Header Ads

KESI YA N'GUMBI,MNYIKA KUSIKILIZWA APRIL 8

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Ijumaa ya wiki hii itasikiliza ombi dogo la aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya (CCM) la kuomba mahakama hiyo impatie msamaha wa kutolipa sh.milioni 15 kama dhamana ya kesi yake ya kupinga ubunge wa mbunge wa Jimbo la Ubungo(CHADEMA), John Myika.


Ng’umbi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza Mnyika kuwa mshindi, ana mshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, John Mnyika na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo ambapo Mnyika anatetewa na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro. Ng’umbi alifungua kesi Na.107/2010 Machi 22 mwaka huu, akitaka mahakama hiyo itengue ushindi wa Mnyika kwasababu sheria ya Uchaguzi ilikiukwa.

Msajili wa wilaya ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salam , Amir Msumi aliyasema hayo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa na akasema tayari uongozi wa kesi hiyo umeishampanga jaji wa kuisikiliza kesi hiyo na kwamba kesi hiyo itasikilizwa na Jaji Upendo Msuya.

Juzi Mnyika aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo dhidi ya ombi hilo dogo la mlalamikaji(Ng’umbi) la kutaka asamehewe kiasi hicho cha fedha , ambapo aliomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi la mlalamikaji kwasababu mlalamikaji ana jiweza kiuchumi hiyo anauwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kama sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002 inavyomtaka mlalamikaji katika kesi ya uchaguzi kuweka mahakamani shilingi milioni tano kwa kila mdaiwa anayemshtaki.

Mnyika katika pingamizi hilo ambalo Tanzania Daima linalo nakala yake anadai kuwa sababu nyingine ya kuwasilisha pingamizi dhidi ya Ng’umbi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe ni kwamba ombi hilo la msamaha mlalamikaji ameshindwa kutaja sababu zinazoonyesha yeye hana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.

“Tena tunaomba mahakama kuu ilitupe ombi kwasababu naamini huyu mlalamikaji kwanza alishawahi kuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero na sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe na ana vyeo vingine hivyo.... ana uwezo wa kiuchumi ambao unamruhusu kulipa mahakamani dhamana hiyo hivyo naomba mahakama hii tukufu isikubali huo msamaha wake kwasababu naamini anao uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.”alidai Mnyika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Aprili 6 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.