Header Ads

KORTI KUU YASIKILIZA OMBI LA NG'UMBI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilisikiliza ombi dogo la aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM, Hawa Ng’umbi, la kuomba mahakama impatie msamaha wa kutolipa sh milioni 15 kama dhamana ya kesi yake ya kupinga ushindi wa mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika (Chadema).


Ng’umbi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza Mnyika kuwa mshindi, ana mshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, John Mnyika na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ambapo Mnyika anatetewa na wakili wa kujitegemea, Edson Mbogoro. Ng’umbi alifungua kesi Na. 107/2010 Machi 22 mwaka huu, akitaka mahakama hiyo itengue ushindi wa Mnyika kwa sababu sheria ya uchaguzi ilikiukwa.

Wakili wa Ng’umbi, Issa Maige, aliiomba mahakama hiyo chini ya Jaji Upendo Msuya anayesikiliza kesi hiyo imsamehe mteja wake asilipe kiasi hicho cha fedha kwa sababu hata Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002 haijaweka kigezo cha mteja wake kwamba ana uwezo wa kifedha, hivyo ni lazima alipe kiasi hicho cha fedha.

“Mheshimiwa Jaji tunaomba mahakama ilikubali ombi la mlalamikaji (Ng’umbi) la kutaka asamehewe asilipe dhamana hiyo na kwamba mahakama itupilie mbali pingamizi la wadaiwa ambao wanataka ombi la mteja wangu litupwe,” alidai wakili Maige.

Kwa upande wake wakili wa Mnyika, Edson Mbogoro na wakili wa serikali Sehel, waliomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa sababu mlalamikaji anajiweza kiuchumi, hivyo ana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kama sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002 inavyomtaka.

Jaji Msuya alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na ameahirisha kesi hadi Aprili 18 mwaka huu atakapotoa uamuzi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.