WAANDISHI WAPIGWA MARUFUKU KESI YA MANJI,MENGI
Na Happiness Katabazi
KATIKA hali ya kustaajabisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam,jana ilitoa maelekezo ya kuvizuia vyombo vyote vya habari nchini kuripoti mwenendo mzima wa kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi na ITV.
Maelekezo hayo yalitolewa jana saa nane mchana na Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta wakati kesi hiyo ya madai Na. 85/2009 ilikuja kwaajili ya kutajwa.
“Kesi hii imekuja leo(jana) kwaajili ya kutajwa lakini naomba mnisikilize kwa makini na utulivu kabisa na nitaongeza sauti ili muweze kunisikia vizuri...maelekezo hayo ni kama yafuatavyo ni kwamba kuanzia sasa vyombo vya habari yaani magazeti na vile vya electroniki havitaruhusiwa kuripoti mwenendo wa kesi hii kwasababu kufanya hivyo kuna athiri uhuru wa hakimu na mahakama;
“Vyombo vya habari katika hili tunaomba mtuwie radhi sana kwani tumevumilia mno hivyo mahakama ina sababu za msingi za kutoa maelekezo hayo na haina sababu ila haitaki kuzitaja sababu hizo adharani kwani taarifa mbili zinazokithana yaani ushahidi unaotolewa na shahidi mahakamani na ushahidi unaoandikwa kwenye vyombo vya habari kuhusu kesi hii zimeathiri hakimu na mahakama kwa ujumla kwani ilifika mahala mahakama haipumui;
Aidha Hakimu Mugeta alisema mahakama hiyo ni mahakama ya wazi hivyo wananchi wataruhusiwa kuudhuria kesi hiyo ila mashahidi wakati wanaotoa ushahidi wao vyombo vya habari havitaruhusiwa kuripoti ushahidi huo badala yake vitaruhusiwa kuripoti tarehe za kesi hiyo zilizopangwa, maamuzi madogo madogo yatakayotolewa na hukumu itakapotolewa”alisema Hakimu Mgeta na kuwafanya waandishi wa habari kushikwa na butwaa.
Baada ya kutoa maelekezo hayo Hakimu Mugeta alipanga tarehe ya kesi hiyo kuendelea kusikilizwa ambayo ni Juni 3 mwaka huu, lakini akazieleza pande hizo mbili kuwa hakimu mpya ambaye amepangwa kuendelea na kesi hiyo baada ya yule hakimu wa mwanzo kujitoa, watamjua siku ya tarehe hiyo kesi itakapoja kwaajili ya kusikilizwa.
Hata hivyo waandishi wa habari za mahakama walivyotoka nje ukumbi wa mahakama hiyo walisema wanashangazwa na maelekezo hayo na kuhoji ni kwanini maelekezo ya aina hiyo yametolewa kwenye kesi hiyo na siyo kesi nyingine ambazo zina maslahi ya umma moja kwa moja.
Aprili 8 mwaka huu, Hakimu Mkazi , Alocye Katemana alitangaza kujitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo kesi hiyo na kusema kuwa hawezi kutaja sababu za kujitoa kwa umma na kwamba jalada la kesi hiyo analipeleka kwa Hakimu Mkuu Mkazi Elvin Mgeta kumpangia hakimu mwingine.
Katemana alitoa uamuzi huo ikiwa ni mara ya kwanza siku hiyo tangu jalada la kesi hiyo lilipotoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage Machi 29 mwaka huu ambaye aliamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa hakimu Katemana ambaye ndiye amekuwa akisikiliza kesi hiyo kwaajili ya kuendelea kusikiliza baada ya ukaguzi wake alioufanya katika jalada hilo akabaini kuwa hakimu huyo hakuwa amepindisha sheria yoyote wakati akiisiliza kesi hiyo.
Jalada la kesi hiyo ambayo lilitua katika Mahakama Kuu Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, likitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na barua ya Februali 23 mwaka huu, iliyoandikwa na wakili wa mdaiwa(Mengi) , Michael Ngaro kwa Jaji Mfawidhi Kaijage ambapo ndani ya barua hiyo Ngaro alimuomba apitie mwenendo mzima wa kesi kwani hawaridhishwi.
Uamuzi wa Hakimu Katemana wa kujitoa, kulikuja siku mbili baada ya mdaiwa katika kesi hiyo Na.85/2009, Reginald Mengi kufanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, na kulalamikia baadhi ya vichwa vya habari vilivyotokana na habari inayohusu kesi hiyo sambamba na kutoa matangazo katika magazeti kadhaa ambapo ndani ya matangazo hayo alilikuwa akilalamikia baadhi ya magazeti yanavyoripoti kesi hiyo na mambo mengine.
Februali 15 mwaka huu, Hakimu Mkazi Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyotolewa na hakimu huyo Februali 11 mwaka huu,ambapo hakimu huyu alikazikataa nyaraka vivuli 14 zikiwemo nyaraka ambazo zinaonyesha ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU),Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba wa kukopeshana fedha baina ya kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Kampuni ya Quality Finance Corporation Ltd , ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kanuni ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, zinakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.
Hakimu Katemana alisema siyo tu sheria hiyo ina kataza maamuzi madogo kama hayo aliyoyatoa kuyakatia rufaa pia nyaraka hizo 14 haziusiani na kesi iliyopo mbele yake, ni nyaraka vivuli ambazo hazijathibitishwa kisheria na pia hazionyeshi kama ofisi hizo za serikali zimetoa kibali kwa mdaiwa kutumia nyaraka hizo katika kesi hiyo na kuongeza kuwa nyaraka hizo zimewasilishwa nje ya muda mwafaka kwani kisheria zilipaswa kuwasilishwa kabla ya mlalamikaji kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake.
Mapema mwaka 2009, Manji anayetetewa na mawakili maarufu nchini, Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk.Ringo Tenga na Beatus Malima alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 16 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment