Header Ads

KESI YA RICHMOND:SHAHIDI WA JAMHURI AIGEUKA JAMHURI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa tano wa upande wa Jamhuri Ruabangi Luteganya(52) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa kampuni ya Richmond Development Company kupitia nyaraka za kuomba tenda ya kuleta mashine ya kuzalisha umeme hapa nchini ungezalisha umeme wa megawati 110.


Luteganya ambaye wakati kampuhi ya Richmond alikuwa ni Meneja Usafirisha na kwa sasa ana cheo cha Meneja Usafirishaji na Manunuzi wa Shirika la Umeme(Tanesco), aliyasema hayo jana wakati akijibu swali la wakili wa utetezi Richard Rweyongeza na Alex Mgongolwa ambao walimuuliza ni kwanini yeye anasema Richmond ilisema itazalisha umeme wa megawati 110 wakati kwa mujibu wa hati ya mashtaka Jamhuri inadai kampuni hiyo ilidanganya kuwa inauwezo wa kuzalisha megawati 100.

Shahidi huyo alieleza kuwa Machi 20 mwaka 2006 alipewa jukumu na mkuu wake wa kazi la kusimamia ufunguzi wa waombaji tenda ambapo kwa mujibu wa orodha ya makampuni yaliyoomba tenda yalikuwa jumla 23 lakini siku hiyo makampuni yaliyoudhulia kwenye kikao hicho ni kampuni 16 na kampuni ya Richmond ilikuwepo na ilikiwakilishwa na mshtakiwa Naeem Gile ambaye alikuwa amepewa nguvu ya kisheria ya kumwakilisha Mwenyekiti wa kampuni hiyo Mohammed Gile.

‘Mimi ndiyo nilikuwa nimefungua kikao cha waombaji tenda siku hiyo ambapo kampuni ya Richmond iliwakilishwa na mshtakiwa ambaye alileta kitabu ya kampuni yao kuomba tena na kwa mujibu wa kitabu cha kampuni hiyo kinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilisema ilikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 110;

‘Sasa kuhusu hati ya mashakta ilitumika kufungulia kesi hii hapa mahakamani inadai kuwa kampuni hiyo ilidai ilikuwa ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100…mimi sijui walikuwa wamepata wapi hilo kwani kilichoandikwa kwenye kitabu cha kampuni hiyo na kuwasilishwa kwenye kikao uombaji tenda na ndicho hiki kitabu kimetolewa mahakamani hapa kama kielelezo kinaonyesha kampuni hiyo ilisema ina uwezo wa kuzalisha megawati 110 na siyo 100”alidai Luteganya.

Aidha shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo ya ufunguzi wa kikao cha uombaji tenda, mshtakiwa hakuzungumza wala kutoa taarifa yoyote kwa maneneo na kuongeza yeye akiwa kama msimamizo wa kikao cha ufunguaji tenda hakuwa amepata malalamiko toka kwenye kampuni ya Richmond kuwa mshtakiwa alikuwa ameiwakilisha kampuni hiyo vibaya na kusema kuwa kikao cha ufunguzi wa tenda uwa kumbukumbu zake urekediwa na kwamba rekodi za kikao hicho zipo.

Wakati shahidi huyo Lutenganya akijibu swali hilo la wakili wa utetezi (Rweyongeza) kuwa mshtakiwa siku ya kikao cha ufunguzi wa tenda hakuzungumza chochote, lakini katika kosa moja linalomkabili mshtakiwa huyo (Naeem) upande wa Jamhuri unadai kuwa mshatakiwa huyo siku hiyo alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali , kuwa kampuni ya Richmond ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango cha megawati 100 ili apewe tenda hiyo.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Waliarwande Lema aliarisha shauri hilo hadi Mei 23-26 mwaka huu ambapo litakuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa Jamhuri kuendelea kutoa ushahidi na akautaka upande wa jamhuri unaowakiliwa na Wakili mwandamizi wa Serikali Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro kuleta mashahidi wao kwa wingi bila kukosa.

Februali 2009 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa (Naeem) alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.Aidha, alidai katika shitaka jingine mshtakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka 2006 iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni, Hemed Gile ambaye ni kaka yake kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la jingine linalomkabiri mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO). Kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Gile amefikishwa mahakamani ikiwa ni takriban mwaka mmoja sasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo ya Kampuni ya Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 11 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.