Header Ads

ALIYEJIFANYA MWANDISHI WA HABARI JELA MIAKA MITATU





Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, imemhukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh.500,000  Msambazaji wa Gazeti la Mtandao,Salum Hassan Goko baada ya kumkuta na hatia ya kujifanya Mwandishi wa habari wa gazeti hilo na kuomba na kupokea rushwa ya Sh.200,000 kutoka kwa Meneja wa Kampuni ya Vinywaji Baridi aina ya Pepsi, Rashid Chenja.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Jocye Minde ambaye alisema amefikia uamuzi huo kwani mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ilala Dar es Salaam, uliokuwa ikiliwakilishwa na  Sarha  Abdallah na Sophia Gula wameweza kuithibitisha kesi hiyo  ya tuhuma za rushwa Na.24/2008 bila ya kuacha mashaka yoyote na kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh.200,000 kinyume na kifungu cha 15(1) A cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007.

Hakimu Minde alisema kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo vilionyesha wazi kuwa mshitakiwa Goko alikuwa ni mfanyakazi idara ya Usambazaji wa gazeti hilo la Mtandao lakini alijifanya yeye ni mwandishi wa habari wa gazeti hilo na akamfuata Chenja na kumweleza kuwa wanataarifa zake kuwa anatembea na mke wa mtu hivyo wakamtaka Chenja awapatie fedha ili wasichapishe habari hizo na endapo asingewapatia fedha hizo wangeenda kuzichapisha na zingemchafulia jina lake.

“Chenja alikubaliana na maelekezo hayo ya Goko na akamtaka Goko aje mwisho wa mwezi ili ampatie fedha ili asiandike habari yake na ushahidi wa mawasiliano ya simu unaonyesha Goko na Chenja walikuwa wanawasiliana na Chenja alienda kutoa taarifa Takukuru na ndipo Takukuru walimpatia Sh.200,000 za mtego wa Rushwa na Goko alipokwenda kuzipokea fedha hizo alikamatwa na maofisa wa Takukuru na kisha kufikishwa mahakamani”alisema Hakimu Minde.

Hakimu huyo alisema amefikia uamuzi wa kuukataa utetezi wa Goko ambaye alikuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Tuliamwesige kwasababu ushahidi wake ni dhahifu  hivyo mahakama yake imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri na kwamba imemkutana na hatia ya makosa hayo na hivyo inamhukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini y a Sh.500,000. Hadi saa nane mchana jana Goko alikuwa chini ya ulinzi mahakamani hapo.

 Katika hatua nyingine mhariri  Mtendaji wa Kampuni ya New Habari ,Absalom Kibanda ambaye Machi mwaka huu alitekwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiyojulikana na hivyo kusababisha kushindwa kuudhiria katika kesi ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi, jana kwa mara ya kwanza aliweza kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, kuudhulia kesi yake.

Mbali na Kibanda katika kesi hiyo washitakiwa wengine ni aliyekuwa Kaimu Mhariri wa gazeti la Mwananchi , Theophil Makunga na mwandishi wa makala hiyo Simon Mwigamba ambao wanatetwa na mawakili wa kujitegemea Isaya Matambo, John Mhozya.

Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alisema kesi hiyo ilikuwa imekuja kwaajili ya kitajwa lakini amepokea taarifa kutoka kwa mdhamini wa Mwigamba kuwa Mwigamba ameshindwa kuudhulia jana mahakamani hapo kwasababu ni mgonjwa hivyo anaiarisha kesi hiyo hadi Julai 17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

Disemba mwaka 2011 ilidaiwa mahakamani hapo na mawakili wa upande wa jamhuri kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo ya kuruhusu na kuchapisha makala ya uchochezi katika gazeti la Tanzania Daima iliyokuwa na kichwa cha habari “Wakala Maalum kwa askari wote’.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni 21 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.