Header Ads

IDD SIMBA AFUTIWA KESI YA UHUJUMU UCHUMI







Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemwachiria huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la UDA,Idd Simba, na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na makosa mbalimbali likiwemo kosa la uhujumu uchumi kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki.

Mbali na Simba ambaye anatetewa na wakili maarufu nchini Alex Mgongolwa ambaye ni Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na mwanasiasa mkongwe nchini,wengine ni Mkurugenzi Salum Mwaking’inda, Meneja wa shirika hilo Victor Milanzi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Simon Group  Ltd, Simon Kisena ambao wanatetewa na Romani Masumbuko .

Amri ya kufutiwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi Na.3/2013 ilitolewa jana asubuhi na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Ilvin Mugeta muda mfupi baada ya wakili wa serikali Awamu Mbagwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa na kuwa hata hivyo upande wa jamhuri hautaweza kuwasomea tena maelezo hayo ya awali kama  ilivyokuwa imepangwa na mahakama kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Elizer Feleshi amewasilisha mahakamani hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitakiwa washitakiwa wote chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

 Baada ya wakili huyo wa serikali Mbagwa kutoa hati hiyo , wakili Mugeta alimpatia fursa wakili wa Idd Simba, Alex Mgongolwa azungumzie hati hiyo, Mgongolwa alieleza kuwa upande wa utetezi hawana pingamizi la hati hiyo  idi mradi tu upande wa jamhuri usije kuwasumbua tena wateja wao.

Akitoa amri ya mahakama, Hakimu Mugeta alisema kwasababu kesi hiyo ni ya jinai na ilifunguliwa na upande wa jamhuri na upande huo wa jamhuri kupitia DPP-Dk.Feleshi amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao, mahakama yake haina mamlaka ya kupingana na hati hiyo ya DPP  hivyo mahakama yake kwa kauli moja inatamka kuwafitia kesi hiyo ya uhujuju uchumi  washitakiwa wote hivyo kuanzia jana washitakiwa hao wapo huru.

Hata hivyo wakati hakimu huyo akitoa amri hiyo Kisena hakuwepo mahakamani hapo bila ya kutoa taarifa yoyote  na itakumbukwa kuwa Mei  20 mwaka huu, Hakimu Mugeta alitoa hati ya kukamatwa kwa Kisena ili aje aunganishwe kwenye kesi hiyo mpya Na.3/2013 iliyofunguliwa  Aprili 30 mwaka huu, ambapo Kisena aliongezwa katika kesi hiyo na kufanya idadi ya washitakiwa kuwa wanne kwani Mei 28 mwaka jana wakati kesi hiyo ilipofunguliwa rasmi washitakiwa walikuwa ni watatu tu yaani Simba, Mwaking’inda na Milanzi.

Mei 20 mwaka huu, kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa lakini ilishindikana kwasababu Kisena hakuwa amefika mahakamani licha ya Aprili 30 mwaka huu, aliunganishwa katika kesi hiyo ya jinai, hali iliyosababisha siku hiyo ya Mei 20 mwaka huu, wakili wa serikali Mbagwa kuiomba hati ya kukamatwa kwa Kisena na mawakili wa utetezi nao kugeuka mbogo na kuungana na upande wa jamhuri kutaka Kisena akamatwe aje aunganishwe na kesi hiyo ili washitakiwa wote kwa pamoja waweze kusomewa maelezo ya awali kwani wanaamini serikali inafahamu Kisena anapoishi na anapofanyia shughuli zake, hoja ambayo ilikubaliwa na hakimu Mugeta ambaye alitoa amri ya kukamatwa kwa Kisena na siku hiyi hakimu Mugeta aliarisha kesi hiyo hadi Juni 4 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Mwandishi wa habari hii ambaye ameifuatilia kesi hii tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo hapo

