Header Ads

MALARIA INAKUBALIKA TANZANIA

Happiness Katabazi

TANZANIA ipo kwenye kampeni kubwa ya kupambana na ugonjwa wa malaria ambao unapoteza idadi kubwa ya watoto, vijana pamoja na watu wazima.

Kampeni ya kupambana na malaria ilizinduliwa jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu na si mwingine ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Kama sehemu ya vita hiyo, nchi yetu imepokea misaada toka taasisi mbalimbali za kimataifa likiwemo Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID).

Katika misaada hiyo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wanaaminika ndio walio kwenye kundi la kuambukizwa kwa urahisi wamepewa fursa ya kupata vyandarua vya Olyset® Net. Ambavyo vina dawa ya kuzuia mbu.

Mfuko ulioifadhi vyandarua hivyo umeandikwa hivi; “(1)Fungua/Tundika chandarua hiki. (2) Lala ndani ya chandarua kila siku. (3) Hakihitaji kutiwa dawa; ‘Mbu wanapogusa chandarua cha Olyset ®wakati wakijaribu kuingia ndani, Huanguka chini na hatimaye hufa ....”

Mimi ni mama wa mtoto mmoja aitwaye Queen, ambaye kesho kutwa anatimizia umri wa miaka miwili, namshukuru Mungu kwa hilo.

Nilipata fursa ya kumchukulia mtoto wangu silaha hii kali ya maangamizi ya adui malaria kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Sinza C.

Niliipokea kwa shangwe nikiamini kwamba Queen sasa ataisikia malaria kwenye redio lakini nimepatwa na jinamizi baada ya kugundua kuna mbu wamejipenyeza kwenye chandarua hicho.

Mbu hao walikuwa wakicheza sindimba usiku kucha huku wengine wakining’inia kwa raha zao nje ya chandarua hicho kiasi cha kunishangaza nisiamini macho na akili zangu ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zikiamini kuwa mbu watakiona chandarua hicho kama kituo cha polisi.

Inabidi wataalamu wa masuala ya afya wanipe ushauri, na maelezo ya kina inakuwaje mbu hawa waliovinjari kwenye chandarua cha Queen wabakie hai licha ya kujigonga kwenye silaha kali ya maangamizi (neti)?

Ukweli niliyougundua ni huu, kwamba chandarua hiki cha Olyset® Net. ni kiini macho na ni usanii mkubwa uliofanyika wa kuwaadaa Watanzania tuamini kwamba mbu watakaogusa au kunaswa na chandarua hiki wataangamia mara moja.

Habari hizo si za kweli na inabidi wananchi tutafute mbinu nyingine ya kupambana na malaria ikiwa tunaamini kaulimbiu kwamba malaria haikubaliki.

Kwa wale walio katika mradi huu kitendo cha kuwaadaa wananchi kupitia chandarua hiki. Tunachoweza kusema mpango wao umebainika, fedha walizopata na watakazopata zisiwafanye wakajiona wajanja na kuwatafutia kifo wananchi.

Si jambo la busara kuendelea kuhamasisha matumizi ya vyandarua wakati tukijua fika kuwa njia hiyo haitufikishi kwenye mafanikio ya muda mfupi ya kupambana na mbu waenezao malaria.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inadaiwa kuwa imeshindwa kupendekeza dawa inayoweza kutibu malaria kwa gharama nafuu na bila ya kuwadhuru baadhi ya watumiaji.

Ilianza kupiga marufuku dawa ya Krorokwini na ikapendekeza dawa ya Metakefin na Fansidar lakini dawa zote hizo mbili zimeshindwa kutibu malaria kwa gharama nafuu bila kudhuru baadhi ya wananchi wanaozitumia.

Hivi sasa malaria ni ugonjwa sugu usiosikia dawa hapa nchini na tayari wizara hiyo imetuletea dawa ya Mseto ambayo nayo ni bomu la aina yake, kwani tayari kuna malalamiko toka kwa watumiaji wa dawa hiyo na bado malaria ni sugu.

Tujiulize, tatizo ni nini? Je, hatuna wataalamu wenye elimu ya kutosha ili kuliokoa taifa letu kwenye janga hili la malaria? Au ugonjwa huu ambao umegeuzwa kitega uchumi kama vile ugonjwa wa ukimwi ulivyogeuzwa kijiwe cha manyang’au wachache kuchuma na kujitajirisha?

Kwa kuwa Tanzania ni kama kichwa cha mwendawazimu kwa kila jambo, kashfa hii ya vyandarua ambayo pia navyo vimeshindwa kukabiliana na mbu hao ni sawa kama kashfa ya kutafunwa kwa fedha za kupambana na ukimwi na watu wasio na ukimwi.

Ni mambo ambayo yanaweza kuingia kwenye mlolongo wa kimfumo wa kisaliti na kifisadi uliojijenga kwenye utawala na utendaji wa umma.

Ni rahisi sisi wananchi kuvutwa na kampeni zinazoletwa na wafadhili ambao huja kwa kuzining’iniza ‘karoti’ tamu na watawala wetu udondokwa mate wanapozitazama lakini kamwe hawajali tupo wapi, tunataka nini na taifa linakwenda wapi.

Sisi kama taifa ni wachezaji wa ngoma yenye muziki tusioujua wala tusioweza kuupiga. Watoto wa Tanzania watakaondelea kuathirika na malaria licha ya kulala ndani ya vyandarua vilivyochemshwa kwenye dawa ambazo hatuzijui athari zake.

Ni vizuri wananchi tuanze kujijengea utamaduni wa kuhoji chanzo cha kampeni hizi za kitaifa zinaletwa na nani kwa kumlenga nani na kwa faida ya nani, ndipo tuanze kushabikia na kuzikubali.

Kampeni zinazokuja na bidhaa zinatolewa bure kama ilivyo kwenye kampeni hii ya malaria, zina mvuto wa kipekee lakini zina athari zake.

Ieleweke kwa Watanzania kwamba hapa duniani hatuna mjomba ,tusijijengee utamaduni wa kupenda vya bure kwani bure ina gharama zake. Nasikitika na kujilaumu kwamba taifa letu bado lipo kwenye utamaduni wa kupenda vya bure kutoka kwa wafadhili na wahisani
Si kweli kwamba zawadi ni zawadi hata ukipewa mfupa. Hapo zamani mfupa ulikuwa unamaanisha uchache na siyo udhaifu wa bidhaa au zawadi yenyewe.

Hivi leo mtu ukipewa zawadi isiyokidhi ubora, unakuwa ama umepewa taka au sumu, vyote ambavyo ni uchafuzi wa mazingira au kuleta madhara kwa afya ya binadamu.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii naiomba ijihadhari ili Tanzania isifanywe dampo la dawa au bidhaa zisizo na ubora unaotakiwa.

Ningefurahi kama ubora wa vyandarua vya Olyset® Net ungechunguzwa kitaalamu na wathibitishie umma uwezo wake wa kuua mbu na pia usalama wakwe kwa watumiaji.

Mwisho nimalizie kwa kuwataka wataalamu wote walioshiriki kumpelekea Rais Kikwete taarifa za wasizokuwa na uhakika nazo juu ya ubora wa vyandarua waache kufanya hivyo kwani wanahatarisha ustawi wa jamii.

Kumpelekea kiongozi mkuu wa nchi taarifa za ubora wa bidhaa fulani wakati haina ubora huo ni kumdhalilisha kiongozi huyo, lakini pia kutengeneza vifo vya watu wengi zaidi.

Binafsi naamini wataalamu wa afya wana upeo mpana wa kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa rais, nawaomba wafanye kazi zao kwa masilahi ya taifa badala ya kuwapendezesha wafadhili au wahisani wanaotoa ‘vijisenti’.

Rais anaposhiriki kwenye uzinduzi wa vyandarua ambavyo mwisho wa siku vinakuja kubainika kuwa si bora kwa kiwango kilichotarajiwa jamii inaweza kumuona naye ni miongoni mwa wasiowatakia mema wananchi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 6 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.