HEKO MIZENGO PINDA KWA AGIZO HILO KWA JESHI LA POLISI
Na Happiness Katabazi
JUNI 20 mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa bungeni
alitoa agizo wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu kuwashughulikia wale wote
wanaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwemo kukaidi amri
zinazotolewa na jeshi la polisi.
Kauli hiyo ya Pinda imekuja hasa kutokana na vurugu
zilizotokea Arusha kuanzia wiki iliyopita ambapo watu watatu wamepoteza maisha na
wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na mtu asiyejulikana kurusha bomu la mkono
katika mkutano wa siasa uliokuwa ukifanyika katika viwanja vya Soweto wilaya ya
Arusha mjini, muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kumaliza kuwahutubia wafuasi wake na hivyo
kusababisha taharuki kubwa.
Wakati mauji hayo ya kitokea huko jimbo la Monduli jumapili
iliyopita kuliwa na uchaguzi wa Udiwani, ambapo Mbunge wa Chadema,(Arumeru
Mashariki), Joshua Nansari, ilidaiwa alipigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni
wafuasi wa CCM hadi kulazwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupishana kauli na
mfuasi mmoja wa CCM na mbunge huyo hali iliyosababisha Nansari kupigwa.
Juni 16 na 17 mwaka huu, kwa nyakati tofauti Mbowe alizungumza na waandishi wa habari na
kusema tukio lile lilipangwa na kwamba anaoushahidi wa aliyefanya tukio lile.Na
baadhi ya watu wengine walinukuliwa wakisema Jeshi la polisi linamfahamu
aliyefanya unyama ule ila imeamua kumficha.
Baada ya Mbowe na baadhi ya wananchi hao kusema hayo, Kamisha
wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, aliibuka na kusema
wanamtaka Mbowe ajisalimishe polisi na aelete huo ushahidi anaosema anao, na
akatoa rai kwa mwananchi yoyote mwenye
kuhafamu aliyerusha bomu hilo aende kutoa taarifa na zitafanyiwa kazi kwani tukio
lile lina uvunjifu wa sheria na limesababisha watu kupoteza maisha na wengine
kujeruhiwa vibaya.
Juni 20 mwaka huu, Mbowe alijisalimisha Polisi na kuhojiwa na
kisha kuzungumza na waandishi wa habari yale aliyoyazungumza na muda mfupi
baada ya Mbowe kuzungumza aliyoyazungumza kwa waandishi wa habari, Kamishna
Changonja naye aliwaambia waandishi wa habari kuwa kilichoelezwa na Mbowe kwa
vyombo vya habari ni tofauti na kile alichokieleza Mbowe wakati akihojiwa na
jeshi la polisi.
Na kwa kauli hiyo ya Kamishna Chagonja inatutaka wananchi
wenye akili timamu kutumia ule msemo wa watoto wa mjini usemao ‘akili kumkichwa’.
Baada ya hapo kumekuwa na kauli ya za kama kurushia vijembe
kama vya ‘mtu na mke mwenzie’ baina ya
polisi na viongozi wa Chadema, jambo ambalo hivi sasa limeonyesha nchi hii
hatuheshimiani,hakuna mkubwa wala mdogo, baba ,mama, mwanamke ,mwanaume
hajulikani, askari ,raia hajulikani.Kila
mtu anataka kujifanya ana sauti na madaraka hata kama hana madaraka ya kijeshi
na kiserikali.
Jeshi la polisi linapofanyakazi yake kwa mujibu wa sheria
utawasikia wanaharakati na wanasiasa uchwara wakishinikiza jeshi la polisi
lipanguliwe,lina kiuka haki za binadamu wakati ni baadhi ya hawa hawa wanasiasa
uchwara wa hapa nchini ndiyo chanzo madhara yote yanayotokea hivi sasa.Ina kera
sana.
Lakini yote hii imesababishwa na baadhi ya viongozi ndani ya CCM, serikalini na vyama vya upinzani ni mandumila
kuwili, wanafki, wasaliti, wasiyo na maadili,wanajikomba ili wapate vyeo na
wapendwe na wananchi, wavivu wa kufikiri na ndiyo maana hii leo hapa nchini baadhi
ya wananchi wamefikia hatua ya kuonyesha dharau hii kwa askari wetu wa jeshi la
polisi wazi wazi hata kama jeshi la polisi linatekeleza majukumu yake kwa mujibu
wa sheria licha ni kweli kuna baadhi ya
askari wa jeshi la polisi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utovu wa
maadili hata Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema
amekuwa akikiri hilo ana amekuwa akiagiza mamlaka zake kuwachukulia hatua askari
hao wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kuonea raia, ujambazi na mfano si wa
kutafuta .
Kwani Machi 13
mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru , Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),
aliwafikishwa jumla ya askari Polisi mkoa wa Dar es Salaam.Washitakiwa hao ni Sajenti Dancan Mwasabila (43) mkazi wa
Kiwalani, Koplo Geofrey (39) Mbezi Luis, Koplo Rajab Nkurukwa (46) mkazi wa
Buguruni, Kolpo Kawanani Humphrey (34) mkazi wa Kijitonyama na Koplo Kelvin
Mohamed (49) mkazi wa Gongo la Mboto.
Wakili wa serikali Bernad Kongola alidai kuwa Desemba 18 mwaka jana
katika eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala Dar es salaam waliiba sh,milioni 150 .
Na kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo. Na si kesi hiyo tu , pia hata yule
askari polisi Pacificus
Cleophase Simon (23) anayedaiwa kumuua marehemu Daudi Mwangosi
aliyekuwa Mtangazi wa Chanel Ten, naye amefunguliwa kesi ya mauaji katika
mahakama ya Mkoa Iringa na kesi yake inaendelea.Na bado washitakiwa hao ambao
ni askari polisi watabaki kuitwa ni watuhumiwa kwani bado mahakama haijawakuta
na hatia.
Lakini kwa sinema hii inayoendelea kuchezwa na jeshi
la polis, ofisi ya DPP na Chadema kwa zaidi ya miaka minne sasa imeanza
kunifanya nianze kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Mosi, nimejiuliza na bado naendelea kujiuliza hii ‘sinema’
inayochezwa na jeshi la polisi, viongozi wa juu wa Chadema na ofisi ya DPP ,
ina nini nyuma yake?
Maana ‘sinema’ ambayo inaendelea kuchezwa na makundi
hayo matatu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, itakamilika lini?Kwani itakumbukwa
kuwa miaka mitatu iliyopita Chadema walifanya mkutano wa hadhara Arusha mjini
na kusababisha polisi kutumia nguvu na watu zaidi ya wawili wakajikuta
wanapoteza maisha na mwishowe Mbowe, Slaa,Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha,
Simson Mwigamba na viongozi wengine walikamatwa na kufunguliwa kesi ya
uchochezi katika mahakama ya Mkoa wa Arusha. Wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Kanda ya Arusha hakuwasilisha hati ya kuwafungia dhamana watuhumiwa hao.
Na matukio mengine kama matatu ambayo polisi
iliwatuhumu viongozi wa Chadema kutoa maneno ya uchochezi na kufanya
mikusanyiko haramu mkoani Arusha, ambapo Mbowe,Godbles Lema na vingozi wengine wana
kabiliwa na kesi za tuhuma kufanya uchochezi zaidi ya moja.Na hadi leo kesi zao
zinaendeshwa kwa kasi ya kinyonga tofauti na kesi nyingine.
Lakini hata siku moja hatujawai kumsikia Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Kanda ya Arusha, kuwasilisha mahakamani hati ya kuwafungia dhamana
washitakiwa hao, au Kamanada wa polisi Mkoa wa Arusha kuwanyima dhamana ya
polisi watuhumiwa hao ambao jeshi la polisi kila kukicha limekuwa likisema
halimuogopi mtu na alimpendelei mtu.
Wakati viongozi hao wa juu wa Chadema wakiipata pepo
hiyo, tungali tukikumbuka hapa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Sheikh
Ponda Issa Ponda na Mukadamu Swalehe ambao walikuwa wakishitakiwa na wenzao 47
walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba
18 mwaka jana, wakikabiliwa na makosa matano ya kula njama,kuingia kwa jinai,
kujimilikisha kwa nguvu kiwanja cha Chang’ombe Markas mali ya kampuni ya
Agritanza Ltd , wizi wa Sh.milioni 59 na uchochezi ambalo lilikuwa linamkabili
Ponda na Mukadamu peke yao.
