Header Ads

HAKIMU KESI YA MANJI,MENGI AJITOA


Na Happiness Katabazi
HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Alocye Katemana ametangaza kujitoa kuendelea kusikiliza kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi na ITV.


Uamuzi huo aliutoa jana mahakamani wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa.Kesi hiyo ilikuja kutajwa kwa mara ya kwanza jana tangu jalada la kesi hiyo lilipotoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage Machi 29 mwaka huu ambaye aliamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa hakimu Katemana ambaye ndiye amekuwa akisikiliza kesi hiyo kwaajili ya kuendelea kusikiliza baada ya ukaguzi wake alioufanya katika jalada hilo akabaini kuwa hakimu huyo hakuwa amepindisha sheria yoyote wakati akiisiliza kesi hiyo.

Jalada la kesi hiyo ambayo lilitua katika Mahakama Kuu Machi 23 mwaka huu, likitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na barua ya Februali 23 mwaka huu, iliyoandikwa na wakili wa mdaiwa(Mengi) , Michael Ngaro kwa Jaji Mfawidhi Kaijage ambapo ndani ya barua hiyo Ngaro alimuomba apitie mwenendo mzima wa kesi kwani hawaridhishwi.

Hakimu Mkazi Katemana jana aliingia mahakamani hapo na wakili wa mlalamikaji(Manji), Dk.Ringo Tenga alianza kwa kujitambulisha kama ulivyo utaratibu wa kimahakama na wakili huyo alipomaliza Hakimu Katemana alieleza kuwa anafahamu kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya kutajwa ila anatangaza kujitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo na kusema kuwa hawezi kutaja sababu za kujitoa kwa umma na kwamba jalada la kesi hiyo analipeleka kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo ili aweze kumpangia hakimu mwingi.

“Kabla ya mawakili kuendelea naomba niwatangazie kuwa kuanzia leo(jana) najitoa kuendelea kusikiliza kesi hii na sababu za kujitoa sitazitangaza kwa umma hivyo basi nalirudisha jalada hili kwa hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hii ili aweze kumpanga hakimu mwingine ili aweze kuendelea kusikiliza kesi hii na ninaiarisha kesi hii hadi Aprili 15 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.”alisema Hakimu Katemana huku akionyesha kujiamini.

Uamuzi wa Hakimu Katemana wa kujitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo, kunakuja siku mbili baada ya mdaiwa katika kesi hiyo Na.85/2009, Reginald Mengi kufanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, na kulalamikia baadhi ya vichwa vya habari vilivyotokana na habari inayohusu kesi hiyo sambamba na kutoa matangazo katika magazeti kadhaa ambapo ndani ya matangazo hayo alilikuwa akilalamikia baadhi ya magazeti yanavyoripoti kesi hiyo na mambo mengine.

Februali 15 mwaka huu, Hakimu Mkazi Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyotolewa na hakimu huyo Februali 11 mwaka huu,ambapo hakimu huyu alikazikataa nyaraka vivuli 14 zikiwemo nyaraka ambazo zinaonyesha ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU),Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba wa kukopeshana fedha baina ya kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Kampuni ya Quality Finance Corporation Ltd , ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kanuni ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, zinakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.

Hakimu Katemana alisema siyo tu sheria hiyo ina kataza maamuzi madogo kama hayo aliyoyatoa kuyakatia rufaa pia nyaraka hizo 14 haziusiani na kesi iliyopo mbele yake, ni nyaraka vivuli ambazo hazijathibitishwa kisheria na pia hazionyeshi kama ofisi hizo za serikali zimetoa kibali kwa mdaiwa kutumia nyaraka hizo katika kesi hiyo na kuongeza kuwa nyaraka hizo zimewasilishwa nje ya muda mwafaka kwani kisheria zilipaswa kuwasilishwa kabla ya mlalamikaji kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake.

Mapema mwaka 2009, Manji anatetewa na mawakili maarufu nchini, Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk.Ringo Tenga na Beatus Malima alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.