela na kuwataka washtakiwa warejeshe kiasi hicho cha fedha kwa mwenyewe ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hiari yao ama sivyo mali zao zitataifishwa na serikali.

Kwa wale tuliokuwa tukiudhuria kesi hii mwanzo mwisho bila kuchoka,kwanza kabisa tuliweza kujionea kuwa kumbe serikali ina mawakili wazuri wa kesi waliobobea kwenye uendeshaji wa kesi za jinai.Huwezi kuzungumzia kesi za EPA, bila kumtaja wakili mkuu wa serikali Stanslaus Boniface ambaye kwasasa amepanda cheo na kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini,Wakili Mkuu wa Serikali Fredrick Manyanda, Oswald Tibabyekomya,Shadrack Kimaro, Thadeo Mwenepazi, Timon Vitalis,Biswalo Mganga,Michael Lwena na mwanadada Arafa Msafiri.

Mawakili wao muda wote wanaendesha kesi zao kwa uweledi zaidi na umakini wa hali ya juu ukilinganisha na baadhi ya mawakili wa serikali ambao tumekuwa tukiwashuhudia kwenye baadhi ya kesi wakileta ubabaishaji hali inayosababisha wakati mwingine upande wa Jamhuri kujikuta wanashindwa vibaya katika kesi walizozifungua mahakamani dhidi ya washtakiwa kadhaa hali ambayo ilisababisha jamii kuanza kuiponda serikali kuwa haina wanasheria wazuri na walisoma vizuri kama mawakili wa kujitegemea hali ambayo kwa upande mwingine ilisababisha baadhi ya wananchi kuwa na fikra kuwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ina mawakili mabomu ambao wameshindwa kazi.

Lakini kuna msemo maarufu usemao ‘kila zama na kitabu chake’.Hivyo alipoingia madarakani rais Kikwete alimteuwa Eliezer Feleshi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na katika uongozi wake akaunda timu yake ya kufanya nayo kazi na muda mfupi baadae ikaibuka skendo ya EPA ambayo mwisho wa siku DDP mwenye akafungua kesi kwaniaba ya jamhuri na kwakuona kesi hizo zinahusisha watu wenye fedha nyingi na wenye majina makubwa kwenye jamii, kwakutambua hilo akaamua kupanga kikosi kazi chake ambacho sisi waandishi wa habari za mahakama tumekipachika jina la ’Siafu’ kwaajili ya kuendesha kesi hizo na kweli wamekuwa wakiziendesha kesi hizo kwa uweledi wa hali ya juu na uaminifu mkubwa ambao umethibittisha ndani ya serikali pia kuna mawakili wazuri tu ila huko nyuma walikuwa hawapewi nafasi na kwa wale wanaodhulia kesi za EPA mahakamani watakubaliana na hayo niliyoandika.

Pia safu hii inatoa pongezi kwa waandishi wa habari wenzangu wa habari za mahakamani jijini Dar es Salaam, ambao kwa umoja wetu bila kuchoka tulisimama imara na tunawaahidi wa watanzania kuwa tutaendelea kusimama imara kuripoti kesi zinazofunguliwa katika mahakama zetu bila kuchoka licha tumekuwa tukikutana na changamoto za hapa na pale,lakini nadiriki kusema mchango wa waandishi wa habari katika kuripoti kesi za mahakama ni mkubwa sana kwani mchango huo pia unachangia kwa kiasi kikubwa kukuza utawala wa sheria hapa nchini.

Baada ya kusema hayo, napenda kutoa pole kwa kaka yangu Maranda na Farijala ambao kwasasa wanaishi makazi mapya katika Gereza la Ukonga.Kwani kwa mara ya kwanza kufahamiana na kaka zangu hao ni siku walipofikishwa mahakamani hapo na hata siku kesi zao zilizopokuwa zikija kwaajili ya kusikilizwa,kabla ya kesi hizo kuanza kusikilizwa tulikuwa tukiketi wote pamoja kwenye mabechi mahakamani hapo na kuzungumza mambo kadha wa kadhaa na hata siku ili ya kusomwa kwa hukumu, saa mbili asubuhi hadi saa nne asubuhi kabla ya kuingia kwenye chumba cha mahakama kusikiliza hukumu yao.

Farijala,Maranda na mtuhumiwa mwingine wa EPA, Bahati Mahenge ambao walitokea majumbani kwao kuja mahakamani walikuja kunisalimu kwenye benchi nililokuwa nimekaa peke yangu na tukazungumza na kucheka lakini saa chache baadaye ndiyo mahakama iwahukumu na kuwashuhudia askari kanzu wameishawavalisha pingu mikononi na kuwapandisha gari la wazi mithili ya ‘maharusi’ na kuondoka mahakamani hapo ambapo kuanzia siku hiyo jina la watuhumiwa lilibadilika na kuuitwa wafungwa.Lakini kwakuwa bado mnakabiliwa na kesi nyingine tatu tutakuwa tukionana mahakamani hapo licha haitakuwa kama zamani kwani hivi sasa mtakuwa mkilindwa na askari wa Jeshi la Magereza. Kwa kweli inasikitisha sana hasa ukifikiria wameacha familia zao zikiwa zinawategemea.

Lakini hakuna jinsi,sisi waumini wa sheria tuna msemo usemao ‘sheria ni msumeno’ na kweli msumeno huo ndiyo umemkata Kaka yangu Farijala na Maranda.Na siku zote mimi usema hukumu mbalimbali zinazotolewa na Mahakama zetu ufunza jamii iishi kwenye mstari ulionyooka. Kwa hiyo hukumu ya Farijala na Maranda imetoa funzo kwao na sisi wananchi wengine ambao ni watuhumiwa watarajiwa kuwa tusithubutu kufanya vitendo vinavyovunja sheria za nchini kwani tukae tukijua vikitenda vitendo vya kuvunja sheria mwisho wa siku tutajikutwa tunafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwenda kuishi Magerezani.

Mwisho Fukuto la Jamii linapenda kuikumbusha ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, kuwa isilewe sifa na ushindi huo, kwani ikumbuke bado ina kesi nyingi ambazo zinafuatiliwa kwa karibu jamiii kwahiyo iongeze nguvu katika kesi hizo ili mwisho wa siku washtakiwa ambao kweli walitenda vitendo vya ufunjifu wa sheria nikiwemo kukwapua fedha za umma watiwe hatiani na mahakama.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 31 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.