Header Ads

CHE MUNDUGWAO KORTINI KWA WIZI WA PASPOTI 26

*DPP AWAFUNGIA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

MSANII wa muziki nchini, Chigwele Che Mundugwao 46, ofisa Manunuzi  wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius 37 na mfanyabiashara, Ally  Jabir ( 34) jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na jumla ya mashitaka manne likiwemo kosa la wizi wa jumla ya Pasipoti 26.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya  mbele ya Hakimu Mkazi  Aloyce Katemana wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha  384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu , Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma,  katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Komanya alidai kuwa washitakiwa  Chigwele, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam ,walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.

Kuhusu  Che Mundugwao,wakili Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa akimiliki  paspoti 12  za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .

Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa Mei , mwaka huu  Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili  zenye majina ya watu wengine sababu yoyote ya msingi. 
Komanya aliendelea kuwa Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally , alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua kuwa si kweli.

Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,   Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya Uhamiaji wakati si kweli.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, walikana na upande wa jamhuri ukadai  kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Wakili Komanya alidai kuwa kutokana na asili ya makosa hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana chini ya kifungu cha 148 (4) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 na ataiondoa hati hiyo pale atakapoona hipo sababu ya kufanya hivyo ila kwasasa amefunga dhamana ya washitakiwa hao. 

Kiongozi wa jopo  la mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Peter Kibatala aliiomba mahakama kuwapa dhamana washtakiwa hao kwa sababu mashtaka yao yanadhaminika na kwamba hayapo katika vifungu ambayo vinazuia dhamana.

Hata hivyo Hakimu Katemana  aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 5, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya hoja hizo zilizowasilishwa mahakamani hapo na akaamuru washitakiwa wote wapelekwe gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 4 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.