Header Ads

UONEVU WAMKERA JAJI MKUU

Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, amesema tatizo la kusuasua kwa uendeshaji wa kesi za jinai ambalo linahusisha mhimili wa mahakama na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hayaleti picha nzuri katika Wizara ya Katiba na Sheria.


Jaji Ramadhani, aliyasema hayo kupitia hotuba yake ya kumkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, wakati akifungua kikao cha Majaji wa Mahakama za Rufaa, Mahakama Kuu Tanzania Bara na Zanzibar kilichofanyika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha hivi karibuni na Tanzania Daima kupata nakala ya hotuba yake.

Alisema matatizo ya ofisi hiyo, yamesababisha lawama nzito kwa mhimili wa mahakama, kitendo ambacho hakipaswa kuanikwa hadharani ama kupitia vyombo vya habari.

Akitoa mfano, Jaji Ramadhan alisema anakumbuka vyema jinsi hali ya kutoelewana iliyowahi kutokea kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hosea, kuhusu kesi za Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), wakati zikiwe kwenye mchakato wa kupelekwa mahakamani.

“Lakini siyo tu kwa mahakama, haki za binadamu zinasiginwa na mhimili wa mahakama unafanywa mbuzi wa kafara,” alisema Jaji Ramadhan.

Akitoa mfano wa raia 36 waliokamatwa wakivua samaki katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ambao wamepachikwa jina la “Samaki wa Magufuli”, alisema walistahili kufunguliwa mashtaka Mahakama Kuu na kwamba ushauri ulitolewa juu ya jambo hilo na mtaalam wa sheria za Maritime, Kapteni Ibrahim Bendera ulipuuzwa.

“Suala hili, lilipofunguliwa rasmi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 23, 2009 hadi lilivyohamishiwa Mahakama Kuu mwaka huu, muda umepotea bure kwa ukaidi,” alisema Jaji Ramadhan.

“…Mwaka mzima washtakiwa wako rumande, wananyimwa dhamana mpaka mshtakiwa mmoja raia wa Kenya alifia gerezani hivi karibuni. Balozi wa China hapa nchini, alikuja kuniona juu ya wananchi wake kuwekwa ndani kipindi chote hiki, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba chombo chetu hakiioni hali hii,” alisema Jaji Ramadhan.

Alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, kodi za Watanzania, zimetumiwa kuwalisha raia hao wa kigeni na kusema kuwa hiyo siyo haki kwa wananchi.

“Hivi haitoshi kumshtaki nahodha wa meli, ambayo imekamatwa na kuwaachia hao watu wengine waende zao? Nimeongea na DPP –Feleshi- na kuumuliza kama hawezi kuwafutia mashtaka hao wengine. Kubwa nililolipata ni kuwa anayemiliki meli hajulikani, lakini nahodha kashikwa tatizo liko wapi?” aliuliza Jaji Ramadhan.

Alitoa mfano wa pili kuwa ni iliyokuwa kesi na.9/2009 iliyofunguliwa Mahakama ya Wilaya Septemba 15, 2009 dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu (BoT), Simon Jengo, Naibu Mkurugenzi wa Fedha za Nje, Kisima Mkango, na Mkurugenzi wa Huduma za Benki Kuu, Ally Bakari, na Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Huduma ya Sheria, Bosco Kimela, wanaotetewa na mawakili Mabere Marando na Richard Rweyongeza.

Alisema hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilitiwa saini Februari, 2009 na miezi nane yaani Septemba 15 mwaka huo, ndipo watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema kila kesi inapotajwa katika mahakama ya Wilaya ya Ilala wimbo umekuwa ni ule ule wa upelelezi bado.

“Suala muhimu ni kwa nini mashtaka yaliandikwa Februari, halafu washtakiwa hao wakakamatwa na kufikishwa mahakamani Septemba na upelelezi uwe bado haujakamilika?” alihoji Jaji Mkuu.

Alisema ilipofika Mei 7 mwaka huu, kesi hiyo ilifutwa na mahakama baada ya kupokea hati ya DPP iliyoiarifu mahakama hiyo iifute kesi hiyo kwa sababu DPP hana nia ya kuendelea na kesi na baada ya muda mfupi DPP akawafungulia washtakiwa kesi nyingine Na.359/2010 dhidi ya watuhumiwa watatu na wakawa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

“Mheshiiwa Waziri Chikawe, huku ni kutumia vibaya madaraka ya kukamata na kufungua mashtaka ambayo yatamnyima mtuhumiwa haki ya dhamana. Je, huku si kukomoana?” aliuliza Jaji Ramadhan.

“Tukumbuke tuwatendee wenzetu kama vile tunavyotaka nasi tutatendewe, sidhani kama kuna yeyote humu ndani au ofisi ya DPP ambao wangependa wenyewe au jamaa zao kurundikwa rumande namna hii, kuna kila sababu ya kuondokana na hali hii,” alisisitiza Jaji Ramadhani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu,Juni 7 mwaka 2010

2 comments:

Anonymous said...

naona jaji mkuu sasa ana hamu na ofisi ya DPP!
Ni kwamba Mahakamani hakuna matatizo, ama muandishi amependa matatizo ya ofisi ya DPP tu? Haki embu tuambie DPP ana lipi la kujitetea na happiness atoe makala nyingien kujibu hili? Saa ya ukombozi ishafika, wakichomana Mtukufu raisi atajua nini cha kufanya.

Anonymous said...

naona jaji mkuu sasa ana hamu na ofisi ya DPP!
Ni kwamba Mahakamani hakuna matatizo, ama muandishi amependa matatizo ya ofisi ya DPP tu? Haki embu tuambie DPP ana lipi la kujitetea na happiness atoe makala nyingien kujibu hili? Saa ya ukombozi ishafika, wakichomana Mtukufu raisi atajua nini cha kufanya.

Powered by Blogger.