Header Ads

MTIKILA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi
MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, jana alifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa mawili ya kusambaza na kumiliki waraka wa uchochezi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Wakili wa Serikali Angel Chacha aliyekuwa akisaidiwa na Inspekta Francis Mboya mbele ya Hakimu Mkazi Michael Mteite alidai kuwa Mtikila amefanya makosa hayo ya uchochezi ambayo ni kinyume cha kifungu cha 32(1)(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Chacha alidai kuwa shtaka la kwanza ni kuwa mnamo Novemba mosi mwaka 2009-Aprili 17 mwaka huu, ndani ya jiji akiwa na nia ya uchochezi Mtikila alisambaza kwa umma waraka uliochapishwa ambao una kichwa cha habari kisemacho: ‘Kikwete kuangamiza ukristo, Wakristo waungane upesi wamuweke Mkristo Ikulu’ huku akijua maneno hayo ni ya kichochezi.

Alidai shtaka la pili ni kwamba Aprili 16, mwaka huu, huko nyumbani kwake Mikocheni bila kibali alikuwa akimiliki waraka huo wa kichochezi ambao ulikuwa na maneno hayo.
Kwa upande wake, Mtikila alikana mashtaka yote na wakili huyo wa serikali aliiambia mahakama kuwa hawana pingamizi na dhamana na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Aidha, Hakimu Mkazi Mteite alisema ili mshtakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika au wadhamini hao wawili watoe fedha taslimu sh 500,000 kila mmoja, lakini hata hivyo ilipofika saa saba mchana Mtikila alidhaminiwa na wadhamini wawili ambao wanatoka taasisi zinazotambulika kisheria na hivyo kumfanya apate dhamana.

Kabla ya hakimu kuingia ndani ya ukumbi wa mahakama kuanza kusikiliza kesi hiyo, Mtikila alisema maneno yafuatayo kwa sauti ya juu: ‘Serikali ilifikiri ikinileta leo (jana) mahakamani nitamkana Bwana wangu Yesu na mwokozi wangu…kamwe siwezi kumkana…nyie waandishi wa habari wengine si Wakristo jitokezeni basi mnidhamini au mnaogopa kushughulikiwa na serikali,” alisema Mtikila huku akionekana mwenye furaha muda wote.
Hii ni kesi ya pili ya kumkashifu Kikwete kufunguliwa katika mahakama ya Kisutu, kesi ya kwanza ambayo imeishaanza kusikilizwa ni ile aliyomuita kiongozi huyo wa nchi kuwa ni gaidi na anaukumbatia Uislamu.

Pia ni mara ya 41 sasa serikali inamfungulia kesi ya kutoa maneno ya uchochezi na kesi nyingi ameshinda isipokuwa kesi moja ya uchochezi iliyokuwa imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe mwishoni mwa miaka ya 1990, ambapo Mtikila alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi alipodai CCM ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba, na ndipo mahakama hiyo ya wilaya ilipomfunga jela mwaka mmoja na alitumikia kifungo hicho katika gereza la Ukonga.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 22 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.