Header Ads

WABUNGE CCM WAIBURUZA SERIKALI YAO MAHAKAMANI


*WAFUNGUA KESI YA KIKATIBA KUZUIA ISIILIPE DOWANS

Na Happiness Katabazi

WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na raia wengine wanne wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Tanzania dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake wakiiomba serikali izuiwe kulipa fidia ya sh bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd.


Kwa mujibu wa hati ya madai, wabunge hao wanataka serikali izuiwe kuilipa Dowans kwa sababu serikali ikilipa tuzo hiyo itakuwa imekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hati hiyo ya madai ya kesi Na. 5 ya mwaka huu, inawataja wabunge waliofungua kesi hiyo kuwa ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe (CCM), George Simbachawene, Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes na Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki.

Wengine katika orodha ya waliofungua kesi hiyo ni raia wa kawaida, Hassan Ngoma, Senkoro Izoka, Salum Kambi na Salma Shomari Mohamed, ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki na Kampuni ya Uwakili ya Lukwaro.
Mbali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wadaiwa wengine ni Waziri wa Nishati na Madini na Shirika la Umeme (TANESCO).
Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, waombaji hao wanaeleza kuwa endapo malipo hayo yatafanywa kwa Dowans ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakuwa wamevunja Ibara ya 26(2),27(1),(2) ya Katiba ya nchi ambayo mahakama hiyo ina wajibu wa kulinda ibara hizo zisivunjwe.

Ibara ya 26(2) inasema: “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”
Ibara ya 27(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.”

Ibara ya 27(2) inasema: “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

“Sisi walalamikaji katika kesi hii tunao wajibu wa kulinda na kuhifadhi mali za umma wa Watanzania na wadaiwa wanao wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha sheria za nchi yetu hazivunjwi;
“Kulipa au kusudio la wadaiwa kutaka kuilipa Dowans Holdings SA (Costa Rica) na Dowans Tanzania Limited, vitakuwa vinavunja Ibara ya 27(1) na (2) ya Katiba ya nchi na tunaomba itolewe amri na mahakama hii ya kuwazuia wadaiwa katika kesi hii kuilipa Dowans tuzo waliyoshinda katika Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICC),” alidai Simbachawene.

Simbachawene anadai kuwa tuzo iliyotolewa na ICC kwa Dowans Novemba 30 mwaka 2010, inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi na inajaribu kufuja fedha za umma.

Alidai tuzo hiyo ipo kinyume cha sheria kwa madai kuwa inakinzana na maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kupitia mjadala juu ya ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba tata wa TANESCO na Richmond, liliwahi kuweka wazi kwamba mkataba huo ulikuwa ni batili.

Aidha, alidai kuwa tuzo hiyo Dowans ikilipwa itakuwa ni kwenda kinyume cha sera za nchi na kwamba haiwezi kutekelezwa na mahakama za Tanzania.

“Kwa sababu hizo hapo juu tunaomba mahakama hii itoe amri ya kuwazuia wadaiwa wasijaribu kulipa fidia hiyo kwa Kampuni ya Dowans kwa sababu tuzo hiyo ni batili kisheria, inakinzana na maazimio ya Bunge na haiwezi kusajiliwa na mahakama za hapa nchini na inakwenda kinyume cha sera za nchi na kitendo cha kuilipa fidia kampuni hiyo basi ni wazi serikali itakuwa imevunja Katiba ya nchi”, alidai Simbachawene.

Simbachawene na wenzake wanaeleza kuwa mdaiwa wa kwanza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ni mshauri wa sheria wa serikali na mdaiwa wa pili ni waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye ndiye mwenye jukumu la mdaiwa wa pili la masuala ya umeme.

Kwamba Juni 21 mwaka 2006 mdaiwa wa tatu (Tanesco) chini ya maelekezo ya mdaiwa wa pili (waziri) waliingia mkataba na Kampuni ya Richmond Develepment Company LLC ya Texas Marekani kwa makubaliano yaliyojulikana kama “Power Off Take Agreement” wa kusambaza umeme wa megawati 100.

Lakini Kampuni ya Richmond ilidanganya na haikuweza kuzalisha umeme huo kwa wakati na wakati wanaingia mkataba huo hakukuwa na mwanasheria wa Serikali ya Tanzania wala wa Marekani.

Hati hiyo ya madai inasema, kwa kitendo hicho mdaiwa wa pili ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini alikuwa amevunja kifungu cha 38,31(1)(a) na 31(1)(b) na 31(2) ,42(a) na 59(1) vya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Kwa maana hiyo utaratibu wote wa kuipatia tenda kampuni hiyo ulikuwa batili na ulikiuka vifungu hivyo vya sheria ya manunuzi ya umma.

Akiendelea kuchambua makubaliano yaliyoingiwa, alidai kuwa Kampuni ya Richmond ilipaswa kuanza kusambaza umeme ndani ya siku 150 kuanzia siku ambapo mkataba baina ya Tanesco na kampuni hiyo ulisainiwa, ambayo ni Juni 23 mwaka 2006 na muda wa kuanza kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ulikuwa ni Februari 2 mwaka 2007.

Walalamikaji hao walidai tangu hapo hadi Desemba mwaka 2006 Kampuni ya Richmond ilishindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano hayo hali iliyosababisha mdaiwa wa tatu (Tanesco) kuandika barua kwa mdaiwa wa pili (waziri) ya kumwomba avunje mkataba huo kwa sababu Richmond imeshindwa kutimiza makubaliano waliyokubaliana na kwamba uthibitisho wa barua hiyo wanao.

Pia walidai kuwa Spika wa Bunge aliyepita, Samuel Sitta, Novemba 2007 aliunda Kamati ya Bunge kuchunguza tuhuma kuhusu mkataba huo, ambapo kamati hiyo ilibaini kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango hicho cha umeme, na taratibu za upatikanaji wa tenda zilikiukwa, hivyo kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, mawaziri waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kujiuzulu nafasi zao za uwaziri.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania ambalo limepewa Na. 8/2011 iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR na Timothy Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.

Kesi hiyo ambayo imekwisha kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Emilian Mushi, itakuja tena kwa ajili ya kutajwa Julai 28, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 2 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.