Header Ads

RUFAA YA DPP VS JERRRY MURRO YAKWAMA





Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilijikuta ishindwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC1), Jerry Murro na wenzake kwasababu ya kusikiliza sababu zilizowasilishwa na mawakili wa DPP za kuwasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa mahakama hiyo wa Aprili 29 mwaka huu.

Mawakili wa  upande wa Jamhuri Lilian Itemba na Emma Msoffe mbele ya Jaji Dk.Fauz Twaib  walianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa rufaa hiyo iliyokatwa na DPP dhidi ya Murro na wenzake ilikuja jana kwaajili ya mahakama kuanza kusikiliza sababu za DPP za kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya mwaka juzi, ambayo ilimwachiria huru Murro na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya madai ya kuomba rushwa ya Sh.milioni 10.

Wakili Itemba  alieleza kuwa  upande wa jamhuri haupo tayari kuanza kusikiliza rufaa hiyo kwasababu Mei 14 mwaka huu, DPP aliwasilisha taarifa ya kukataa rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Twaib wa Mei 29 mwaka huu, ambao ulitupilia mbali ombi la DPP lililokuwa linaomba mahakama hiyo itoe amri ya kesi hiyo iiliyoamriwa na mahakama ya Kisutu irudishwe katika Mahakama ya Hakimu Kisutu na ianze upya kwasababu mwenendo wa kesi hiyo hausomeki. Mwaka juzi DPP alikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu ya Novemba 31 mwaka 2011  na  DPP aliomba mahakama kuwa kwanza ianze kusikiliza ombi lake hilo la linaloomba kesi iliyohukumiwa na mahakama ya Kisutu ianze kusikilizwa upya na kisha ndiyo sababu zake za kukata rufaa ndio zifuate kusikilizwa.
‘Kwakuwa tayari DPP ameishawasilish mahakama ya rufaa hatia ya nia ya kukatia rufaa uamuzi wako wa Aprili 29 mwaka huu, ni wazi kisheria rufaa ya DPP dhidi ya Murro ambayo leo ilikuja mbele yako kwaajili ya kuanza kusikilizwa haiwezi kuendelea kusikilizwa kwasababu hati ya kusudio la kukataa rufaa inaunda rufaa …hivyo tunaiomba mahakama itoe amri ya kusimamishwa usikilizwa wa rufaa ya DPP dhidi ya Murro  iliyopo mahakama kuu, hadi rufaa iliyokatwa na Dpp mahakama ya rufaa itakapotolewa uamuzi”alidai wakili Itemba.

Kwa upande wake wakili wa utetezi Richard Rweyongeza na Pascal Kamala waliomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo na badala yake mahakama iendelee kusikiliza rufaa hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa kwasababu uamuzi wa jaji Dk.Twaibu wa Aprili 29 mwaka huu, ulizungumzia ombi moja tu la DPP katika rufaa yake,na hivyo uamuzi ule hauwezi kukatiwa rufaa kwasababu amri ile ni amri ya muda ambayo haitakiwi kukatiwa rufaa wakati rufaa yenyewe  bado haijaanza kusikilizwa na kwamba upande wa jamhuri ungesubiri rufaa iliyopo mahakama kuu isikilizwe na iamriwe ndipo DPP aende mahakama ya rufaa kukata rufaa.

Kwa upande wake Jaji Twaib alinza kwa kuwauliza mawakili wa jamhuri kuwa wanaenda mahakama ya rufaa kukatia rufaa uamuzi wake kwakutumia sababu gani.

‘Katika uamuzi wangu wa Aprili 29 mwaka huu, ambapo nilitupilia mbali ombi la DPP lilokuwa linaomba kesi ya msingi irudishwe Mahakama ya Kisutu na ianze upya kwasababu mwenendo wa kesi hiyo hausomeki vizuri…na kama mtakumbuka nilisema wazi kuwa sababu ya mimi kutupilia mbali ombi la DPP sikuzitaja nilisema nitazitaja katika hukumu yangu ambayo nitaitoa baada ya kumaliza kusikiliza rufaa hii....licha ya kutozitaja sababu hizo ila sababu ninazo na moja ya sababu ya kufikia uamuzi ule ni kwamba nilikwepa kuwa maamuzi tofauti tofauti katika rufaa moja’alisema Jaji Twaib.

Hata hivyo  wakili Itemba akijibu hoja hiyo ya Jaji Twaib huku akitumia mfano wa kesi moja ,alieleza kuwa ni kawaida kwa mahakama Kuu kutoa amri ya kusitisha kuendelea na shauri lolote kama inatokea kuna upande mmoja katika shauri husika umekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa , hivyo sijambo geni kwa upande  jamhuri kuwasilisha ombi hilo la kuomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia usikilizwa wa rufaa iliyokatwa na DPP dhidi ya Murro   hadi pale mahakama ya rufaa itakapotoa uamuzi wake katika rufaa iliyokatwa na DPP dhidi ya Murro ya kupinga uamuzi huyo wa Jaji Twaib.

Jaji Twaib alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba anaomba ajipe muda wa kwenda kufanya utafiti ili mwisho wa siku aje kutoa uamuzi sahihi wa kisheria, hivyo akaaiarisha shauri hilo hadi Julai Mosi mwaka huu, atakapokuja kutoa uamuzi wake wa ama usikilizwaji wa rufaa hiyo iliyopo mahakama Kuu iendelee au isiendelee kusilizwa kwa sababu DPP amewasilisha hati ya kusudia la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Mbali na Murro washitakiwa wengine Edmund Kapama na Deo Mugasa ambao wanakabiliwa na makosa ya kula njama na kuomba rushwa Sh.milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamayo Michael Wage.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 4 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.