DPP alimfungia dhamana Ponda na Mukadamu na kweli
walikaa gerezani tangu Oktoba 18 mwaka jana
hadi kesi yao hiyo ilipotolewa hukumu Mei 9 mwaka huu, ambapo Hakimu
Mkazi Victoria Nongwa aliwaachiria huru washitakiwa wote 48 na akamtia hatia
Ponda peke yake tena kwa kosa moja tu la kuingia kwa jinai na akamfunga kifungo
cha nje cha mwaka mmoja.
Itakumbukwa kuwa Machi 21 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa
mahakama ya Kisutu ,Sundi Fimbo aliwahukumu adhabu ya kwenda jela mwaka mmoja
jumla ya wafuasi 53 wa
Sheikh Issa Ponda ,baada ya kuwakuta na hatia ya kufanya kosa la
kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
ya mwaka 2002, kosa la pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu
cha 74 na 75 cha sheria hiyo ambavyo
vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya
mwaka 2002 , kuwa Februali 15 mwaka huu, walitenda kosa hilo la kutaka kuandamana
kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ,Dk.Eliezer Feleshi
kumshinikiza ampatie dhamana Sheikh Ponda,kwani Feleshi alimfungia dhamana
Ponda tangu Oktoba 18 mwaka jana hadi Mei 9 mwaka huu, alipohukumiwa kifungo
cha nje kwa mwaka mmoja.
Wafuasi hao wa Ponda
walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Februali 18 mwaka huu, na
nilikuwepo mwanzo hadi mwisho wa kesi hiyo,na siku ya kwanza tu katika hali
iliyotushitua wengi,wakili Mwandamizi wa Serikali Bernad Kongora alidai kuwa
upelelezi umekamilika na kesho yake yaani Februali 19 mwaka huu, upande wa
jamhuri ukawasomea maelezo ya awali washitakiwa na siku hiyo hiyo shahidi wa
kwanza wa upande wa jamhuri (ZDCO) Mkoa wa Dar es Salaam, Msangi alipanda
kizimbani na kuanza kutoa ushahidi wake.
Hakika kesi ya wafuasi
hao wa Ponda na kesi ya Ponda iliendeshwa kwa kasi sana ambayo ilitufanya
tujiulize ni kwanini kesi hizi mbili zinaendeshwa kwa kasi hiyo, askari wengi
zaidi ya 30 kutanda mahakamani hapo kila siku kesi hizo zinapokuja kusikilizwa.
Na katika kesi hii ya wafuasi 53 wa Ponda, DPP aliwafungia dhamana washitakiwa
watatu wengine wakapewa dhamana na mahakama baadaye kwani mahakama hapo mwanzo
iliwanyima dhamana kwasababu ya hali ya usalama mkoani Dar es Salaam,iliuwa haijatengamaa.
Na itakumbukwa kuwa
wafuasi wa Ponda hawakupewa dhamana ya polisi kwani walikamatwa Ijumaa na Jumatatu
yake waliletwa mahakamani , pia wafuasi
wa Ponda walikamatwa Februlia 15 mwaka huu, tena kama Mukadamu alikaa mikononi
mwa jeshi la polisi kwa siku tano tena bila kupewa dhamana na kisha akafikishwa
mahakamani na DPP akamfungia dhamana kama alivyopewa mamlaka hayo kwa mujibu wa
kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwendeno wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
Na
baadhi ya madai ya Ponda na wafuasi wenzake ni kwamba serikali inawaonea
Waislamu na inawapendelea wakristo,mali za waislamu zinafujwa na viongozi wa
Bakwata na madai mengine mengi.
Sote
ni mashahidi kuwa tuhuma zilizokuwa zikielekezwa na jeshi la Polisi kwa Ponda
na wafuasi wake ambao walishitakiwa nao hazikuweza kusababisha watu kupoteza
maisha, ni vurugu ambazo zilisababisha uvunjifu wa amani wa watu kushindwa
kufanya shughuli zao kwa amani kwa kuhofia maandamano ya wafuasi wale ambayo
yalikuwa hayana kibali cha polisi.
Watu
tunaofiriki sawa sawa tumeanza kujiuliza ni kwanini basi wanapoandamana watu
wanajitambulisha kuwa ni waumini wa dini ya kiislamu bila kufuata sheria za
nchi, jeshi la polisi linawakamata haraka haraka na DPP anaibukia mahakamani na
kuwafungia dhamana washitakiwa hao?
