RIPOTI YA KUPIGWA,KUJERUHIWA VIBAYA KWA ABSALOM KIBANDA
UTANGULIZI
Usiku
wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari
(2006) Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Absalom Kibanda, alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia
nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Tukio
hilo lililishtua na kulitikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya
habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji
na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio
lililomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka,
lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni
26, 2012.
Ukiacha
matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa, mwandishi Daudi
Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko
Nyololo, Iringa akiwa kazini.
Tukio
la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari,
hasa ikitiliwa maanani kuwa mwandishi Issa Ngumba (45) wa Redio Kwizera
aliyekuwa anafanya kazi zake katika wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari, mwaka
huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Kama hiyo
haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda lilitokea mwezi mmoja tu
baada ya mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu, kupigwa risasi
na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa polisi kwa makosa
walidhani Matutu ni jambazi.
Mazingira
ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na
dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi
wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo
shilingi milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama
(ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawakuchukua chochote baada ya
kukamilisha uhalifu wao.
Kibanda
aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya
kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa.
Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji hawa katika
unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na
kuondokana nayo.
Hali
hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za
kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki.
Kutokana
na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa
la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.
Katika
kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda timu ya watu
watano na kuipa hadidu za rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya
shambulio hilo ili kubaini limetokana na nini.
Timu
hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na
baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari
kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF).
Ruzuku
ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza
mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio
ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka. Timu hii
imefanya kazi usiku na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi.
Timu
imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu
zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na
vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari
zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012
na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata
kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.
Vyombo
vya dola akiwamo waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya
serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani
na tume hiyo.
Leo
tunawasilisha muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho
vyake, itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa
kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold
stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya
kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.
HADIDU
ZA REJEA
Timu
ilipewa hadidu za rejea zifuatazo:-
- Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.
- Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.
- Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
- Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.
- Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika
YALIYOJIRI
KATIKA UCHUNGUZI
1.0. Kuchunguza
mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake.
Kabla
ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote
vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake, timu ya uchunguzi
ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria,
sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili.
Tuliangalia
pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au
kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii.
Uchunguzi
umebaini kuwa kulikuwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa
karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeleta madhara makubwa kiasi hiki
kama ifuatayo:-
1.1. Wiki tatu
kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na
PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe, likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza
Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari
yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao.
Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.
1.2. Usiku wa
Februari 25, mwaka huu, majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda alivamiwa na watu
walioingia kwenye uzio wa nyumba yake wakavunja kioo cha gari analotumia,
lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu
hao wakakimbia.
1.3. Kutokana na
uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio
mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya
Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi
watano.
Hadi
Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya
Kiwango.
1.4. Kuna askari
anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata
kumpa Kibanda taarifa za kiintelijensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na
kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika
Jeshi la Polisi.
Kwa
maneno yake Kibanda alisema: “Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi kabla ya tukio aliwahi
kuniambia: “Unaandika sana, usidhani watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa
unapofika getini nyumbani kwako.”
“Tangu
wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana. Wiki mbili kabla ya tukio,
niliwahi kuhisi kitu kama hicho (cha kuvamiwa) nikiwa getini. Nilipiga honi
wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana! Hata nilipoingia ndani nilikuwa
nimekosa raha kabisa.
“Pia
kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu
wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au
Kubenea.”
1.5. Ndani ya miezi
mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara
kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu.
Haikufahamika
kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali
waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa,
Ansbert Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.1.6.
Mfanyakazi
mwandamizi wa kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki
mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwambia Kibanda maneno
mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:
“Aliniambia
Danny Mwakiteleko (aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari) hakufa kwa
ajali, bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo
ikitokea mtu ukapata ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi
au tumbo, ni lazima madaktari wadhibiti sana blood clotting.
“Na
kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga
sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina
linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira
yasiyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina
linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”
Ofisa
huyu, alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya
kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester United kumaliza
nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.
2.0. Kuchunguza
mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima
ya Jumanne Machi 5, 2013.
2.1. Familia ya
Kibanda na Kibanda mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani
hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.
2.2. Kibanda
alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo
kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim
mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. Aliogopa kwa maana hakuwa na silaha yoyote
mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:
“Nilivyoona
ningefungua geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa
hata na namba ya simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa
mimi tu, imani yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo
tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”
Mlinzi
huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini
akaanza kumwamsha ‘house girl’, ili amwamshe baba mwenye nyumba. Kitendo cha
kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda
huo, mlinzi anasema watekaji wa Kibanda walikuwa wamefanya unyama na uasi huo
na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho.
“Watu
hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.
2.3. Mke wake
alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu
wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda
anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani
na usingizi ukampitia. Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa.
“Hii
inanitesa sana moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa
nini siku hiyo tu nililala mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi
yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”
2.4.
Mmoja
kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele za Kibanda
akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga
kelele kama amevamiwa hivi.”
Mwenzake
alimjibu: “Unaota maana kuna kelele za mpira.”
Siku
hiyo kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United. Ni kweli
zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda
alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira.
Binti
aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia
dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele
yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti mmoja alibaki sebuleni.
Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe
ameshambuliwa.
2.5.
Kibanda
kwa upande wake, anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu
wawili wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha
akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, alitokea mlango wa
abiria na kuanza kukimbia huku akiita. “Mama Joshua nisaidieeeeee.”
Katika
kukimbia aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu: “Afande
piga risasi.”
Kibanda
alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige
kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza
fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala
pingiri ya kidole chake imekatwaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe.
Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0. Kuangalia
mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni
hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka
jana na kuhamia New Habari.
3.1. Mazingira ya
kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali
kadhaa yenye kustahili majibu.
Kama
ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari
imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia
ya habari kwa ujumla.
3.2. Mazingira ya
kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba
cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua
wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika
kumteka na kumuumiza Kibanda.
Haya
yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya
kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince
Bagenda, anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa
New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
3.3. Timu ya uchunguzi
ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo
kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita
katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa
za kitaaluma.
3.4.
Kibanda
hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya
kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free Media
Ltd, Freeman Mbowe, alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye alikuwa
Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo, kuliko yeye Kibanda.
Kwa
maneno yake, anasema: “Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni
bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”
Anasema
alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika
makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la
kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala hiyo, yalimsukuma aondoke.
4.0. Kuchunguza
jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa
kwa Kibanda.
4.1. Uchunguzi
ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo mienendo ya watu waliotajwa kwa njia
moja au nyingine kuhusina na tukio hili. Hata hivyo, karibu watu wote
waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka
mwenendo wa kijana Joseph Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi
aliyoyachapisha Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2.
Usiku
aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick naye alidai kuwa ametekwa katika eneo
la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu,
ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha taslimu sh 35,000, akavuliwa nguo na
kubaki na chupi tu. Pia alieleza kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi
Mabibo.
4.3. Maelezo ya
Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kueleza kuwa watekaji
walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa
kawaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10.
4.4. Daniel Chongolo
aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai kutekwa Ludovick, yeye
alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. Chongolo alikwenda kituo cha
polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa
alikuwa ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote.
“Alipouliza
amefuata nini polisi, akawaambia kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu
kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema
Chongolo.
Timu
ya uchunguzi ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.
4.5. Pia taarifa za
uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya madai ya kuibwa
kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo (inayodaiwa kuibwa)
ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huo ofisi za serikali
na kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa.
5.0. Kuchunguza
mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua
kutokana na kile kitakachobainika.
5.1. Uchunguzi
umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii inatokana na
makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui
wa masilahi yao haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi
inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
5.2. Uchunguzi
umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani
ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia
jina la MWANDISHI WETU, siku hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka
majina yao na hata wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wako
tayari kutaja nani ameandika habari fulani.
5.3. Usaliti
miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na
usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Reginald
Mengi, anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi
wataumia.”
5.4. Pia alishauri
waandishi wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa
ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya wamiliki
au makundi yenye masilahi binafsi.
6.0.
KILICHOBAINIKA.
6.1. Uchambuzi uliofanywa
na timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na
kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi yake ya uandishi wa habari (ii)
Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali (iii) Uhusiano wa kijamii
ikiwamo mapenzi (iv) Vitendo vya rushwa.
6.2. Timu
imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa,
havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na
shaka kwamba suala hili la kushambuliwa na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa
Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
6.3.
Kutokana
na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi
kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya
vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa
kuumizwa kwa Kibanda na waandishi wengine.
6.4.
Baadhi
ya waliohojiwa walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa
sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.
6.5.
Wanayataja
matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa
kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, kuwa vililenga
kuifanya CHADEMA ichukiwe na Watanzania kwa kuitaja kama chama cha kigaidi
ambacho kinateka watu na kinawaumiza.
6.6. Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, anadai kwamba mpango kama huo wa vyombo vya dola
ulitumiwa kwa NCCR-Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF)
kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kuifanya
CHADEMA ionekane ni chama cha kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana
imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo.
6.7.
Wakati
Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA imepewa
mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa ikitumia baadhi ya watumishi wa
vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu
maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa
Chama cha Mapinduzi na serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi
ya kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa njia hiyo,
inaelezwa kuwa hesabu za CHADEMA ni kuwa wananchi wataichukia CCM na serikali
yake na kuipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya CHADEMA kuwa NCHI
HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9.
Dhana
nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi,
hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo
limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na
aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua
amshughulikie Kibanda.
7.0.
MAPENDEKEZO:
Baada
ya timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii
ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.
7.2. Yanahitajika
marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya
habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.
7.3. Usalama wa
wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii
kwa ujumla. Hapa timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari
kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
7.4. Kwa kiwango
alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu,
hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi na mifuko
mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari
Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)
kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika kugharamia matibabu ya waandishi
watakaoumia wakiwa kazini.
7.5. Tukio la
kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari
zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii zimeonyesha
haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na
masilahi kwa tasnia ya habari.
7.6.
Kuna
viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au
kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka
huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo,
vyombo vya habari na waandishi wa habari wachukue tahadhari kuanzia sasa.
7.7. Taasisi za
habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na
CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari
vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.
8.0.
HITIMISHO
Ni
dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa na kazi
yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi.
Kwa
upande wa serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya
kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika. Na
kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua
viashiria vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri na
kutengeneza mazingira yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0.
SHUKURANI
9.1. Tunapenda
kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha
kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea.
9.2. Tunapenda
kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na
kuiwezesha timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.
9.3. Tunapenda
kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku,
uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika
Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza
mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.
9.4. Tunawashukuru
Kibanda, mkewe Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari
wote waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa timu hii.
9.5. Tunawashukuru
wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara
mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.
10.0.
WAJUMBE WA TIMU
Timu
hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni Deodatus Balile – Mwenyekiti, Pili
Mtambalike – Mjumbe, Jane Mihanji, Mjumbe, Tumaini Mwailenge, Mjumbe na Rashid
Kejo, Katibu
Imetolewa
Mei 30 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment