Header Ads

KESI YA MAUJI YA MTOTO WA FUNDIKILA YAIVA

Na Happiness Katabazi MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Juni 4-8 mwaka huu, itaanza kusikiliza kesi ya mauji ya mtoto wa marehemu Chifu Abdallah Fundikila,Swetu Fundikila inayowakabili MT 1900 Sajenti Roda Robert(42) wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni na wenzake. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya uendeshaji wa kesi za Mahakama Kuu ambayo gazeti hili imeiona nakala yake, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Zainabu Mruke na jumla ya mashahidi tisa wa upande wa jamhuri wanakuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo. Mbali na Dorisi washtakiwa wengine ni MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni. Wakili wa serikili Dionisia Saiga awali alidai mahakamani hapo kuwa Januari 23 mwaka 2010 kuanzia majira ya saa 6 usiku, kuwa marehemu akiwa na wenzake wawili wakitumia gari aina ya Toyota Corolla, walikuwa wanatoka Mwananyamala na kwamba walikutana na washtakiwa wakiwa kwenye gari lao wakitokea kwenye maegesho ya magari ya Baa ya Mango Garden. Wakili Saiga alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza alimwamuru dereva wa gari alilokuwemo marehemu, arudi nyuma na kwamba dereva huyo alitii.Alidai kuwa washtakiwa walilifuata gari hilo na kusimama pembeni na baadaye mshtakiwa wa kwanza alishuka na kumfuata dereva na kumuonya kuwa siku nyingine asipowaheshimu viongozi wa nchi atapata shida. Aliendelea kudai kuwa baada ya hapo marehemu na wenzake waliondoka lakini walipofika kwenye makutano ya Barabara ya Kawawa na MwinyiJuma, walikutana tena na washtakiwa ndipo mshtakiwa wa kwanza akawatukana. Alidai kuwa marehemu aliuliza sababu ya kuwatukana bila kosa, lakini badala yake mshtakiwa wa kwanza aliaanza kumpiga dereva, jambo lililomlazimisha marehemu kwenda kuzuia dereva asipigwe. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni Mosi mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.