Kwa
nini baadhi ya wafuasi wa Chadema wanapofanya kile kinachodaiwa na jeshi la
polisi kuwa ni mikusanyiko,maandamano haramu ambayo imepigwa marufuku na jeshi
la polisi na polisi wamekuwa wakidai kuwa baadhi ya wafuasi wa chama hicho
wamekuwa wakipambana na polisi, jeshi la polisi linasuasua kuwakamata na
likiwakamata utasikia muda mfupi limewapa dhamana, na hatumsikii DPP wala
Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Arusha akiwasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa
baadhi ya viongozi hao wa Chadema ambao
kila kukicha tumekuwa tukilisikia jeshi
la polisi likiwatuhumu kufanya vurugu na kuwafungulia kesi za uchochezi lakini
kesi hizo zinakwenda mwenendo wa kinyonga ukilinganisha na kesi nyingine kama
hizo za Ponda na wafuasi wake, watuhumiwa ambao wanaelezwa kuwa ni waumini wa
dini ya Kiislamu ambao wanadaiwa kuchoma makanisa eneo la Mbagala?
Au
kwa sinema hii, mnataka waamini ile minong’ono inayoenezwa chini chini kuwa
baadhi ya viongozi wa Chadema ambao wanatuhumiwa na jeshi hilo kufanya vitendo
vya uvunjifu wa sheria wanapata jeuri hiyo kwasababu eti baadhi ya viongozi wa
juu wa jeshi hilo la polisi wanatoka wote mikoa ya Kanda ya Kaskazini ndiyo
maana wanawalea?
Binafsi
siamini katika minong’o hii kwani ninapinga upendeleo wa aina yoyote ile,ubaguzi
wa aina yoyote na uonevu pia.Na ninavyomfahamu IGP-Mwema si mtu wa kuendekeza
ujinga huo na ndiyo maana katika utawala wake ndani ya jeshi hilo, ameweza
kuruhusu askari wengi tu kushitakiwa katika mahakama za kijeshi na mahakama za
uraiani.
Na
mimi nikiwa mwandishi wa habari za mahakamani ni shahidi katika hilo.Na katika
hilo amejitofautisha na watangulizi wake ambapo licha wananchi walikuwa
wakilalamika kuwa kuna baadhi ya askari polisi wanaonea raia, wanashiriki
katika vitendo vya utovu wa nidhamu lakini watangulizi wa IGP-Mwema waliweka
pamba masikioni ,hawakuwachukulia hatua askari polisi wao.
Watanzania
tunapwasa tujiulize kunanini hapa? Kwa nini wananchi wengine wakituhumiwa
kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria,hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa
moja wa kuhusika kutenda uhalifu huo, hatusikii polisi ikiwabembeleza wananchi
hao kwa kuwatangazia kupitia umma kuwa wajisalimishe, ila inapotokea polisi
inawatuhumu viongozi wa Chadema kuhusika kutenda vitendo vya uvunjifu wa sheria
,basi utalisikia jeshi la polisi likijitokeza hadharani kutoa rai ya kutaka
Mbowe na Lema wajisalimishe.
Ninavyofahamu
mimi serikali ina mkono mrefu pindi inapoamua kuweka unafki, ghiliba pembeni na
kuamua kufanyakazi yake, na serikali inamfahamu kila mwananchi nyendo zake na
anapoishi.
Lakini
itakumbukwa kuwa mwaka juzi, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokratic,Mchungaji
Christopha Mtikila aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kuchapisha wakala wa
uchochezi ambao alimuita Rais Kikwete ni gaidi anaungamiza ukristo, kesi hiyo
mwanzoni ilikuwa kwa hakimu Waliarwande Lema, na siku hiyo ya kesi Mtikila
alichelewa kwa zaidi ya saa mbili kuingia mahakamani akakuta kesi hiyo imeishahairishwa
na hakimu Lema kato amri ya Mtikila akamatwe, na ilipofika saa tano, Mtikila
alifika mahakamani hapo akajikuta amewekwa chini ya ulinzi na wanausalama na Mtikila alivyopelekwa mbele ya Hakimu Lema
ajieleze kwanini alichelewa kufika ,Mtikila alijitetea kuwa wakati akiwa njiani
kuja kwenye kesi yake suruali yake ilichanika hivyo alilazimika kurudi nyumbani
kubadilisha nguo kisha ndiyo aje mahakamani lakini utetezi huo ulikataliwa na
alipelekwa rumande.
Hata
hivyo mwaka jana, Hakimu Mugeta ambaye alikuwa akisikiliza kesi hiyo ya Mtikila
baada ya Mtikila kumkataa Lema asiendelee na kesi yake kwani hana imani naye na
akamtaja hakimu Lema kuwa ni mtu katili asiyejali utu wa watu wengine
,alimwachilia huru Mtikila kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri umeshindwa
kuthibitisha kesi hiyo.
Turejee kwenye kauli ya ‘Msomi wa Sheria ’ Mizengo Pinda,kwanza
binafsi ninaunga mkono kauli hiyo na
ninaamini wale wenye akili timamu, ambao
hawajawahi kupata magonjwa yanaombatana na mtikisiko wa ubongo na elimu zao
siyo za kugelezea mitihani watakubaliana na makala yangu hii ambayo inaunga
mkono kauli hiyo Pinda.
Na kwa wale mambumbumbu wa sheria watampinga Pinda tena
bila kutoa vielelezo vya kumpinga au watajitutumua kwa kutumia Ibara 13(6) (b)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ambapo ibara hiyo
inasema ‘mshitakiwa yoyote anayeshitakiwa kwa makosa ya jinai asichukuliwe kuwa
ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta
na hatia’.
Lakini atakayetumia ibara hiyo kumpinga kauli ya Pinda
atakuwa amekosea , kwani Ibara hiyo inatumika pale tu mshitakiwa aliyeshitakiwa
kwa makosa ya jinai.Na kwa mujibu wa agizo la Pinda ni amewataka polisi kutumia
nguvu kuwakamata wale wote wanaokaidi amri za jeshi hilo na kuvunja sheria za
nchi na kisha kuwafikisha kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Mkoa husika kwaajili ya ofisi hiyo ya Mwanasheria Mkuu
wa serikali iwafikishe mahakamani.
Kwani kwa zaidi ya miaka mitano sasa, Jeshi la polisi
limeondolewa jukumu la kuwafungulia kesi washitakiwa wa makosa ya jinai badala
yake limebakidhiwa majukumu mengine yakiwemo majukumu ya kupeleleza matukio ya
uhalifu,kuwakamata.
Na hivyo basi jukumu la kuwafikisha watuhumiwa wa kesi za
jinai mahakamani limekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kama
ilivyoanishwa kwenye kifungu cha 90 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
ya mwaka 2002.
Binafsi nasema kauli hiyo ya Pinda ni kauli yenye afya
na imekidhi kiu ya watanzania wengi
wenye akili timamu tuliokuwa tukiisubiri kwa hamu na ama kwa hakika kauli hiyo
inaungwa mkono na kifungu cha 21(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
ya mwaka 2002, ambacho kifungu hicho
kinawataka polisi kutumia nguvu kuwakamata wale wote wanavunja kwa makusudi sheria za nchi.
Lakini licha ya mimi
binafsi kuunga mkono kauli hiyo ya Pinda, lakini napenda niseme wazi baadhi ya
viongozi wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete
wamekuwa ni ndumila kuwili, hawana msimamo na maelekezo wanayoyatoa kwa
watendaji wao wa chini, kwani ni
aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Rick Mahalu ambaye alifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na wizi Euro milioni 3
katika ununuzi wa jengo la ubalozi wetu nchini Italia,muda mfupi tu tangu
serikali ya Rais Kikwete iingie madarakani.
Na mawakili wa TAKUKURU
walidai Mahalu hakupewa idhini na serikali ya kununua jengo
hilo kwa njia ya mikataba miwili na kwamba serikali ilikuwa haina taarifa za
yeye kununua jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili.
Lakini katika utetezi wake Mahalu na shahidi wake Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu , Ilvin Mugeta,binafsi nilikuwepo
kwani nimeudhuria kesi hiyo mwanzo hadi mwisho. Mahalu alionyesha vielelezo
vyake vinavyoonyesha kuwa serikali ilibariki ununuzi wa jengo hilo kwa njia ya
mikataba miwili, na Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa ni Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,ndiye aliyempa nguvu ya kisheria (Power of
Attoney), Mahalu kuendelea na shughuli zote za ununuzi wa jengo hilo.
