Header Ads

HUKUMU KESI YA EPA KUSOMWA LEO

.MARANDA NA MWENZAKE KUCHEKA AU KULIA KISUTU
Na Happiness Katabazi

JOPO la Mahakimu Wakazi watatu leo linatarajia kuketi katika viti vitatu vya enzi ndani ya ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kumsomea hukumu Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda (53) na mpwa wake Farijala Hussein ambao wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.

Jopo hilo linaloundwa na Mahakimu wakazi Saul Kinemela, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Focus Bambikya na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Elvin Mgeta.

Washtakiwa hao ambao wanatetewa na wakili machachari Majura Magafu wanakabiliwa na kesi ya jinai Namba 1161/2008 kwa makosa ya kula njama,kuwasilisha nyaraka za uongo, za kughushi, wizi na kujipatia ingizo la Sh 1,864,949,294.45.

Katika shitaka hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa Benki Kuu zilizoonyesha kampuni yao ya Kiloloma & Brothers ambayo hata hivyo haijawahi kusajiliwa kwa msajili wa makampuni nchini (BRELA), kwamba imepewa idhini na kudai deni la kampuni ya nje ya M/S BC Cars Export huku wakijua si kweli.

Wakati macho na masiko ya Watanzania yameelekezwa mahakamani hapo katika kesi hiyo itakayotolewa hukumu leo, pia kesi nyingine mbili zinazowakabili washtakiwa hao zitakuja mahakamani hapo kwaajili ya kuendelea kusikilizwa. Nyingine itakuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasilisha majumuisho yao ya kumuona mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu.

Ikiwa hukumu hiyo itatolewa kama ilivyopangwa na jopo hilo Januari 26 mwaka huu, kesi hiyo ya jinai Na.1161/2008 itakuwa ni kesi ya kwanza kati ya jumla ya kesi 11 za wizi wa akaunti ya EPA kufunguliwa mahakamani hapo.

Kesi hizo zilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), Eliezer Feleshi kwa kishindo kuanzia Novemba 4 mwaka 2008 dhidi ya washtakiwa mbalimbali wakiwemo mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel na wenzake na baadhi ya maofisa wa BoT ambao bado kesi zao zinaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

Mbali na kesi hiyo, Maranda na Farijala wanakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa Sh milioni 207 ambapo anashtakiwa yeye na maofisa wa BoT, Mkuu wa Idara ya EPA, Iman Mwakosya na Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo Ester Komu, na Katibu wa Benki Bosco Kimela.

Katika kesi hiyo ya wizi Maranda anadaiwa kutumia nyaraka za kughushi kuonyesha kampuni yake ya Rashaz Tanzania kuwa imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Rashaz T Ltd na kisha kujipatia ingizo hilo la Sh milioni 207 huku akijua si kweli.

Kesi ya tatu ya jinai ni kesi Na. 1164/2008 ya wizi wa shilingi bilioni 3.8 katika akaunti hiyo ambayo inasikilizwa mbele ya jaji Beatrice Mutungi, Hakimu Mkazi Samwel Karua na Elvin Mugeta.

Katika kesi hiyo, washitakiwa Farijala, Maranda, Iman Mwakosya, Ester Komu, Ajay Somani na Sophia Lalika walitumia kampuni ya Mibale Farm kuonyesha imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Lakshmi Textile Mills co. Limited ya India huku wakijua si kweli.

Juni 11 mwaka 2009, mahakama hiyo ilimuona Maranda na Farijala ambao wanakabiliwa na jumla ya kesi nne za wizi katika EPA, kuwa wana kesi ya kujibu na kwamba upande wa Jamhuri unaowakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface aliyekuwa anasaidiwa na Timon Vitalis, Frederick Manyanda, Ephery Cedrick na Michael Lwena na Oswald Tibabyekomya, umeweza kuthibitisha kesi yao.

Juni 6 mwaka 2009, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Boniface aliwasilisha majumuisho ya kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wote hao wana kesi ya kujibu, kwani Jamhuri imeweza kuthibitisha kesi hiyo na kwa hiyo washtakiwa hao wana kila sababu ya kujibu kesi inayowakabili.

Aidha, Aprili 29 mwaka 2010, Rajabu Maranda alipanda kizimbani kutoa utetezi wake katika kesi hiyo ambayo leo inatolewa hukumu ambapo aliieleza mahakama hiyo kuwa alichokuwa akikizingatia katika mchakato wa kudai deni katika (EPA) ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.

Itakumbukwa kuwa serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) Feleshi iliwaburuza mahakamani watuhumiwa wa wizi katika akaunti ya EPA, baada ya tuhuma kuibuliwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoo, kelele za wananchi na wafadhili, hali iliyosababisha Rais Kikwete kuunda Tume ya uchunguzi wa wizi huo ambayo ilimshirikisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP-Said Mwema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dk. Edward Hosea na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa sasa amestaafu, Johnson Mwanyika.

Tume hiyo iliwahoji watuhumiwa na hatimaye kuwafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.