Header Ads

BALOZI MAHALU KUANZA KUJITETEA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, umesema kwamba aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia,Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala wa Ubalozi huo Grace Martin wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na wizi wa zaidi ya Euro milioni mbili wataanza kujitetea Mei 31 mwaka huu.


Amri hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Ilvin Mugeta wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa na kuangalia kama uongozi wa mahakama hiyo umeishampanga hakimu mpya wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwasababu Machi 28 mwaka huu, Jaji Sivangilwa Mwangesi ambaye ndiye alikuwa akiisiliza kesi hiyo tangu awali kujitoa kwasababu mawakili wa washtakiwa waliwasilisha sababu sita kumtaka ajitoe kwasababu hawana imani naye kwani amekuwa akiendesha kesi hiyo kwa maslahi yake binafsi badala ya misingi ya kisheria.

“Tayari kesi hii imeshapangiwa hakimu wa kuendelea kuisikiliza na mimi (Mgeta) ndiye nimejipangia kusikiliza kesi hii na kwamba washtakiwa wataanza kujitetea Mei 31 na kesi hii itakuja kwaajili ya kutajwa Mei 18 mwaka huu… na mahakama hii imekubaliana na maombi ya Profesa Mahalu kwenda Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza kati ya Mei 12-22 na
Limekubali ombi la Grace la kwenye kijijini kwao mkoani Kilimanjaro kwa shughuli za kifamilia kuanzia Mei 4-15 mwaka huu”alisema Hakimu Mgeta.

Machi 28 mwaka huu, Jaji Sivangilwa Mwangesi alijitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo kufuatia sababu sita zilizowasilishwa mbele yake na jopo la mawakili wa utetezi linaoloongozwa na Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthbert Tenga Machi 25 mwaka huu, ambapo walimuomba jaji huyo ajitoe kwasababu hawana imani naye kwani amekuwa akiendesha kesi hiyo kwa malengo yake binafsi badala ya sheria.

Miongoni mwa sababu sita zilizowasilishwa na wakili Marando mbele ya Jaji Mwangesi siku hiyo ni kwamba upande wa utetezi ulishatoa mahakamani Kumbukumbu ya Bunge ‘Ansard’ ya Agosti 24 mwaka 2004 inayomnukuu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete akiliambia bunge kuwa taratibu za utafutaji, ununuaji wa jengo la ubalozi wa Tanzania ,Rome nchini Italia ulifuata taratibu zote za kisheria na kwamba fedha za ununuzi huo zilitumwa kwa awamu kwenye akaunti ya muuzaji na zilimfikia na kwamba hakukuwepo na wizi wowote lakini jaji huyo hakuzingatia ansard hiyo.

Sababu nyingine ya jaji huyo kukataliwa ni kwamba Jaji Mwangesi alipindisha kwa makusudi sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002 na akaamua kuchukua ushahidi wa shahidi wa Jamhuri aliyekuwa nchini Italia kwa njia ya video wakati sheria hiyo ya ushahidi ya hapa nchini inakataza na kwamba ndiyo maana hivi sasa serikali ipo kwenye mchakato wa kupelekwa mswaada bungeni wa kuifanyia marekebisho sheria iliyopo hivi sasa,ili ushahidi kwa njia video(video conference) uweze kuruhusiwa na mahakama zetu.

Mapema mwaka 2006 ,Jamhuri kupitia mawakili wake toka Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Ben Lincoln na Ponsian Lukosi iliwafikisha mahakamani hapo kwa mara ya kwanza washtakiwa hao kwa makosa ya uhujumu uchumi, wizi wa zaidi ya Euro milioni mbili wakati wakisimamiza ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome nchini Italia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.