Header Ads

CHE MUNDUGWAO AKWAMA MAHAKAMANI


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la dhamana lilowasilishwa mbele yake na Msanii wa muziki wa asili nchini Chigwele Che Mundugwao na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya wizi wa Paspoti 26 kwa maelezo kuwa mahakama haiwezi kumpatia dhamana licha makosa yanayomkabili yana dhamana kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi amewasilisha hati ya kuwafungia dhamana.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambaye hakimu huyo amepangwa Ijumaa iliyopita kuanza kuendelea kusikiliza kesi hiyoi ikiwa ni Alhamisi iliyopita Hakimu Mkazi Alocye Katemana ambaye alipangwa kuaza kusikiliza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa rasmi Juni 3 mwaka huu, alipotangaza kujitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
“Katika kesi hii DPP-Dk.Feleshi Juni 6 mwaka huu, aliwasilisha upya hati ya kuwafungia dhamana washitakiwa wote , na kisheria pale DPP anapowasilisha hati hiyo ya kuwafungia dhamana washitakiwa chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, mahakama inakuwa imefungwa mikono kwa maana kuwa mahakama inakuwa haina mamlaka ya kuipinga hati hiyo ya DPP:

“Na kwa sababu hiyo mahakama hii inatupilia mbali ombi la dhamana lilowasilishwa na wakili wa washitakiwa Peter Kibatara kwasabababu hiyo niliyoitaja hapo juu na ninaiarisha kesi hii hadi Juni 24 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na ninaamuru washitakiwa wote warejeshwe rumande’alisema Hakimu Fimbo.

Juni 6 mwaka huu, hakimu Katemana aliyekuwa akisikiliza hiyo tangu awali , alijikuta akishindwa kutekeleza amri yake aliyoitoa Juni 5 mwaka huu,  ya kuwapatia dhamana washitakiwa hao kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi  Juni 5 asubuhi aliwasilisha  upya  hati ya kuwafungia dhamana washitakiwa hao.

Sambamba na hiyo Hakimu Katemana siku hiyo alitangaza kutojitoa  kuendelea kusikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa Juni 3 mwaka huu, na akasema jalada la kesi hiyo linarudishwa kwa uongozi wa mahakama hiyo ili apangiwe hakimu mwingine wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo na akaiarisha kesi hiyo hadi leo.

Juni 5 mwaka huu,  Hakimu Katemana alitoa uamuzi wa kutupilia mbali hati hiyo ya DPP iliyowasilishwa chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ya kuwafungia dhamana washitakiwa hao ambao wakili Mwandamizi wa Serikali Lasdlaus Komanya kuiwasilisha kwaniaba ya DPP , kwa maelezo kuwa hati hiyo iliwasilisha kinyume na sheria kwani haikuwasilishwa kwanza katika ofisi ya usajili ya mahakama hiyo badala yake wakili Komanya aliiwasilisha moja kwa moja mahakamani na kisha hakimu akatoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa hao juzi ambapo walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na akaamuru washitakiwa warudishwe gerezani na waletwe jana mahakamani  hapo ili watimize masharti ya dhamana na kisha wapatiwe dhamana.

Mbali na Che Mundugwao ,washitakiwa wengine ni ofisa  Manunuzi  wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius (37) na mfanyabiashara, Ally  Jabir  (34) wanaotetewa na wakili Peter Kibatara.

Juni 5 mwaka huu, Hakimu Katemana akitoa uamuzi wake  wa kuwapatia dhamana washitakiwa ambapo DPP aliwasilisha hati ya kuwafungia dhamana, Katemana  alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama yake imebaini kuwa hati hiyo ya DPP iliwasilishwa bila kufuata taratibu za kisheria kwani kisheria hati hiyo ya DPP ilipaswa kwanza ifikishwe kwenye ofisi ya usajili wa mahakama ili hiyo hati isajiliwe na mahakama hiyo kwanza kabla ya wakili wa serikali kuitoa hati hiyo mahakmani muda mfupi baada ya kumaliza kuwasomea mashitaka washitakiwa.

Hakimu Katemana alisema baada ya kuikataa hati hiyo ya DPP ya kuwafungia dhamana, mahakama yake inawapatia dhamana washitakiwa kwa masharti ya fuatayo kwamba kila mshitakiwa ili apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili  wakiaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh.milioni 10.Lakini hata hivyo washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana akaamuru warudishwe rumande hadi jana  ili waje watimize masharti ya dhamana.

Mei 3 mwaka huu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya  mbele ya Hakimu Mkazi  Aloyce Katemana aliwasomea mashitaka washitakiwa hao na kudai kuwa wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha  384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu , Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma,  katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Komanya alidai kuwa washitakiwa  Chigwele, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam ,walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.

Kuhusu  Che Mundugwao,wakili Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa akimiliki  paspoti 12  za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .

Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa Mei , mwaka huu  Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili  zenye majina ya watu wengine sababu yoyote ya msingi.
Komanya aliendelea kuwa Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally , alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua kuwa si kweli.

Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,   Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya Uhamiaji wakati si kweli.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 11 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.