Header Ads

VITA YA LUKUVI MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

OFISA Ardhi wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, Magesa Magesa(33) jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka moja la kughushi dondoo ya barua inayoonyesha imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Noel Mkomola Mahyenga.


Kufikishwa kwa mshtakiwa huyo mahakamani jana kunafuatia amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi aliyoitoa wiki iliyopita ambapo alizifunga ofisi za Ardhi katika Manispaa ya Kinondoni baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba baadhi ya maofisa ardhi wamekuwa wakijiusisha na vitendo vya ufisadi katika suala zima la utoaji hati za kumiliki ardhi kwa wananchi.

Katika kesi hiyo iliyofika kwa mara ya kwanza jana mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Betha Misonge mbele ya Hakimu Mkazi Gabrile Milumbe alidai kuwa Magesa ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Godwin Mussa na Majura Magafu alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo la kughushi kinyume na kifungu cha 333,335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Misonge alidai kuwa tarehe na muda usiyojulikana mwaka 2009 , mshtakiwa huyo alidanganya na kisha akagushi dondoo ya barua yenye kumbukumbu Na.TBW/ADM/IN/250/2009 ya Juni 8 mwaka jana,inayotoka Tanzania Building Works Ltd kwa lengo la kuonyesha kwamba Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Kinondoni, Mahyenga alitoa kibali kumilikishwa ardhi katika kitalu Na.1274/1275 kilichopo Msasani Penisula kwa Tanzania Building Works Ltd huku akijua nondoo za barua hiyo ni za kughushi.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na wakili wa serikali Misonge alidai hawana pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa na hakimu mkazi Mirumbe alisema ili mshtakiwa apate dhamana ni lazima atoe mahakamani sh milioni 10 au wadhamini wawili mmoja ambaye atatoa hati ya mali yenye thamani hiyo.

Hata hivyo Hakimu Mirumbe alisema utekelezwaji wa masharti hayo ya dhamana utafanyika kesho(leo) hivyo akaamuru mshtakiwa apelekwe rumande na arudishwe leo kwaajili ya kuja kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 22 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.