Header Ads

MAHITA AUMBUKA TENA


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, Omari Mahita, dhidi ya aliyekuwa msichana wake wa kazi anayedaiwa kuzaa naye.


Katika rufaa hiyo, Mahita alikuwa akiiomba Mahakama Kuu itengue hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ambayo ilimuamuru kupeleka gharama za matunzo ya mtoto wake Juma Omary Mahita (14) mtoto anayedaiwa kuzaa na msichana huyo Rehema Shabani.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Fauz Twaib ambapo alisema rufaa hiyo ya madai Na.149/2009 iliwasilishwa mahakamani hapo na mrufani (Mahita) anayetetewa na Charles Semgalawe dhidi ya mrufaniwa (Rehema) anatetewa Frederick Mkatambo toka Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) akipinga hukumu ya kesi ya madai Na.9/2007 iliyotolewa mwaka 2009 na Hakimu Mkazi Kihawa.

Katika rufaa hiyo Mahita aliwasilisha sababu nne za rufaa ambazo ziliiomba Mahakama Kuu itengue hukumu hiyo ya mahakama ya chini.

Hata hivyo katika hukumu yake, Jaji Twaib, alisema amezisoma sababu zote nne, na hukumu ya mahakama ya wilaya ya Kinondoni na amebaini sababu zote hizo ni dhaifu na zimeshindwa kuishawishi mahakama hiyo iikubali rufaa hiyo na kuongeza kuwa kwa mantiki hiyo mahakama hiyo inakubaliana na hukumu iliyokwishatolewa na hakimu Mkazi Kihawa kuwa ilikuwa ni hukumu iliyokidhi matakwa yote ya kisheria.

Jaji Twaib alisema kwa mujibu wa hati ya madai ya rufaa hiyo, wakili wa mrufani anataja sababu ya kwanza ya kukata rufaa kuwa kesi iliyofunguliwa na Rehema dhidi ya Mahita katika mahakama ya Kinondoni ilifunguliwa nje ya muda
hivyo ilikuwa ikikinzana na kifungu cha tatu cha Sheria ya watoto Waliozaliwa nje ya ndoa (Affiliation Act: Cap 273.

Kwa mujibu wa wakili wa Mahita, alidai kifungu hicho kinataka mwanamke aliyezaa nje ya ndoa atapaswa kumfungulia kesi mzazi mwenzie ndani ya miezi 12 baada ya mtoto kuzaliwa lakini Mrufaniwa (Rehema ) alifungua kesi ile miaka tisa baada ya Juma kuzaliwa.

Katika hilo Jaji alipinga sababu hiyo akisema, “Mahakama hii inatupilia mbali sababu hiyo kwani haina ukweli wala mantiki ya kisheria kwani kifungu hicho cha Sheria ya Watoto waliozaliwa nje ya ndoa, kinasema mwanamke anaweza kuchagua kumfungulia kesi mahakamani mwanamme anayedai amemzalia mtoto na hataki kumpa matunzo ndani ya miezi 12 kuanzia mtoto alipozaliwa au muda wowote ule baadaye,” alisema Jaji Twaib.

Aidha katika sababu ya pili ya wakili huyo wa Mahita, Semgalawe alidai Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilikosea pale ilipoukubali ushahidi wa mrufaniwa kuwa Mahita alikataa kwenda kupimwa kipimo cha Vinasaba (DNA) kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Mkemia Mkuu wa Serikali aliiandikia mahakama ya Kinondoni barua ya Mei 5 mwaka 2009 ambayo inasomeka hivi.

“Naijulisha mahakama yako kuwa ofisi yangu imeshindwa kutekeleza amri iliyotolewa na mahakama yako kwasababu Omar Mahita hajatokea ofisini kwangu na Rehema na mwanae Juma ndiyo wamekuwa wakifika ofisini kwangu kuanzia Aprili 24-27-30 na Mei 4 - 5 mwaka 2009 kwaajili ya kufanyiwa kipimo hicho,” inasomeka barua hiyo ya Mkemia Mkuu kwa mahakama ya wilaya ya Kinondoni.

Wakili Semgalawe alidai pia mrufaniwa katika mahakama ya chini alitoa ushahidi unaonyesha mkanganyiko wa tarehe; akisema yeye alimzaa mtoto wake Machi 1997 na kwamba mrufaniwa aliondoka nyumbani kwa mrufani Oktoba 1996 na kwamba alikuwa na ujauzito Mei 1996.

Na Mahita katika ushahidi wake alidai kuwa mwaka 1995 alikuwa Moshi wakati Rehema anadai kipindi hicho alikutana na kufanya tendo la ndoa na Mahita mwaka 1996.

Pia Mahita alihamishwa mwaka 1996 kwa hiyo haikuwezekana kwenda kitandani na mrufani Mei 1996 Moshi wakati tayari alikuwa ameishateuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na alikuwa akiishi Dar es Salaam, na kwamba tayari mrufani alikuwa ameishapata uhamisho kutoka Moshi kwenda Arusha mwaka 1996.

Jaji Twaib alisema anakubaliana na kipisi cha ushahidi kilichotolewa na wakili Semgalawe unaoonyesha mrufaniwa alichanganya tarehe za yeye kupata ujauzito na kumzaa Juma lakini mrufani wakati akitoa ushahidi wake katika mahakama ya chini alieleza kuwa alivyoteuliwa kuwa IGP aliandaa ‘Maulid’ na mrufaniwa na mwanae walihudhuria na hakuwafukuza kwa sababu mkewe hakuwaona.

“Kama ni kweli Mahita aliteuliwa kuwa IGP mwaka 1996, sioni sababu ya kutofautiana na hilo na kwa mujibu wa mrufani alieleza aliaandza Maulid na alikwenda Arusha na mwanaye Juma siku hiyo na kwamba mtoto wao huyo alizaliwa kipindi hicho hicho cha mwaka 1996 …kwa kuwa mrufani alijichanganya kutaja tarehe hizo na alidai kupata ujauzito wakati akifanya kazi nyumbani kwa Mahita ….kwa mantiki hiyo nakubaliana na wakili wa mrufani kuwa mrufaniwa alijichanganya kutaja tarehe hizo na mahakama hii inatupilia mbali sababu hiyo ya pili kwa sababu utata huo wa tarehe unatatulika.

“Kwa maelezo hayo ya sababu ya pili na ushahidi uliotolewa na barua ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mahakama hiyo ya chini na kwa mazingira hayo na vitendo vile vilivyokuwa vikifanywa na Mahita vya kushindwa kwenda ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali mara tano kupimwa DNA,
“Mahakama hii imefikia uamuzi wa kumuona Mahita alikataa kupimwa kipimo hicho licha ya kuwa hakusema wazi wazi kuwa hataki kupimwa kipimo hicho cha vinasaba….hivyo basi mahakama hii inaitupilia mbali sababu hii ya pili,” alisema Jaji Twaib.

Aidha alisema sababu ya tatu ilikuwa ikiiomba mahakama hiyo itengue hukumu ya mahakama ya chini iliyomtaka mrufani kila mwezi ampatie mrufaniwa sh 100,000 kwaajili ya matunzo ya mtoto kwasababu kiwango hicho cha fedha kinakwenda kinyume na Sheria ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa (Affiliation Act) , inayomtaka mzazi atoe shilingi 100 na kwamba hata baadaye sheria hiyo ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kiwango hicho cha sh 100 hakijaondolewa kwa hiyo sheria na mahakama ya chini ilijipangia kiasi hicho cha sh 100,000 kinyume cha sheria hiyo.

Jaji Twaib katika uamuzi wake wa sababu hiyo ya tatu, alisema anaitupilia mbali kwani ni kweli sheria hiyo inataka mzazi atoe fedha ya matunzo ya shilingi mia moja lakini kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kiasi hicho cha fedha hakiwezi kutumika kugharamia matunzo ya mtoto.

Katika hilo mahakama hiyo nayo ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya chini iliyomuamuru Mahita kupeleka sh laki moja kwa mzazi mwenzake kwa ajili ya matunzo ya mtoto.

Aidha jaji huyo alisema sababu ya nne, mrufani alikuwa anaomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa mahakama ya chini ukimtaka mrufani alimpe mrufaniwa fidia kuanzia mwaka 2003 na siku ambayo hukumu ilitolewa na mahakama hiyo ya chini kwani Mahakama haikurekodi kuwa mrufani alikuwa akimtunza mtoto muda wote na kwamba mrufaniwa alikuwa alikuwa akihudumiwa tangu mwaka 1997 ambapo mtoto huyo alizaliwa.

Wakili wa Mahita alidai Hakimu wa Mahakama hiyo alikosea alipomtaka mrufani alipe gharama za matunzo kuanzia mwaka 2003 ambapo mwanamke huyo alidai Mahita alisitisha matunzo na kumuitia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU) kumfukuza wakati alipokuwa akienda kufuata gharama za matunzo.

“Nimesoma hukumu hiyo na hakimu yule alitoa amri ya kumtaka mrufani alipe fidia kwa mrufaniwa tangu siku mtoto alipozaliwa hadi siku ya hukumu ilipotolewa mwaka 2003 ya sh 100,000, hivyo sababu hii ya nne ya mrufani kwamba hakimu alijichanganya kutoa amri hiyo haina msingi na hivyo mahakama hii leo inatamka kuwa rufaa iliyokuwa imefunguliwa mahakamani hapo na Mahita dhidi ya Rehema imetupiliwa mbali na ninamwamuru mrufani amlipe mrufaniwa gharama za uendeshaji kesi hii,” alisema jaji Twaib.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, dada huyo anayedai kuzaa na Mahita, Rehema, alisema amefurahishwa na uamuzi huo wa mahakama kwani umezingatia haki na kusema kwamba mwanaye Juma Omar Mahita hivi sasa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Hananasif Kinondoni jijini Dar es Salaam, na kwamba yeye binafsi kwa sasa ni mwalimu wa madrasa ya Taqwa baada ya kuachana na biashara ya kuuza karanga.

Mwaka 2009, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilitoa hukumu katika kesi ya madai iliyokuwa imefunguliwa na Rehema aliyewekewa mawakili wa (LHRC) dhidi ya Mahita akiomba mahakama hiyo itoe amri itakayomlazimisha Mahita kumtunza yeye na mtoto wake kwa sababu kiongozi huyo mstaafu aligoma kutoa fedha za kumtunza mtoto huyo anayedaiwa kuwa ni wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 25 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.