Header Ads

KESI YA ZOMBE YAPANGIWA JAJI

Na Happiness Katabazi

UONGOZI wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, umempangia Jaji Upendo Msuya kusikiliza kesi ya madai ya fidia ya sh bilioni tano iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (57) dhidi ya serikali.


Kwa mujibu wa hati ya kuitwa mahakamani iliyotolewa na mahakama hiyo Machi 16, inazitaka pande zote katika kesi hiyo wafike mahakamani hapo Mei 16 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itatajwa kwa mara ya kwanza tangu ilipofunguliwa.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Zombe alithibitisha kupokea hati ya wito iliyotolewa na mahakama hiyo.

“Kwa sasa nipo Morogoro kwenye shughuli zangu za kujiingizia kipato ila ni kweli nimeishapokea hati hiyo ya kuitwa mahakamani Mei 16 mwaka huu, siku hiyo ya kesi nitahudhuria,” alisema Zombe.

Machi 7 mwaka huu, Zombe kupitia wakili wake, Richard Rweyongeza, alifungua kesi namba 35/2011 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jeshi la Polisi na akataja sababu 21 za kufungua kesi hiyo ya madai ya fidia ya kutaka alipwe sh bilioni tano na riba ya sh milioni 200.

Zombe anadai Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa ni lazima aelezwe anakamatwa kwa sababu gani na akifikishwa kituo cha polisi ni lazima ahojiwe na kuchukuliwa maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo, lakini jeshi hilo lilitenda kinyume cha sheria hiyo.

Zombe anadai sababu nyingine iliyosababisha afungue kesi hiyo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema kushindwa kulijibu kusudio lake la kuishitaki serikali ambalo lilipaswa kujibiwa ndani ya siku 90.

Agosti 17, mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimwachia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Baada ya hukumu hiyo, serikali ilikata rufaa Oktoba 7 mwaka 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu hiyo, hata hivyo ilishindwa baada ya mahakama kueleza kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashitaka hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Aprili 11 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.