Header Ads

JAJI ATAKA USHAHIDI KESI YA MPENDAZOE,MAHANGA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imezitaka pande mbili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa Jimbo la Segerea iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Fred Mpendazoe (CHADEMA) dhidi ya Mbunge wa sasa, Dk. Makongoro Mahanga (CCM) na wenzake kuwasilisha haraka iwezekavyo orodha ya nyaraka za ushahidi wanazokusudia kuzitumia katika kesi hiyo.


Mbali na Dk. Mahanga anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambao nao wanatetewa na wakili wa serikali, Patience Ntwina. Mpendazoe anatetewa na wakili wa kujitegemea, Peter Kibatala.

Jaji Profesa Ibrahim Juma, alitoa rai hiyo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa na kuongeza kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, kesi ya uchaguzi inapaswa imalizike ndani ya miezi 12 tangu ilipofunguliwa. Mpendazoe alifungua kesi hiyo Novemba mwaka jana mahakamani hapo.

“Kesi hii ni ya uchaguzi na imefunguliwa chini ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inataka kesi imalizike kusikilizwa ndani ya miezi 12 tangu ilipofunguliwa …sasa ili twende na muda huo, mahakama inazitaka pande zote kuwasilisha orodha ya nyaraka za ushahidi haraka iwezekanavyo,” alisema Jaji Profesa Juma.

Kabla ya Jaji Juma kutoa rai hiyo, wakili wa serikali, Patience Ntwina, alisema kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo kuomba mahakama iwapatie siku 14 kuanzia jana, ili waweze kuwasilisha majibu ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo Juni 20 mwaka huu.

Kuwasilishwa mahakamani kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho, kulitokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa na Jaji Juma, Juni 6 mwaka huu, ambapo aliamuru hati ya madai ikafanyiwe marekebisho kwa kuviondoa vituo 10 vya kupigia kura ambavyo mlalamikaji hakuvitaja kwa majina.

Baada ya kufanyiwa marekebisho, Wakili Kibatala alisema hivi sasa hati hiyo inasomeka kuwa wamebakiwa na vituo vya kupigia kura 249 ambapo vituo 120 ni vya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ni vya Kata ya Vingunguti.

Jaji Juma aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 12 mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa na kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Novemba mwaka 2010 Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza mbunge wa sasa Dk. Mahanga kuwa ndiye mshindi kwa sababu uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 23 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.