Mei 29 mwaka jana hadi jana kesi hiyo imefikia tamati,Juni 4 mwaka huu kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kusomewa maelezo ya awali lakini pia ,washitakiwa hakuweza kusomewa kwasabababu hakimu Mugeta alikuwa nje ya ofisi kikazi, Kisena hakufika mahakamani na kesi hiyo iliarishwa hadi jana ilipokuja kwaajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali na maelezo hayo ya awali hayakuweza kusomewa kwasababu DPP aliwasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa hao kwasababu hana haja ya kuendelea kuwashitaki , pia Kisena hakuwa amekamatwa na wanausalama kama amri ya mahakama ilivyokuwa imeelekeza na wala hakuwepo mahakamani hapo.

 Akizungumzia uamuzi huo wa DPP-Dk.Feleshi wa kuwafutia kesi wateja wake, nje ya viwanja vya mahakama hiyo,  Wakili Mgongolwa alisema anapongeza uamuzi huo wa DPP kwani ni uamuzi mzuri na pia ni matumizi mazuri ya sheria pale tu DPP anapoona  hana mashahidi thabiti wa kuja kujenga kesi yake atumie kifungu hicho kufuta kesi kwani DPP kuendelea kuwa na kesi za jinai mahakamani ambazo anaona kabisa hana mashahdi thabiti wa kuwaleta mahakamani kuja kujenga kesi yake ,hayo ndiyo matumuzi mabaya ya sheria kwani pia hali hiyo itaisababishia serikali gharama za kuwaleta mashahidi na kuongeza mrundikano wa mashauri mahakamani.

‘Minampongeza Dk.Feleshi kwa uamuzi wake huu wa kuwafutia wateja wetu kesi hii ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na umma wa watanzania wengi…..DPP ametumia sheria vizuri tena kwa maslahi ya taifa hili kwa kuamua kuifuta kesi hii na ninamshauri pia pale DPP anapoona kuna mashauri mengine ambayo hana hajaya kuendelea nayo pia atumie kifungu hicho kuzifuta ‘alisema wakili Mgongolwa.

Aprili 30 mwaka huu, upande wa jamhuri uliifuta kesi ya awali  ya matumuzi mabaya ya madaraka iliyokuwa ikimkabili Simba na wenzake wawili na kisha kufungua kesi mpya yenye mashitaka sita yakiwemo mashitaka ya rushwa na uhujumu uchumi  na kisha kumuunganisha Kisena katika kesi hiyo ambapo katika kesi ya awali iliyofutwa Kisena alikuwa ni shahidi wa upande wa jamhuri na hivyo kufanya kesi hiyo ya makosa ya rushwa, uhujumu uchumi kuwa na jumla ya washitakiwa wa nne hivi sasa.  

Wakili Mwandamizi wa Serikali Oswalid Tibabyekomya akiwasomea upya mashitaka yao katika kesi hiyo mpya Na.3/2013 alidai washitakiwa wanakabiliwa na  makosa ya rushwa,uhujumu uchumi,matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh. Bilioni 8.4. Na kwamba Tibabyekomya alieleza kuwa baada ya kuyachambua makosa hayo wamebaini kuwa yanaangukia katika Sheria ya Uhujumu Uchumi

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya kesi mpya , shtaka la kwanza la kula njama linawahusu Simba na Milanzi na Kisena.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, shtaka la pili la vitendo vya rushwa linamhusu Kisena peke yake, hata hivyo shtaka hilo halikusomwa kutokana na mshtakiwa huyo kutokuwapo mahakamani.

Shtaka la tatu ni la vitendo vya rushwa ambalo linawahusu Simba na Milanzi. Wakili Mbagwa alidai kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walikubali kupokea  Sh. Milioni 320 milioni kutoka kwa Kisena ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA ambazo zilikuwa bado hazijagawiwa.Katika shtaka la nne ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka, linawahusu Simba , Mwaking’inda na Milanzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 20 mwaka 2013.


No comments:

Powered by Blogger.