Header Ads

KESI YA MAHALU: USHAHIDI WA MKAPA TISHIO


*MAWAKILI WAVUTANA CHANZO CHA KUVUJA KWAKE

Na Happiness Katabazi

WAKATI Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kuanza kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya euro milioni 2, sawa na sh bilioni 3 inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na Grace Martin, ushahidi wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, umeivuruga serikali ya Rais Kikwete.


Mvurugano huo ulijionyesha jana mahakamani baada ya wakili mkuu wa serikali, Ponsian Lukosi, anayesaidiwa na wakili mwandamizi toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln, kuwasilisha ombi la kuitaka mahakama itoe mwongozo wa kesi hiyo kwa madai kuwa mawakili wa Mahalu, Mabere Marando na Alex Mgongolwa, wamekuwa wakitoa mwenendo wa kesi hiyo kwenye vyombo vya habari kabla ya kusikilizwa na mahakama hiyo.

Akitolea mfano wa ushahidi wa kiapo wa Mkapa, wakili huyo wa serikali alidai kuwa ulitolewa kwenye vyombo vya habari kabla haujawasilishwa mahakamani.

Aliyataja gazeti la Mwanahalisi la Aprili 27 mwaka huu, Toleo Na.239, Tanzania Daima, Mwananchi, The Citzen na Mtanzania la Mei 6 mwaka huu kwamba yaliandika habari kuhusu ushahidi wa Mkapa kabla ya kufikishwa mahakamani.

“Tunavyoona sisi ni kwamba kama kesi inakuja mahakamani, kuna haja gani sisi maofisa wa mahakama kwenda kuzungumza kesi hiyo na vyombo vya habari halafu ndipo tuje mahakamani kuendelea na kesi? Upande wa jamhuri kwa namna moja ama nyingine tunaona huko ni kuingilia uhuru wa mahakama,” alidai Lukosi.

Wakili Lukosi alilibana gazeti la Mwanahalisi kwamba ndilo lililochapisha hati ya kiapo cha Rais Mkapa kabla hakijawasilishwa mahakamani na mwisho wa habari hiyo, likatoa hukumu kabla ya mahakama kufanya hivyo.

Alinukuu sehemu ya gazeti hilo ambayo ilisomeka hivi ‘Jamhuri kwa hati hiyo ya kiapo cha Mkapa akiwa Mtendaji Mkuu wa serikali ya Tanzania, alikuwa akielewa kila kitu kilichokuwa kikitendeka chini ya uongozi wake. Upande wa Jamhuri katika kesi ya Mahalu, ujiandae kufungasha jamvi la mashtaka’.

Aliendelea kulalamika kuwa “Wakati gazeti hilo likichapisha habari hiyo, kiapo cha Mkapa kilikuwa hakijawalishwa mahakamani na tumekuwa tukijiuliza kwa nini mawakili wa utetezi, wenye hati hiyo hawajajitokeza kulalamika kwamba ushahidi wao umevuja kwenye vyombo vya habari wakati bado hawajauwasilisha mahakamani?!” alihoji Lukosi.

Akijibu kombora hilo mahakamani hapo, wakili Marando alidai kuwa yeye ndiye aliyeandaa hati hiyo ya kiapo cha Mkapa na kabla ya kuiwasilisha mahakamani, aliiwasilisha kwa baadhi ya maofisa wa serikali kwa sababu ya unyeti wa hati hiyo kabla ya Aprili 27 mwaka huu na ndiyo siku gazeti la Mwanahalisi lilichapisha taarifa ya kiapo hicho.

Marando aliiambia mahakama kuwa yeye na wakili mwenzake, walishtushwa kuiona taarifa hiyo gazetini na alifanya mawasiliano na mhariri kujua walikozipata nyaraka hizo bila mafanikio.

‘Mheshimiwa hakimu na mahakama yako tukufu, katika hili wa kulaumiwa ni serikali. Wao ndio waliovujisha nyaraka za kiapo hicho kwenye vyombo vya habari kwa sababu mimi ndiye niliyeiandaa na kabla ya kuiwasilisha mahakamani, nilipeleka kwa siri kubwa kwa maofisa wa serikali na wakati ipo mikononi mwa maofisa wa serikali, haijarudi kwangu kwa ajili ya kuendelea kuiandaa, ndipo nyaraka hizo zilipovuja kwenye vyombo vya habari,” alisema Marando.

Wakili huyo maarufu nchini, alidai kuwa kutokana na umaarufu wa kesi hiyo ya Mahalu, hakuna mwandishi wa habari makini ambaye angekubali kuacha kuichapisha kabla haijafikishwa mahakamani.

Marando alidai kuwa kama ni onyo, ionywe serikali kwa kuvujisha nyaraka hizo na aliiomba mahakama isikubali ombi hilo kwa madai kuwa lina lengo la kunyamazisha vyombo vya habari visiendelee kuripoti kesi hiyo.

Akitoa uamuzi wa hoja hiyo iliyovuta hisia za wengi mahakamani hapo, Hakimu Mugeta alisema kwa mamlaka aliyonayo hawezi kutoa mwongozo wala onyo kwa vyombo vya habari na kuamua kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24. Washtakiwa hao sasa wataanza kujitetea Julai 8 hadi 11.

Awali kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea, lakini walishindwa kufanya hivyo kwa kuwa mawakili wa Mahalu walikusudia kuwasilisha maombi mawili.

Akiwasilisha maombi hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elvin Mugeta, Marando kwanza aliiomba mahakama iuingize kwenye jalada la kesi hiyo utetezi wa maandishi wa Rais mstaafu Mkapa ambao umeandaliwa kwa njia ya kiapo kumtetea Mahalu.

Katika ombi la pili, Marando aliiomba mahakama iwape mwenendo mzima wa kesi ili wakaandae utetezi wa wateja wake kwani mwenendo wa awali, una makosa ya kimaandishi.
Akitolea uamuzi wa maombi hayo, Halimu Mugeta alisema si muda muafaka kwa mahakama na pande zote mbili kuanza kuzungumzia ushahidi wa Mkapa kwa sababu hata washtakiwa wenyewe hawajaanza kujitetea.

“Kuhusu ombi la pili, mahakama hii imekubaliana na ombi hilo na kuahidi ifikapo hadi Juni 4, mahakama itakuwa imeshawapatia mwenendo sahihi wa kesi hiyo tangu ilipoanza hadi pale mahakama ilipowaona washtakiwa wana kesi ya kujibu,” alisema Hakimu Mugeta.

Hivi karibuni Mkapa alitoa utetezi wake mahakamani kwa njia ya maandishi ambao unaweza kuandika historia mpya katika mwenendo wa kesi nchini.

Katika hati ya kiapo chake cha Machi 31, mwaka huu, ambayo imeandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Nyaraka (The Registration of Documents Act, Cap. 117 of 2002), Mkapa anaeleza kuwa kila kilichofanywa na Mahalu kilikuwa sahihi na kilikuwa na baraka ya serikali aliyokuwa akiingoza toka mwaka 1995-2005.

Ushahidi huo wa Rais Mkapa umeorodhesha maelezo yake yaliyoainishwa katika vipengele 13.
Mkapa katika utetezi wake huo anadai kuwa mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi lililoko katika mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Rome ulizingatia sera ya serikali ya upatikanaji au ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi na makazi na kwamba ulizingatia maslahi ya taifa.

Hati hiyo ya kiapo ambayo tayari wakili Marando amesema ameishaiwasilisha pia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, inaanza kwa kusema, “Mimi Benjamin Mkapa, mtu mzima, Mkristo, mkazi wa Dar es Salaam, ninaapa kama ifuatavyo, ’nilikuwa Rais mtendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viliwili mwaka 1995-2005 na nina uhakika wa yote haya nitakayosema ndani ya kiapo hiki.’”

Katika kiapo hicho Mkapa anadai pia kuwa alifahamishwa na watendaji wa serikali aliyokuwa akiiongoza jinsi mchakato ulivyofanyika na ripoti ya uthamini wa serikali iliyotumika katika kufikia hatua ya kununua jengo hilo la ubalozi.

Anadai kuwa tathmini ya jengo hilo ambalo Mahalu anadaiwa kufanya udanganyifu na wizi kwa kulipa fedha kinyume na ilivyotajwa katika mkataba ambao ulifanywa na serikali ya awamu ya tatu kupitia wizara mbili tofauti, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Ardhi na Maendeleo Mijini.

Anaendelea kudai anatambua kuwa ripoti ya serikali ya uthamini wa jengo hilo iliandaliwa na Wizara ya Ujenzi kwa kiwango cha dola za Marekani milioni 3 na Wizara ya Ardhi kwa thamani ya euro milioni 5.5.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa wa aina mbili, mmoja ni rasmi na mwingine wa kibiashara na kuongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu ya serikali ya Italia na kuwa hilo lilifanyika kwa baraka za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shahidi huyo wa Mahalu anadai pia kuwa kwa mujibu wa kiapo chake anakumbuka vyema taarifa ya serikali iliyotolewa bungeni Agosti 3, 2004 iliyosema na kuthibitisha kuwa taratibu zote zinazohusiana na manunuzi ya jengo kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, zilifuatwa na kwamba muuzaji wa jengo hilo alilipwa fedha zote.

Akimwelezea Mahalu katika utetezi wake, Mkapa alidai katika kipindi chote alichokuwa Rais wa nchi alifanya kazi na mshtakiwa huyo katika nyadhifa mbalimbali za utumishi wa umma na kwamba mshtakiwa huyo ni mtu wa tabia njema, mkweli, mwaminifu na mchapaji kazi.

Katika kesi hiyo namba 1/2007, Mahalu na Martin wanatuhumiwa kwa wizi wa sh bilioni 3 katika ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome.

Mbali na Mkapa, mashahidi wengi wanaotarajiwa kumtetea Mahalu na mwenzake ni Rais Kikwete, kwani wakati akinunua jengo hilo ndiye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mashahidi wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, ambaye pia anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bil. 11.7.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 1 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.