Header Ads

KORTI KUU YATENGEUA MASHARTI YA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetengua masharti ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Agnes Mchome kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu, Simon Jengo na wenzake wawili ambao wanakabiliwa na kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, baada ya kubaini hakimu huyo hakufuata sheria husika kutoa masharti hayo.


Mbali na Jengo,washitakiwa wengine ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Fedha za Nje, Kisima Mkango na Mkurugenzi wa Huduma za Benki Kuu, Ally Bakari, ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando na Richard Rweyongeza.

Uamuzi huo ulitolewa jana asubuhi na Jaji Emilian Mushi ambaye alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba Hakimu Mfawidhi Mchome kwa kwa uzembe hakuisoma vizuri hati ya mashtaka kwasababu hati ya mashtaka inaonyesha idadi ya noti zilizochapishwa na wala haijata kiasi thamani ya fedha za noti hizo zilizochapwa na mwisho wake akajikuta Mei 7 mwaka huu, anatoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa kwa kufuata kifungu cha 148(5)(e) ambacho kinamtaka mshtakiwa atoe nusu ya kiasi anachotuhumiwa kuiba au kusababisha hasara badala ya kutoa masharti ya dhamana kwa kutumia kifungu sahihi cha 148(6)(a) na (b) cha sheria.

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama hii imebaini kwamba Hakimu Mchome aliisoma vibaya hati ya mashtaka na akajikuta anatumia kifungu kisichohusika kutoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa na kwa sababu mahakama hii kuanzia sasa inatengua masharti ya dhamana yaliyotolewa na mahakama hiyo ya chini, na hivyo basi mahakama kuu leo(jana) inatoa masharti mapya ya dhamana kama ifuatavyo:

Alisema ili washtakiwa wapate dhamana nilazima kila mmoja asaini bondi ya Sh milioni tano, awe na wadhamini wawili watakaosaini ya kiasi hicho cha fedha ambao wataakikiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wasitoke nje ya jiji bila kibali cha Kamanda wa Polisi Kanda maalum,wasalimishe hati zao za kusafiria na waripoti katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa mujibu wa tarehe iliyopangwa ili waweze kuendelea na kesi inayowakabili.

Baada ya kutoa masharti hayo ndugu na jamaa wa washtakiwa hao walionekana wenye furaha na hatimaye washtakiwa hao waliweza kutimiza masharti ya dhamana hivyo wakaruhusiwa kurejea majumbani wako.

Mei 7 mwaka huu,Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliwafutia kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 500 ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo Septemba 15 mwaka jana na muda wote huo walikuwa wakisota rumande kwakushindwa kutimiza masharti ya dhamana.Licha ya kuwafutia mashtaka wagurungezi hao walijikuta wakikamatwa tena baada ya kutuhumiwa mashtaka matatu ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Wakili Sedekia, alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa
hao wanakabiliwa na mashtaka matatu, ambapo kosa la kwanza walilifanya 2004, kwa kuchapisha noti zenye thamani ya sh milioni 500.
Wakili Sedekia, alidai shtaka la pili linafanana na la kwanza ambapo wanadaiwa kutumia nyaraka hizo kumdanganya mwajiri wao ili aweze kuongeza gharama za uchapishaji wa noti zenye thamani hiyo mwaka 2005.

Aidha, wakili alidai shtaka la tatu ni la kutumia madaraka yao vibaya, ambapo watuhumiwa hao kwa pamoja wakiwa na nafasi zao, waliongeza gharama za uchapishaji wa noti zenye thamani ya sh bilioni 1.4 mwaka 2007.

Wakati huo huo Jaji Mushi alitoa masharti ya dhamana kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Michael Wage Karoli na maofisa wenzake tisa ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara halmashauri hiyo ya Sh 850,108,137 na kusema kuwa Juni 11 mwaka huu, atatoa uamuzi kuhusu ombi hilo.

Mbali na Karoli washtakiwa wengine ni Godwin Mwambashi ambaye Mhasibu, Suleiman Kitenge ambaye ni ofisa Afya
,Felix Ngomano ambaye ni Mhandisi,Cheka Omari ,Aloyce Gabrile ambaye ni Ofisa Mipango, Alex Mwakawago ambaye Ofisa elimu ,Rhoda Nsemwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Abdul Mwinyi ambaye ni Mhasibu wa Ndani.Washtawakiwa wote ni watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na wanatetewa na mawakili wa Edgi Mkoba,Ruthi Chiloma ,Asha Nassoro na Juma Nyamugaruri.

Jaji Mushi alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi,Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa masharti ya dhamana washtakiwa wanaokabiliwa na makosa ambayo yanazidi sh milioni 10 na kuongeza kuwa mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kutoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao kama ifuatavyo:

Jaji Mushi alisema ili wapate dhamana ni lazima kila mshtakiwa atoe fedha taslimu sh milioni 47,228,299.80, hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha, wadhamini wawili wanaoaminika, wasalimishe hati ya kusafiri kwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, na kila Jumatatu kila mshtakiwa atapaswa kuwa anaripoti kwa mkuu huyo wa polisi wa wilaya hiyo.

Hata hivyo gazeti hili wakati linaondoka mahakamani hapo bado washtakiwa wote walikuwa hawajatimiza masharti ya dhamana.

Mei 5 mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo wakikabiliwa na mashtaka mawili.Shataka la kwanza ni la kula njama ambalo linawakabili washtakiwa wote.Wakati shtaka la pili,pia linawakabili washtakiwa wote pia kwamba katika mwaka wa fedha Julai 2009 –Februali 28 mwaka 2010 katika muda tofauti huku Bagamoyo mkoani Pwani ,wakiwa waajiriwa wa halmashauri ya wilaya hiyo waliiba Sh 850,108,137.

Jamhuri ilidai shtaka jingine ambalo ni shtaka mbadala wa shtaka la pili , ni shtaka la kusababisha hasara kinyumbe na kifungu cha 10(1) na (2)(a) na (b) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002. Kwamba washtakiwa wote kwa pamoja wakiwa watumishi ,walisababisha halmashauri hiyo ya wilaya ya Bagamoyo ipate hasara hiyo..Na toka kipindi chote hicho hadi leo washtakiwa wanaendelea kusota rumande.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 12 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.