AKIBA BENKI KORTINI KWA UPOTEVU WA FEDHA ZA MTEJA WAKE
Na Happiness
Katabazi
MKURUGENZI wa Kampuni
ya Principal Company Limited, Godfrey Mosha ameieleleza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu Dar es Salaam jinsi Benki
ya Akiba Commercial Tawi la Ubungo ilivyoidhinisha
malipo ya fedha kwa mtu mwingine kutoka
katika akaunti yake ndani ya benki hiyo, bila yeye kuwa na taarifa wala
kuridhia.
Katika kesi hiyo ya
madai ya uzembe iliyofunguliwa na Mosha dhidi ya Benki ya Akiba, inayosikilizwa
na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema, Mosha anaomba
Benki hiyo imlipe Sh.milioni 46.8 ,
zilizolipwa kwa mtu asiyemfahamu kwa kutumia hundi nne tofauti na kwa tarehe
tofautitofauti ambazo alidai hundi hizo zimeghushiwa.
Akiongozwa na
wakili wake Michael Ngaro kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Lema, Mosha
ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo, alidai kuwa aligundua hamisho hilo la kiasi hicho cha fedha katika
akaunti ya kampuni yake Na. 0400438671, Novemba 15, 2011, alipochukua taarifa ya
kibenki (Bank Statement).
Mosha alidai kuwa baada ya kubaini hamisho hilo , alikwenda
makao makuu ya benki hiyo ambako alimuona Meneja wa Fedha, Vicent Antony na
kumwalifu kuhusu tukio hilo wakati yeye
hajawahi kuidhinisha hamisho hilo.
“Vicent aliniambia
kuwa siyo transfer (hamisho) bali ni malipo yaliyofanyika kwa kutumia cheque.
Aliniambia namba za hundi hizo na ikaonekana kuwa zililipwa kwa Rafael John
Mkwabi, mwenye namba ya akaunti 11000787541.”, alidai Mosha na kuongeza:
“Binafsi huyo John sijawahi kumwandikia hundi wakati wowote ule ,
wala sijawahi kufanya naye biashara, sijawahi kukutanana naye, wala simfahamu
kabisa.”
Mosha alidai kuwa
hundi hizo zilikuwa zimesainiwa na Vicent na Meneja Mkuu, Salehe Ramadhani,
huku akidai kuwa saini inayoonekana katika hundi hizo si yake.
Alizitaja hundi
hizo kuwa ni hundi namba 083722, ya Sh11.6 milioni iliyolipwa Novemba 11, 2011
na hundi namba 083723, ya Sh 9 milioni, pia iliyolipwa tarehe hiyo.Hundi
nyingine ina namba 083724
, ya Sh milioni 14.4 iliyolipwa Desemba
2011, na hundi namba 083725, ya Sh.milioni 11.8 iliyolipwa Desemba 3, 2011.
Mosha kupitia
wakili wake Ngaro alizitoa hundi hizo na nyaraka nyingine mbalimbali na kuomba zipokelewe kama vielelezo.Na baada
ya kumaliza kutoa ushahidi wake, wakili , Ngalo alifunga ushahidi na hakimu
Lema aliarisha kesi hiyo hadi Julai 8 mwaka huu, iyakapokuja kwaajili ya mdaiwa
ambaye ni benki ya Akiba inayotetewa na wakili wa kujitegemea Karoli
Tarimo waanze kujitetea.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Juni 24 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment