Header Ads

RUFAA YA KASUSURA YAGONGA MWAMBA




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na aliyekuwa dereva wa kampuni ya Ulinzi ya Knight Support, Justine Kasusura kwa maelezo kwamba sababu sita alizozitumia kukata rufaa zimeshindwa kuthibitisha kwamba Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomtia hatiani kwa makosa unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi dola milioni mbili za Marekani mali ya Citibank ilikuwa na dosari za kisheria.


Hukumu ya Rufaa hiyo ilitolewa jana na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye alisema baada ya kupitia kwa kina hukumu iliyotolewa Aprili mosi mwaka 2007 na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Sivangilwa Mwangesi ilikidhi matakwa ya kisheria na ilikuwa sahihi kuwaachiria huru washtakiwa wengine waliokuwa wakishtakiwa na mshtakiwa huyo.

Mwangesi alimtia hati Kasusura kwa makosa hayo mawili, kosa unyanganyi wa kutumia silaha ambalo ni kinyume na kifungu cha 285 na 286 alimhukumu kwenda jela miaka tano na viboko 12 na kosa la wizi ambalo ni mbadala wa shataka la unyanganyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 265 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, alimhukumu kwenda jela miaka 30.

“Baada ya kupitia kwa kina hukumu ya mahakama ya chini na sababu sita za kukata rufaa zilizowasilishwa hapa na mrufani, mahakama inatupilia mbali rufaa ya mrufani na badala yake inakubalina na hoja za upande wa Jamhuri zilizodai kuwa hukumu ya Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi kumhukumu adhabu hiyo,” alisema.

Aidha, alisema kisheria tangu awali mrufani alipowasilisha rufaa yake ,mahakama ilipaswa iifute rufaa hiyo kwa sababu ilikuwa imekiuka sheria, lakini ili kusahihisha adhabu iliyotolewa na mahakama ya chini ndiyo maana haikuifuta rufaa hiyo kwa sababu hakimu Mwangesi alikosea kibinadamu alipomtia hatiani katika kosa la unyang’anyi wa kutumia na kuamuru aende jela miaka mitano.

Jaji Mihayo alisahihisha adhabu huyo na kusema kuwa katika kosa la kwanza atatumikia ambalo ni la unyang’anyi wa kutumia silaha mrufani atumikia miaka 30 jela na viboko 12 na kosa la wizi atatumikia miaka mitano na kwamba adhabu hizo ataitumikia kwa pamoja.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Juni 24 mwaka 2010

1 comment:

Anonymous said...

Ameshapata fundisho. Na kama hii ndio style basi hata mafisadi washtakiwe.

Powered by Blogger.