Header Ads

KORTI YATOA MASHARTI YA DHAMANA KWA CHE MUNDUGWAO


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi iliyokuwa imemfungia dhamana Msanii wa muziki nchini, Chigwele Che Mundugwao 46 na wenzake wanaokabiliwa na jumla ya makosa manne likiweko kosa la wizi wa paspoti 26.

Mbali na Che Mundugwao ,washitakiwa wengine ni ofisa  Manunuzi  wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius (37) na mfanyabiashara, Ally  Jabir  (34) wanaotetewa na wakili Peter Kibatara.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Alocye Katemana  ambapo alisema kesi hiyo ilifunguliwa rasmi Mei 3 mwaka huu, na DPP kupitiwa wakili wa serikali Mwandamizi Lasdlaus Komanya  baada ya kuwasomea mashitaka washitakiwa aliwasisha hati hiyo  iliyosainiwa na DPP ya kuwafungia dhamana washitakiwa wote chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, lakini wakili wa washitakiwa Kibatara alipinga hati na kudai dhamana na  haki ya washitakiwa.

Hakimu Katemana akitoa uamuzi wake jana alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama yake imebaini kuwa hati hiyo ya DPP iliwasilishwa bila kufuata taratibu za kisheria kwani kisheria hati hiyo ya DPP ilipaswa kwanza ifikishwe kwenye ofisi ya usajili wa mahakama ili hiyo hati isajiliwe na mahakama hiyo kwanza kabla ya wakili wa serikali kuitoa hati hiyo mahakmani muda mfupi baada ya kumaliza kuwasomea mashitaka washitakiwa.

“Na kwa mazingira ya kesi hii, wakili wa serikali halishindwa kufanya hivyo kwani aliileta moja kwa moja hati hiyo hapa mahakamani bila ya kwenza kuipeleka kwenye ofisi ya usajili ya mahakama hii isajili kisha ndiyo aje kuitoa mahakama…na kwa sababu hiyo mahakama hii inaitupilia mbali hati hiyo ya DPP iliyokuwa inataka mahakama hii iwafungie dhamana washitakiwa kwasababu hati hiyo imeletwa mahakamani bila kufuata taratibu”alisema Hakimu Katemana.

Hakimu Katemana alisema baada ya kuikataa hati hiyo ya DPP ya kuwafungia dhamana, mahakama yake inawapatia dhamana washitakiwa kwa masharti ya fuatayo kwamba kila mshitakiwa ili apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili  wakiaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh.milioni 10.Lakini hata hivyo washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana akaamuru warudishwe rumande hadi leo ili waje watimize masharti ya dhamana.

Mei 3 mwaka huu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya  mbele ya Hakimu Mkazi  Aloyce Katemana wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha  384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.

Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu , Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma,  katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Komanya alidai kuwa washitakiwa  Chigwele, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam ,walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.

Kuhusu  Che Mundugwao,wakili Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa akimiliki  paspoti 12  za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .

Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa Mei , mwaka huu  Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili  zenye majina ya watu wengine sababu yoyote ya msingi. 
Komanya aliendelea kuwa Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally , alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua kuwa si kweli.

Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,   Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya Uhamiaji wakati si kweli.Wakili Komanya alidai kuwa kutokana na asili ya makosa hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana chini ya kifungu cha 148 (4) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 na ataiondoa hati hiyo pale atakapoona hipo sababu ya kufanya hivyo ila kwasasa amefunga dhamana ya washitakiwa hao. 

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi , Juni 6 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.