Header Ads

TANZANIA INA MAWAKILI 1,322-JAJI JUNDU

Na Happiness Katabazi

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini, Fakhi Jundu amesema hadi kufikia jana taifa lina jumla ya mawakili wa kujitegemea 1322 idadi ambayo alisema ni ndogo ukilinganisha na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Jaji Jundu aliyasema katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana ofisini kwake ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Jaji Mkuu Agustino Ramadhani kufunga sherehe za kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya 128 toka 1194 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kuudhuliwa na watu mbalimbali akiwemo mke wa rais,Salma Kikwete.

Alisema mahitaji ya uhuduma ya mawakili inazidi kuongeza lakini idadi ya mawakili wa kujitegemea hapa nchini bado haikidhi mahitaji ukilinganisha na nchi kama ya Kenya ambayo ina zaidi ya mawakili 3000.

“Nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na huko tuendako milango itafunguliwa ambapo mawakili toka nchi hizo watakuwa wakiruhusiwa kwenda kutoa huduma za kisheria katika mahakama za nchi jirani,hivyo idadi ya mawakili wa kujitegemea isipoongezeka nchini ni wazi tutashindwa kufurukuta;

“Hivyo sisi kama mhimili wa mahakama nchini tumejipanga kuakikisha tunaendelea kuapisha mawakili wengi zaidi ili taifa liwe na mawakili wengi ambao wataenda kutoa huduma hiyo kwa wananchi lakini pia ni washauri mawakili hawa wa kujitegemea ofisi zao za kisheria wanazozifungua waakikishe inakuwa na mawakili wengi ili wakili mmoja akiumwa, akipa udhuru au akienda mahakama nyingine kusikiliza kesi ya mteja mwingine basi wawepo mawakili toka kwenye ofisi hiyo ambaye ataweza kuendelea kutoa huduma kwa wateja” alisema Jaji Kiongozi Jundu.

Jaji Jundu alisema idadi hiyo ya mawakili wapya 128 imegawanyika katika mafungu mawili, kundi la kwanza ni waombaji 53 waliohitimu shahada ya sheria na baadaye kuhitimu katika chuo cha Wanasheria kwa Vitendo na kuongeza kuwa kundi hilo ni la kihistoria kwa vile hii ni mara ya kwanza kwa wanasheria wanaohitimu kutoka chuo hicho kukubaliwa kuwa mawakili kwa mujibu wa kifungu cha 12(3) cha Sheria ya chuo hicho ya mwaka 2007.Kundi la pili lina waaombaji 75 ambao walipitia usaili wa Baraza la Elimu ya Sheria.

Alisema hapa nchini mawakili wa kujitegemea wengi ofisi zao zina mawakili wasiozidi watatu au wakili mmoja hali inayosababisha baadhi ya wateja kusita kuwapatia kazi za kuwawakilisha mahakamani kwa hofu kuwa inaweza ikatokea wakili huyo akapata udhuru na hivyo akashindwa kumwakilisha mahakamani au kumpatia msaada wowote wa kisheria kwa muda mwafaka na kuongeza tayari mawakili wa nchi jirani wameishaondokana na kasumba hiyo na sasa ofisi moja ya mawakili inakuwa na zaidi ya mawakili kumi.

Hata hivyo aliwashauri waombaji li waomba usajili wa mawakili ambao bado majina yao hayajapitishwa kuwa mawakili,wawasiliane na Baraza la Elimu la Sheria ambalo yeye ni Mwenyekiti wake ili waweze kujua ni tarehe gani wamepangiwa kuja kufanya usahili nakuongeza wamefanya mabadiliko na kwamba kila wiki sasa wamekuwa wakiwahoji waombaji 20 hapa jijini Dar es Salaam, na siyo Arusha peke yake kama ilivyozoeleka hapo zamani.

Naye mtoto wa rais, Ridhiwan Kikwete ambaye alikuwa miongoni mwa mawakili wapya waliopewa usajili aliwaambia waandishi wa habari kwamba anafuraha kupata usajili huo na kwamba ndoto yake ya siku nyingi ya kuwa wakili imetimia na kuahidi kwamba katika taaluma yake ya sheria anachozingatia ni kutenda haki na sivinginevyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni 25 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.