Header Ads

KWANINI WANAHABARI TUZUIE KURIPOTI KESI HII?


Na Happiness Katabazi
IJUMAA ya wiki iliyopita Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Elvin Mugeta alitoa amri ya kushangaza iliyovipiga marufuku vyombo vya habari nchini kuripoti mwenendo wa kesi ya madai Na.85/2009 ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mfanyabishara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na ITV.


Mapema mwaka 2009, Manji anayetetewa na mawakili maarufu nchini, Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk.Ringo Tenga na Beatus Malima alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake hiyo kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Maelekezo hayo ambayo yalitushtua baadhi ya waandishi wa habari za mahakamani waliokuwa ndani ya chumba hivyo, yalitolewa na Hakimu Mgeta ambapo siku hiyo kesi ilikuja kwaajili ya kutajwa.Mshangao huo uliotukumba wanahabari ulisababisha baada ya hakimu huyo kutoka mahakamani kumfuata ofisini kwake ili aweze kutufafanulia kwa mapana hayo maelekezo yake na kweli hakimu huyo alitufafanulia.

“Naomba mnisikilize kwa makini na utulivu kabisa na nitaongeza sauti ili muweze kunisikia vizuri licha kuna kelele za mafundi ujenzi ...maelekezo hayo ni kama yafuatavyo ni kwamba kuanzia sasa vyombo vya habari yaani magazeti na vile vya electroniki havitaruhusiwa kuripoti mwenendo wa kesi hii kwasababu kufanya hivyo kuna athiri uhuru wa hakimu na mahakama na sababu za maelekezo hayo hatuna sababu ya kuzitaja adharani kwani imefika mahala mahakama ya kisutu haipumui.

Kwa wale wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi hii, watakumbuka kuwa Aprili 8 mwaka huu, Hakimu Mkazi , Alocye Katemana alitangaza kujitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo na kusema kuwa hawezi kutaja sababu za kujitoa kwa umma.

Katemana alitoa uamuzi huo ikiwa ni mara ya kwanza siku hiyo tangu jalada la kesi hiyo lilipotoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage Machi 29 mwaka huu ambaye aliamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa hakimu Katemana ambaye ndiye amekuwa akisikiliza kesi hiyo kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

Jalada la kesi hiyo ambayo lilitua katika Mahakama Kuu Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, likitokea Mahakama ya Kisutu kutokana na barua ya Februali 23 mwaka huu, iliyoandikwa na wakili wa mdaiwa(Mengi) , Michael Ngaro kwa Jaji Mfawidhi Kaijage ambapo ndani ya barua hiyo Ngaro alimuomba jaji huyo apitie mwenendo mzima wa kesi.


Uamuzi wa Hakimu Katemana wa kujitoa, kulikuja siku mbili baada ya mdaiwa katika kesi hiyo Mengi kufanya mkutano na waandishi wa habari na kulalamikia baadhi ya vichwa vya habari vilivyotokana na habari inayohusu kesi hiyo sambamba na kutoa matangazo katika magazeti kadhaa ambapo ndani ya matangazo hayo alilikuwa akilalamikia baadhi ya magazeti yanavyoripoti kesi hiyo na mambo mengine.

Februali 15 mwaka huu, Hakimu Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyotolewa na hakimu huyo Februali 11 mwaka huu,ambapo hakimu huyu alikazikataa nyaraka vivuli 14 zikiwemo nyaraka ambazo zinaonyesha ni mali ya TAKUKURU,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba wa kukopeshana fedha baina ya kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Kampuni ya Quality Finance Corporation Ltd , ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kanuni ambazo Na. 25 ya mwaka 2002, zinakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na ya chini .

Kwa muktadha huo hapo juu binafsi nimeshangazwa ana amri hiyo licha nafahamu fika kuwa mahakama inaweza kutoa amri kadhaa kwenye masuala kadha wa kadha kwasababu mahakama zetu zimepewa nguvu ya kipekee(discretion Power) ambazo si lazima ziwe zimeanishwa kwenye vitabu vya sheria.Na ndiyo maaana hakimu huyo wakati akitoa maelekezo hayo hakunukuu kifungu chochote cha sheria.

