MHINZI WA TEFFA KORTINI KWA KUISHI NCHINI BILA KIBALI
Na Happiness Katabazi
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu wilaya ya Temeke (TEFA), Peter Steven Mhinzi (64),jana alifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka
ya kuishi nchini, kinyume na sheria.
Mbele ya Hakimu Devotha Kisoka,
Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Patrick Ngayomela alidai
kuwa Mhinzi anakabiliwa na kosa la kuishi nchini kinyume na kifungu cha
31 (1) na (2) cha sheria ya Uhamiaji, na kuwa Julai 14, mwaka 2010
katika ofisi ya uhamiaji Temeke , Mhinzi akiwa raia wa Burundi
alipatikana akiishi nchini bila ya kuwa na kibali cha kuishi nchini.
Wakili Ngayomela alidai kuwa upelelezi wa kesi
bado haujakamilika ,na kwamba hawana
pingamizi na dhamana na akaomba mahakama
ipange tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo ili kuangalia kama upelelezi wa shauri
hilo kama umekamilika.
Wakili wa Muyinzi, Mtiginjola
aliiomba mahakama kumpa dhamana mteja wake, Hakimu Devotha Kisoka
alimuachia huru Mhinzi baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na
wadhamini wawili wanaominika ambao kila mmoja wao pamoja nay eye mwenyewe
walisaini bondi ya Sh 5 milioni.
Hata hivyo, baada ya zoezi hilo kukamilika,
Wakili Mtiginjola aliiomba mahakama kuifuta kesi hiyo kwa madai kuwa
ilipelekwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kinyume na sheria.
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi
kuandikiwa barua na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam,
akimtuhumu kuwa yeye siyo raia wa Tanzania na kumuamuru aondoke
nchini ama aombe kibali cha kuwepo hapa nchini.
Mtiginjola alidai kuwa baada ya kutolewa kwa tuhuma hizo,
Mhinzi alifungua maombi maalum Oktoba 7 mwaka 2011 katika Mahakama Kuu ya
Tanzania akidai kuwa ametuhumiwa pasipo kupewa nafasi ya kusikilizwa.
Aliongeza kudai kuwa, Mahakama Kuu
ilikubaliana na maombi ya Mhinzi Oktoba 20, 2011 na kuamuru kuwa
asifanyiwe bughudha yoyote hadi maombi yake ya msingi yatakaposikilizwa.
Alisisitiza kuwa uamuzi huo ulikuwa na maana kuwa chochote kisifanyike dhidi ya
mshtakiwa hadi hapo maombi ya msingi yatakaposikilizwa baina ya pande
mbili.
“Mheshimiwa hakimu tumeshtushwa kwa
kufunguliwa kwa shauri hili jipya linalodai mteja wangu anaishi nchini kinyume
na sheria wakati tayari kuna amri ya Mahakama Kuu inayozuia Mhinzi
asibughudhiwe hadi maombi ya msingi yatakaposilizwa, chochote kitakachoendelea
kitakuwa ni dharau dhidi ya uamuzi huo uliotolewa na Jaji Frederick Mgaya
ambao hadi sasa bado haujatenguliwa.”Alidai wakili Mtiginjola.
Alidai kuwa ilikuwa ni tegemeo la
Muhinzi kuona upande wa Jamhuri ukijibu maombi yake ili iweze kuonekana
kuwa alipata haki ya kusikilizwa ama la na ndipo afunguliwe shtaka hili lakini
hilo halikufanyika.
Hivyo kuendelea kusikilizwa kwa shauri hili
ni kama Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu zinapimana nguvu
na kuomba ifutwe.
Kwa upande wa wakili Ngayomela,
aliiomba shauri hilo liendelee kusikilizwa katika mahakama ya Kisutu kama
jinsi lilivyosajiliwa na kwamba muda uliowekwa na mahakama Kuu wa kutaka
mshtakiwa huyo asibughudhiwe umekwisha pita. Hata hivyo kwa upande wake Hakimu Kisoka
alisema atatoa uamuzi juu ya hoja hizo Juni 14, mwaka huu,.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 30 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment