Header Ads

SOPHIA SIMBA UMEGEUKA KUNGWI?



Na Happiness Katabazi
RAIS Jakaya Kikwete wakati akipanga safu yake ya uongozi muda mfupi tu tangu alipoapishwa, hakuficha dhamira yake kwa kutamka bayana kwamba katika uongozi wake atahakikisha anawateua wanawake wenye sifa za uongozi.

Nadiriki kukiri bila kumng’unya maneno kwamba rais amejitahidi kuitekeleza kwa vitendo dhamira hiyo.

Nasema hivyo kwa sababu tumeshuhudia wanawake wengi ukilinganisha na awamu zilizopita, ambao wameweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Ni nia njema ya rais wetu kutaka kutuinua sisi wanawake ili tuweze kushiriki kwenye ngazi za uamuzi, lakini ili wananchi waendelee kuamini anachoamini rais kwamba wanawake wanaweza kama walivyo wanaume, ndiyo maana ameamua kuwabeba kwa mbeleko.

Lakini Juni 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (CCM) Taifa, Sophia Simba, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), aliwataka wanawake wa jumuiya hiyo wanaoishi na wanaume ambao si wanachama wa CCM kuwanyima waume wao unyumba kwa lengo la kuwakomesha.

“Ninyi wanawake wenzangu ambao waume zenu wapo katika vyama pinzani na mnajua wazi kuwa hawawapi ushirikiano wowote katika siasa ya CCM wanyimeni ‘nonino’, muone kama hawatarejea katika chama tawala, nonino nikiwa na maana ya tendo la ndoa,” alisema Sophia huku akishangiliwa na wanawake wote kuonyesha kuwa alilolisema limewagusa.

Agizo la Waziri Simba kwa wanawake wa CCM, ni wazi kabisa limetia doa jitihada za rais za kuwapa madaraka wanawake, kwani si siri, baadhi ya wananchi wamekuwa wakihoji uwezo wa kiutendaji wa kiongozi huyo.

Wananchi wameibuka na maswali kutokana na waziri huyo mara kadhaa kunukuliwa na vyombo vya habari akitoa matamko ambayo hayarandani na nyadhifa alizonazo.

Hakuna ubishi kwamba taifa hili limo kwenye vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi, pia ongezeko la watoto wa mitaani, lakini cha kushangaza, waziri halioni hilo hadi anaamua kutoa agizo la wanawake wa CCM kuwanyima unyumba waume wao ambao ni wanachama wa vyama vya upinzani.

Kwa mtazamo wangu, binadamu aliyekamilika na ambaye yumo ndani ya ndoa, kuna wakati huhitaji unyumba, sasa kama mwanadamu huyo ambaye ni mume wa mwanamke wa CCM, asipopewa haki yake ya ndoa, eti kwa sababu waziri amewaambia wake zao wawanyime unyumba, ni wazi wanaume wengi wataamua kutafuta njia mbadala, ili kuwapata wanawake wengine pembeni.

Nao wanawake watakapohitaji tendo la ndoa, je waende wapi?Au tayari ameishawatafutia wanaume wengine ambao watawatimizia hamu hiyo?

Kama tunavyojua, ukimwi umetamalaki, mwanamume huyo anapokwenda kutafuta mwanamke mwingine, tuna uhakika gani kuwa mwanamke huyo mpya hajaambukizwa maradhi ya ukimwi?

Si kuambukizwa ukimwi tu, je, ikitokea mwanamume aliyenyimwa unyumba na mkewe akahamia nyumba ndogo, si ni wazi anaweza kutelekeza familia yake na wakati mwingine kusahau au kupunguza kupeleka matunzo kwa familia yake ya awali?
Hivi watakaopata shida si watoto ambao hawana hatia na mwanamke aliyerubuniwa na agizo la Simba?

Hivi huyu Simba alivyotoa agizo la kipuuzi kama hili huku akijua yeye ni Waziri ambaye wizara yake inaziongoza idara nyeti kama Idara ya Usalama wa Taifa,hivi anataka watumishi wa idara hiyo wananchi kwa ujumla wamueleweje?Je waendelee kumheshimu kama Waziri wao au sasa waanze kuamini waziri wao amejigeuza na kuwa Somo au Kungwi? Hatukuelewi.

Na yote hayo yakishatokea mwisho wa siku huyo mwanamke aliyetekeleza agizo la Simba, si atakuwa wa kwanza kulalamika kwamba mumewe kamtelekeza na kukimbilia mahakamani kudai haki na mwisho wa siku watoto watakosa ada za shule na wengine kujikuta wakijiingiza kwenye vitendo haramu vya uvutaji bangi, ukahaba na ombaomba mitaani?

Wakati umefika kwa viongozi wanawake wote mliopewa madaraka kama rais wetu alivyoahidi kuwainua wanawake, mchunge kauli zenu na nyendo zenu, muwajibike kwa masilahi ya taifa ili hata wale wote waliokuwa wakiibeza dhamira hiyo ya rais wakose la kusema.

Namshauri Waziri Simba achague maneno ya kuongea mbele ya umma, kwani kwa agizo hilo endapo litatekelezwa ni wazi litavunja ustawi wa jamii yetu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Juni 24 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.