Na Rais Mkapa katika ushahidi wake, alieleza kuwa yeye ndiye
aliyekuwa kiongozi mkuu wa mhimili wa serikali na kwamba serikali yake ya awamu
ya tatu ilimwagiza Mahalu anunue jengo la ubalozi wetu kwanjia ya mikataba
miwili na kwamba anashangazwa ni kwanini Mahalu ameshitakiwa kwa makosa hayo
wakati ni serikali yake ya awamu ya tatu ambayo Kikwete alikuwa ni mjumbe wa
Baraza la mawaziri na baraza hilo la mawaziri ililidhia Mahalu aendelee na ununuzi wa jengo la ubalozi
wetu kwa utaratibu alioutumia Mahalu kununua jengo hilo.
Lakini Agosti 9 mwaka jana, Hakimu Mugeta alitoa hukumu ya
kesi hiyo ya kihistoria na kumwachiria huru Mahalu na Grace Martin baada ya kuona upande wa jamhuri umeshindwa
kuthibitisha kesi hiyo.Hata hivyo Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer
Feleshi hajaridhishwa na hukumu hiyo na amekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam, na rufaa hiyo itaanza kusikilizwa rasmi Julai Mosi mwaka huu,
mbele ya Jaji John Utamwa.
Kwa hiyo hukumu hiyo ya kesi ya Mahalu, imetufundisha kuwa
ndani ya serikali kuna viongozi au watendaji ambao hawapo njia moja, wanafki na
wazandiki wanatoa maelekezo kwa watendaji wao wa chini watekeleze jambo fulani,
na watendaji hao wakishatekeleza jambo hilo mwisho wa siku ama wanawaundia tume
kuwachunguza, kuwafukuza kazi,au kuwafikisha mahakamani kitendo ambacho hivi
sasa kimewafanya baadhi ya watendaji wa baadhi ya vyombo vya dola tunaozungumza
nao kutotilia mkazo maelekezo yanayotolewa kwao na viongozi wa kisiasa na
wanawadharau sana viongozi wa kisiasa.
Nimalizie kwa kusema hivi Chadema, CUF, CCM, NCCR na viongozi
wa vyama vyote vya siasa vitapita, ila Tanzania yetu itabaki. Hivyo watanzania
wote tuukatae uhuni na umwagaji damu wa
aina yoyote unaofanywa ama na wanasiasa, wananchi wanaokubali kutumiwa na
wanasiasa uchwara, au njaa zao zinawatuma kufanya matendo ya uvunjifu wa amani
ili wapate ujira.
Na vyombo vya dola bado ninaimani navyo kuwa vinapoamua
kufanyakazi yake kikamilifu vinafanya.Na viomba vitambue kuwa hivi sasa tayari
sifa ile ya amani ambayo Tanzania tuliyokuwa tukijivunia imeishaingiwa na doa
,hivyo ni kazi kwenu wanausalama na wananchi kwa ujumla kukomesha wale wote
wanaotia doa amani yetu kwa gharama zozote ilimradi amani yetu iendelee kudumu.
Baba wa Taifa, marehemu Julias Nyerere na makomredi wenzake
wakati wanatafuta uhuru wa Taifa la Tanganyika, hawakutumia silaha kutafuta uhuru, walitumia akili, weledi na siasa safi hadi wakatuletea
uhuru.
Sasa inakuwaje leo hii wanatokea wahuni wachache tu ambao hata mkononi
hawajai ,hawana hata uwezo wala kufanya ushawishi wa kutengeneza uasi ndani ya
majeshi yetu wakaweza kupata silaha na kwenda kujificha msituni, wawe na jeuri
ya kila kukicha kuanzisha matukio ya uvunjifu wa amani ambayo yanasababisha pia
wananchi wenzetu kupoteza maisha, kujeruhiwa,makazi ya watu kuharibiwa,
shughuli za kiuchumi kusimama, watu kuanza kuishi kwa hofu utafikili wanaopa
Barazani.Maana siku zote mtu anayeoga barazani anakuwa na wasiwasi kuwa kuna
mtu anaweza kupita akamtazama maungo yake.
Vyombo vya dola mmeapa kuilinda serikali ya Jamhuri ya
Muungano na wananchi wake kwa hali yoyote ile, sasa tunawaomba sasa mtumie
mafunzo yenu mliyopewa mkiwa katika vyuo vya kijeshi kuwashughulikia wale wote
wanaojihusisha na uvujifu wa amani kwani wahalifu kama wahalifu wengine bila
kujali mharifu huyo ni kiongozi wa serikali, chama cha siasa au mhalifu huyo
anafahamiana na kiongozi fulani.Tumechoka na matukio haya ya kishenzi na
kikatili.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook: happy katabazi
0716 774494
Juni 21 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment