Header Ads

HAKIMU AGNES MCHOME ACHA UZEMBE

Na Happiness Katabazi

IJUMAA ya wiki hii Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam , ilibadilisha masharti ya dhamana yaliyokuwa na Mahakama ya wilaya ya Ilala katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu, Simon Jengo na wenzake wawili.


Mbali na Jengo,washitakiwa wengine ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Fedha za Nje, Kisima Mkango na Mkurugenzi wa Huduma za Benki Kuu, Ally Bakari, ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea maarufu nchini,Richard Rweyongeza na Mabere Marando.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Emilian Mushi ,ambaye bila kumung’unya maneno alisema amefikia uamuzi wa kubadilisha masharti hayo ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Mfawadhi Agnes Mchome,na kuweka masharti mapya ya dhamana, ni baada yakubaini hakimu huyo alikosea kisheria kutumia kifungu cha 148 (5)(e) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 katika shauri hilo.

“Hakimu Mchome hakuwa makini,alizembea kiasi cha kushindwa kung’amua kwamba hati ya mashtaka haikutaja thamani ya idadi ya noti zilizochapishwa….hivyo kwa uzembe huo hakimu huyo akajikuta anatumia kifungu hicho ambacho hakipaswi kutumika katika kesi hii kutoa dhamana…kwa hiyo mahakama hii inatoa masharti mapya ya dhamana kama ifuatavyo”alisema Jaji Mushi.

Kila mshtakiwa atapaswa kusaini bondi ya Sh milioni tano, awe na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali ambao watakaguliwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam,kusalimisha hati ya kusafiria,hawataruhusiwa kutoka nje ya jiji bila kibali cha Kamanda wa polisi kanda maalum ya dar es Salaam,kwenda kuripoti Mahakama ya Ilala ilikujua kesi yao ya msingi imepangwa tarehe gani.Washtakiwa wote juzi walimiza masharti hayo ya dhamana wakaruhusiwa kurejea uraiani kuungana na familia zao baada ya kusota rumande kwa miezi kumi sasa.

Itakumbukwa kwamba hakimu Mchome alitoa masharti hayo ya dhamana Mei 7 mwaka huu, ikiwa ni dakika chache tu baada ya mahakama hiyo kuwafutia kesi ya awali ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 500 bada ya mahakama hiyo kupokea hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),Elizer Feleshi ambayo aliliwasilisha chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Makosa ya jinai, ambayo ilisema DPP hana haja kuendelea na kesi hiyo ambayo ilisababisha washtakiwa hao kusota rumande kwa miezi tisa baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kila mmoja kutoa fedha au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh bilioni 14.Kesi hiyo iliyofutwa ilifunguliwa rasmi mahakamani hapo Septemba 15 mwaka jana.

Licha ya siku hiyo ya Mei 7 mwaka huu, kufutiwa kesi hiyo na mahakama, washtakiwa hao walijikuta dakika chache baadaye wakikamatwa tena na kufunguliwa kesi Na.359 ya mwaka huu, na wakili wa serikali Ephrey Sedekia mbele ya hakimu Mchome, lidai kuwa washtakiwa katika kesi hiyo mpya wanakabiliwa na mashtaka matatu.

Wakili wa Sedekia alieleza kuwa kosa la kwanza,walilifanya 2004, kwa kuchapisha noti zenye idadi ya 500,000,000. Wakili Sedekia, alidai shtaka la pili linafanana na la kwanza ambapo wanadaiwa kutumia nyaraka hizo kumdanganya mwajiri wao ili aweze kuongeza idadi ya kuchapisha noti yenye idadi hiyo mwaka 2005.

Aidha, wakili alidai shtaka la tatu ni la kutumia madaraka yao vibaya, ambapo watuhumiwa hao kwa pamoja wakiwa na nafasi zao,waliongeza idadi ya uchapishaji noti na kufikia 1,400,000,000 mwaka 2004.

Masharti hayo ya dhamana yaliyowataka washtakiwa watoenusu ya thamani ya fedha zilizotajwa kwenye hati ya mashtaka wakati hati ya hiyo ya mashtaka haikutaja thamani ya fedha isipokuwa ilitaja idadi ya hizo za noti zilizochapwa, yaliyotolewa siku hiyo na hakimu Mchome na hivyo kusababisha washtakiwa kuendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo hadi juzi asubuhi walipofikishwa mahakama kuu na mchana kufanikiwa kupata dhamana baada ya kutimiza masharti mapya yaliyotolewa na mahakama hiyo ya juu.

Chini ya kifungu cha 148(5)(e)cha Sheria ya makosa ya Jinai,mahakama ina mamlaka kumuamuru mshtakiwa anayes kwa kosa linalohusu fedha inayozidi sh milioni 10 ,mshtakiwa atatakiwa atoe nusu ya kiasi anachotuhumiwa kuiba au kusababisha hasara ndiyo apate dhamana.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwenye kesi hii inayowakabili walshtakiwa hao iliyofunguliwa katika mahakama ya wilaya ya Ilala.Washtakiwa hao hawakulidhika na masharti ya dhamana ya mahakama hiyo ya chini na wakaamua kuwasilisha ombi na.24 ya mwaka huu, Mahakama Kuu, ili mahakama hiyo ya juu iweze kubadilisha masharti ya dhamana kwakuwa yamekosewakupita kiasi na yanawauiza kwa kuwanyima uhuru.

Juni 4 mwaka huu, washtakiwa hao kupitia mawakili walimweleza Jaji Mushi kupita hati ya kiapo kilichoapwa na wakili Mabere Marando kwamba mashtka hayo matatu yanayowakabili wateja wake,yanadai walichapisha idadi ya noti 1,400,000,000.Na kwamba idadi hiyo ya noti haikutajwa kwa thamani yake.

Ombi la utetezi liliungwa mkono na Wakili mwandamizi wa serikali Timon Vitalis aliyekuwa akisaidiwana Ephrey Sedekia.Hatua hiyo ya mawakili hawa wa serikali imeonyesha ni waadilifu na weledi wa taaluma ya sheria ,kwani kwa vinywa vyao walikiri kwamba hati ya mashtaka imetaja idadi ya noti zilizochapishwa na wala haikutaja thamani ya noti hizo jambo ambalo linafaya matumuzi ya kifungu cha 148(5) (e) cha sheria ya makosa ya jinai,katika kesi hii ni batili.

Ili kutoa haki na kupunguza mlolongo wa urasimu,uamuzi huu wa jaji Mushi , unazua hoja kwenye safu hii ya Fukuto la Jamii ambayo imekuwa mstari wa mbele kuatilia kesi mbalimbali ikiwemo kesi hii tangu ifunguliwe hadi juzi yalipotolewa masharti mapya, kwamba baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola waliokabidhiwa mamlaka ya kutoa haki bila upendeleo wala husuda, hawafanyi hivyo.Sababu zinaweza kuwa nyingi rushwa,uzembe,ukosefu wa umakini,uoga au udhaifu katika taaluma ya sheria.

Vyovyote iwavyo sababu zote hizo zinajenga hisia hasi kwa jamii dhidi ya mhimili wa mahakama na na serikali kwa ujumla.Tunachoweza kusema iweje waajiriwe watu wanaoweza kuchukua maamuzi kama haya ya hakimu Mchome ambayo yamesababisha washtakiwa ambao wanategemewana familia zao kusota rumande?

Je thamani ya uhuru wa watu iko wapi? Tunachoweza kusema ni kwamba wakati umefika sasa kutupia macho aina ya watendajiwa mhimili wa mahakama tulionao.

Wale wenye taaluma dhaifu ama waondolewe na wasipewe fursa ya kuhujumu haki za watu jambo ambalo linaiaibisha mhimili wa mahakama na kuidhalilisha taaluma ya sheria.

Sheria ilipoweka vifungu vinavyoruhusu rufaa,mapitio, marejeo,masahiisho,haina maana kwamba sheria hiyo inaruhusu baadhi ya mahakimu na majaji kuwa wazembe,kutokuwa makini na kwa ujumla kuna hujumu haki.

Lengo la vifungu kama hivyo ni kurekebisha makosa ya kiufundi na ya kibinadamu lakini uamuzi wa mshartiya dhamana yaliyotolewa na hakimu huyo ,umeonekana kuwa ni wa kizembe na wala hauna jinsi ya kuelezea wala kuutetea.

Wakati umefika sasa baadhi ya sheria za nchi zibadilishwe ili kutoa fursa kwa wananchi wenzetu wanaokosewa haki na mahakama zetu kuweza kupata fidia na mahakimu na majaji wanaowakasesha haki wananchi hao wawajibike.

Haki na uhuru wa mahakama uliotamkwa na ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,usitafsiliwe kwa maana hasi ya kuweka kinga ya baadhi ya mahakimu na majaji wasiyo makini.

Fukuto la Jamii,linawaasa majaji na mahakimu kuwa na taadhari kwa wananchi wenzetu wanaoletwa mbele zenu ni watuhumiwa tu siyo wahalifu na wakati huo tambueni wengine ni raia wema na wenye familia zinazowategemea wakati ukweli ni kwamba wamebambikiziwa kesi kwasababu ya chuki binafsi,umbeya na hata visasi vya kisiasa na kibiashara na kunyang’anya wanawake.

Matatizo kama hayo ya kubambikiziana kesi ni matokeo ya mfumo hai wa utendaji wa vyombo vya dola ambayo yanaweza kumkuta mtu yoyote.

Tunafahamu fika kwamba wapo baadhi ya mahakimu wanaokubali kirahisi kulogwa kizungu ‘kupokea rushwa’ ili wapindishe haki za watu,wapo pia mahakimu waoga kufikia maamuzi yanayojali misingi ya haki badaya yake wanatoa hukumu za kuwakandamizi makusudi wananchi wasiyo na hatia kwa vile tu mahakimu hao wamepokea maelekezo ya kupindika haki toka kwa baadhi ya viongozi serikalini na wanasiasa.

Na baadhi ya mahakimu hao bila haya wakati wanatoa hukumu hizo utawasikia wakisema wamefikia hatua za kumuona mshtakiwa fulani ana hati kwasababu eti Taifa hivi sasa lipo kwenye vita dhidi wa badhilifu wa fedha za umma ingali mashtaka aliyoshtakiwa nayo mshtakiwa hayausiani kabisa na wizi wala ubadhilifu.

Mahakimu wengine wanatumia kinga ya uhuru wa mahakama kutoa hukumu zinazowakandamiza baadhi ya washtakiwa idi mradi tu hakimu huyo amenyimwa rushwa na mshtakiwa, au hakimu huyo ameaidiwa na viongozi wenye hulka za kinyang’au serikalini kumfunga mshtakiwa fulani bila hata ushahidi wa kutosha wa kumtia mtu hatiani na mwisho wa siku tunashuhudia maisha ya baadhi ya mahakimu wa aina hiyo maisha yao uanza kuwanyokea.

Na haya mambo yapo wananchi tunayashuhudia katika baadhi ya maamuzi ya kesi mbalimbali na pia kuambiwa kwa siri na baadhi ya mahakimu wanaofuata maadili ya kazi yao na matapeli wanaokaa nje ya mahakama zetu hususani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama ya Wilaya ya Ilala, ambao watu hao ambao wanadaiwa kuwa mabingwa wa kuwasaidia washtakiwa kupata hati wanazozitumia ili wapate dhamana mahakamani na watu.

Kwanza nikiri kwamba ‘wajanja’ambao kutwa wanashinda mahakamani wanamtandao mpana sana unaowawezesha kupenya kilaini kwa baadhi ya mahakimu na mawakili wa serikali ‘watoto wa Eliezer Feleshi ‘ wenye hulka za kifisadi ambao wanasikiliza kesi za washtakiwa wa wanaowatuhumiwa watu hao,kucheza mchezo mchafu wa kutumia taaluma yao ya kisheria kupendekeza kwa viongozi hao watoe kibali cha kuzifuta kesi za washtakiwa wa aina hiyo na kweli ufisadi wao unafanikiwa.Hilo ndilo Fukuto la Jamii kwa leo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.mwisho

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Juni 13 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.