Header Ads

UN KUENDELEA KUGHARAMIA MAFUNZO KWA WANAHABARI

Na Happiness Katabazi, Zanzibar

UMOJA wa Mataifa (UN) nchini Tanzania umesema utaendelea kutoa fedha za kugharamia mafunzo ya habari za uchunguzi kwa waandishi wa habari wa Tanzania Bara na Visiwani, kwani wanaamini habari zikifanywa kikamilifu zitaendelea kuleta maendeleo nchini.


Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa - Tanzania, Usiah Nkhoma Ledama, alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View wakati akifunga mafunzo ya wiki moja ya waandishi wa habari yaliyofadhiliwa na UN-Tanzania, Unesco na kuratibiwa na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC).

Alisema lengo la kufadhili mafunzo hayo ni kwamba wanaamini vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuleta maendeleo katika taifa lolote duniani, hivyo akawaasa wahitimu hao kwenda kutumia vema elimu hiyo, ili waweze kuleta maendeleo kwa taifa.

“Sisi kama UN nia ya kukuza taaluma ya habari tunayo na ndiyo maana mafunzo haya ni ya pili kufanyika hapa nchini na tutaendelea kutoa mafunzo kama haya hapa nchini na tutagharamia haya mafunzo ili vyombo vya habari viwe vinaandika mazuri ya UN, hivyo tunaomba kila mmoja wenu aliyepata mafunzo hayo akawe chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji,” alisema Nkhoma.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma - Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ireneus Kapoli, alisema kazi ya uandishi wa habari za uchunguzi si kazi rahisi, hivyo akawataka waandishi wote kuacha woga na kuandika habari za uchunguzi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma ya uandishi wa habari.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi 24 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.