Maelekezo hayo ambayo hayakutaja wazi sababu za kutuzuia kuripoti kesi hiyo siyo tu yamenyima haki vyombo vya habari ya kuchapisha habari ya kesi hiyo pia unanyima umma wa watanzania kufahamu kinaochendelea kwenye kesi hiyo ambayo hadi sasa ni shahidi mmoja tu (Manji) ambaye ndiye ametoa utetezi wake.

Ieleweke kwamba makala hii haina lengo la kuidharau au kuipinga amri hiyo la hasha kwani mwandishi wa safu hii ana heshimu uhuru wa mahakama na utawala wa sheria.Ila katika akili yake amekuwa akijiuliza Je ni kwanini Hakimu Mgeta kabla ya kutoa amri hiyo ambayo inaacha maswali mengi kuliko majibu hakueleza bayana sababu za kufikia uamuzi huo?

Uenda uamuzi huo umetokana na baadhi ya sisi waandishi waandishi wa habari za mahakamani tumeripoti kinyume ,lakini kama hivyo ndivyo,Je ni kwanini hakimu huyo asingeona haja ya kabla ya kufikia uamuzi huo wa kushtusha angewaita wahariri na waandishi waliondika visivyo kuwahoji,kutuelekeza tumekosoa wapi ili kesho tusirudie makosa hayo?

Fukuto la Jamii kila siku linaamini mahakama ni kama shule ambapo kwa wananchi wanaofuatilia mashauri mbalimbali upata fursa ya kujifunza vitu vipya vya kisheria kila siku, sasa Hakimu Mgeta haoni amri yake hiyo kwa njia moja ama nyingine inanyima fursa ya wananchi kujifunza kupitia kesi hiyo matajiri wawili yaani Manji anamtaka Mengi amlipe shilingi moja ili hali Manji amekodi mawakili maarufu nchini wamtetee?

Mgeta alisema eti kesi hiyo imeripotiwa sana na vyombo vya habari.Binafsi uwa sipendi unafki na katika hili sitamung’unya maneno hoja ya kesi hiyo minaiita ni hoja mfu,isiyo na mantiki ya kisheria na haina ukweli wowote kwani Watanzania wote wakiwemo mabosi wake Mgeta ni mashahidi kwamba hakuna kesi iliyoandikwa sana tena kwa miaka miaka minne mfululizo kama kesi ya Mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili , ACP-Abdallah Zombe na wenzake, kesi za EPA, kesi za matumuzi mabaya ya ofisi za umma iliyokuwa ikimkabili Amatus Liyumba,Profesa Costa Mahalu, Bazir Mramba na wenzake.

Sote tungali tukikumbuka jinsi ya vyombo vingi vya habari vilivyokuwa vikiripoti kesi ya Zombe kishabiki na upotoshaji wa hali ya juu hali iliyosababisha kabla ya hata Jaji wa Mahakama ya Rufaa Salum Massati kutoa hukumu yake Agosti 17 mwaka 2009, tayari umma na vyombo hivyo vya habari vilikuwa vimeishamhukumu Zombe kuwa ni muaji na anastahili adhabu ya kunyongwa na kamba hadi kufa.

Na siku zote hizo hatukuusikia mhimili wa mahakama ukitokeza adharani kukemea vyombo vya habari wala kuvizuia na wala hatukumsikia Jaji Massati akikemea hali hiyo zaidi jaji huyo alikuwa akivumilia vituko vyote vilivyokuwa vikitendeka ndani na nje ya mahakama hadi mwisho wa siku alivyokuja kutoa hukumu yake ya kushtusha ambapo aliwaachiria huru washtakiwa wote kwani alibaini ushahidi uliotolewa na jamhuri ulikuwa ni dhaifu.

Na wakati yote hayo yakitendeka Hakimu Mgeta alikuwa yumo ndani ya mhimili wa mahakama, tumuulize je alishawahi kutoa maoni kwa wakubwa zake wavizuie vyombo vya habari visiripoti kesi hiyo?

Kwa kuwa Hakimu Mgeta amevipiga marufuku vyombo vya electroniki na magazeti, tumuulize je wale waandishi wanaotafuta habari na kutawanya kwenye mitandao ‘on line’ kama Jamii Forum, blogg nao hawataruhusiwa kuripoti ushahidi wa kesi hiyo?

Mbona baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kesi ya mauji ya mtoto Salome Yohana inayomkabili Ramadhani Mussa na mama yake na vyombo hivyo vilikuwa havimtendei haki mtoto huyo vinamuita ‘Rama Mla watu”,iliyofunguliwa mahakama ya Kisutu kabla ya kuamishiwa Mahakama Kuu, mbona hatujakusikia ukitoa amri kama hiyo?.Maana maandishi hayo yalikuwa yameishamhukumu Ramadhani kuwa anakula vichwa vya watu wakati bado kesi yake haijatolewa hukumu.?

Kwa watu kama sisi tunaofikiri sawa sawa , tuna hoji ni kwanini Hakimu Mgeta ambaye hajabainisha wazi kwamba yeye ndiye atasikiliza kesi hiyo au atampanga hakimu mwingine, ni kwanini amekuwa mwepesi mno kutoa amri hiyo na mbona kuna kesi nzito zinazohusiha waliokuwa vigogo wa serikali, watuhumiwa wa ujambazi wanaokabiliwa na kesi za unyang’anyi wa kutumia silaha,rushwa ya ngono,kesi za ndoa ambazo baadhi mashahidi wamekuwa wakitoa ushahidi ambao unafichua mbinu za kipelelezi zilizotumiwa na makachero ‘manusanusa,machatu’ wetu kuwakamata wahalifu lakini hatujamsikia hakimu huyo akitoa maelekezo kuzuia tusiripoti ?

Kwani siyo siri ushahidi unotolewaga na baadhi ya wapelelezi unakuwa mbinu na mikakati inayotumiwa na ‘manusanusa’ wetu kuwakamata wahalifu hivyo ushahidi huo unakuwa unatoa faida kwa wahalifu ambao hawajatiwa nguvuni kuwakwepa ‘manusanusa’.?

Mbona mabosi wako kule Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa hawajawi kutupiga marufu kuripoti kesi wanazoziendesha?Maana kesi nzito kama za mauji, kesi mgombea binafsi,kesi ya ubakaji inayomkabili mwana muziki nguli wa dansi, Nguza Vicking ‘Babu Seya na Papi Kocha,kesi ya kusajiliwa tuzo ya kampuni ya Dowans dhidi ya Tanesco,kesi ya madai dhidi ya Dk.Wilbroad Slaa ya kudaiwa kuiba mke wa mtu,kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010,kesi wizi wa samaki wa Magufuli’zimekuwa zikiendeshwa huko na kuudhuliwa na mamia ya wananchi ukitofautisha na kesi hiyo ya manji na mengi ambayo uudhuliwa na watu wachache sana.

Wanahabari tumebaki tukijiuliza kuhusu uamuzi huo kwamba uenda hakimu huyo amepata taarifa za Kiintelijensi kwamba kuripotiwa kesi hiyo kutaatarisha usalama wa wafanyabiashara hao na taifa?.

Hatukusikia uongozi wa mahakama nchini ukitoa maelekezo ya kuvikataza vyombo vya habari kutoripoti kesi, zaidi zaidi sisi waandishi wa habari za mahakama tumekuwa tukishuhudia mawakili wa washtakiwa wenyewe pindi wanapoona baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti uongo, wamekuwa wakifika na magezeti hayo mahakamani na kuiomba mahakama iyaonye magazeti hayo na ndiyo maana amri hiyo ya mahakama imetushangaza sana kwani ni mpya.

Siyo siri tena kwamba tumeanza kupatwa na wasiwasi kuwa huko mbele ya safari baadhi ya mahakimu wetu ambao siyo waadilifu wanaweza wakatumia gia kama ya hakimu Mgeta ambaye sisemi siyo mhadilifu kuvizuia vyombo vya habari visiripoti kesi nyingine ambazo zinafuatiliwa hatua kwa hatua na jamii ambazo zinaonekana kumuelemea mlalamikaji au mdaiwa ambao wana ukaribu nao.

Fukuto la Jamii linasisitiza kuwa lina heshimu uhuru wa mahakama ila amri ya hakimu Mgeta imetuachia maswali mengi kuliko majibu.Na amri hiyo inataka kufanana na amri ‘shindwa’ iliyowahi kutolewa na mtangulizi wako Addy Lyamuya ,Februali mwaka juzi, siku ya kwanza kabisa kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.8 katika akaunti ya EPA inayomkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijara Hussein ilipoanza kusikilizwa rasmi kuwataka waandishi wa habari waweke peni chini eti si kila mtu anaruhusiwa kuripoti kesi.

Lyamuya alitoa amri hiyo ambayo ni amri ‘kihoja’ ambayo ilisababisha waandishi wa habari kuchachamaa na kesho yake asubuhi alimtuma karani wake kuwaita waandishi wahabari ofisini kwake bila ya kutoa ufafanuzi wowote akasema hataki malumbano akasema ni lazima kila siku tujiandikishe majina kabla ya kuingia mahakamani utaratibu ambao halishindwa kuusimamia hadi anastaafu kwani mimi , Grace Michale wa Majira na Faustine Kapama wa Dailnews kwa kauli moja tulimweleza utaratibu wake utatuwia vigumu kuutekeleza na kweli utaratibu huo ulikufa ndani ya siku mbili.

Tunamuomba Mgeta kufikiria upya amri yake.Pia tunamuomba Jaji Mkuu Chande Othman, Jaji Kiongozi Fakhi Jundu,Jaji Mfawidhi Semistocles Kaijage na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,Amir Msumi kuutazama upya amri ya hakimu huyo kwani wakae wakijua siku hizi hakuna siri hapa nchini, sisi waandishi wachokonozi ambao tunaouwezo mkubwa tu wa kutafuta kilichomsukuma hakimu huyo kutoa maelekezo hayo na hatimaye tutakianika na mwisho wa siku itayochafuka ni mhimili mzima wa mahakama na siyo hakimu huyo.

Ieleweke kuwa tangu amri hiyo itolewe tayari mitaani baadhi ya wananchi wameanza kuwa na fikra mbaya kuhusu amri hiyo.Ila tunavyoifahamu mahakama yetu ni mahakama isiyona ubaguzi wakati wakuzishughulikia kesi mbali mbalimbali.Kesi zinazowahusu watoto chini ya umri wa miaka 18 kwa mujibu wa sheria vyombo vya habari haviruhusiwi kuziripoti lakini tunashangwazwa kesi hii ambayo ni ya madai y ash moja ambayo hata serikali yake haijashtaki au kushtakiwa mahakama ya Kisutu kwa nguvu ilizonazo imeamua kuingilia kati na kutupiga marufuku tusiripoti ushahidi utakaotolewa mahakamani.Inashangaza sana.

Namalizia kwa kujiuliza tena na tena hivi ni kwanini Hakimu Mgeta atupige marufuku kuripoti ushahidi wa kesi ya Manji na Mengi tu?Mahakama ya Kisutu ina nini katika kesi hiyo ya madai ya shilingi moja hadi kufikia uamuzi wa kutoa amri hiyo ambayo ni ngeni kutolewa na mahakama zetu hapa nchini?Hivi kesi hii ina unyeti gani ? Wakati ukifika tutakuja kujua chanzo cha kutolewa maelekezo hayo nini. Naomba kutoa hoja.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.