Header Ads

FEDHA ZA MISAADA ZISIVURUGE WANATAALUMA


Na Happiness Katabazi

HABARI za mtandao wa Wiki leaks zinazosema kwamba fedha za Marekani za Millennium Challenge Account zimekuwa zikitumika kuiwezesha Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutekeleza mpango wake wa kufungua kesi zenye mvuto kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kila siku; ni jambo la kushangaza na kutia aibu.


Katika mfumo wa jamii ya Kidemokrasia na Utawala Bora huzingatia mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.Takukuru ni chombo cha serikali kilicho chini ya Ofisi ya Rais.

Inapotokea habari iliyojaa tuhuma kwamba chombo hicho kina mkakati wa kuwaburuza mahakamani baadhi ya wananchi, ni kashfa kubwa na uonevu wa hali ya juu.

Tunapozungumzia ufisadi, tunamaanisha uozo ndani ya serikali basi kitendo hicho ni cha kifisadi, udhalimu na kwa maana hiyo endapo chombo cha serikali cha ufisadi na uonevu kwa baadhi ya raia wetu wasiyo na hatia, ina maana kwamba baadhi ya kesi tunazosikia na kuziona si kesi zilizofanyiwa uchunguzi makini.

Ni kesi za kubambikiza ili tupate sifa Marekani na nchi nyingine.

Hivi sasa kumekuwa na tuhuma zinazotolewa chinichini na wanataaluma ya sheria nchini kuwa baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa wakitoa maelekezo kwa baadhi ya mahakimu na majaji wetu kuamua kesi kwa kupendelea upande wa Jamhuri.

Kwa maana hiyo tuhuma hizo ambazo zimedhirisha katika mtandao wa Wiki leaks hivi karibuni zimetuambia kwamba mahakamani siku hizi si shwari tena.

Ile imani tuliyokuwa nayo kwamba mahakama ni hekalu la haki sasa haina msingi tena wa kuegemea.

Ikiwa ni kweli baadhi ya majaji na mahakimu wetu wanaelekezwa au kushawishiwa na serikali angalau kuwatia hatiani katika mahakama za chini ili waje kuachiliwa kwenye rufaa.

Kutokana na kuwepo kwa taarifa za mtandao huo hivi karibuni, serikali yetu haijazikanusha hadi sasa kwamba fedha za Millennium Challenge Account zinatumika nchini kwa minajili ya kidhalimu.

Kwa kuwa serikali ya Marekani haijakanusha pia tuhuma hizo, sisi tumebakiwa midomo wazi kuhusu Uhuru wa Mahakama zetu na kuhusu mustakabali wa utawala bora nchini.

Tuna historia ya muda mrefu ya kuwa na Takukuru lakini hakuna kipindi cha historia cha taasisi hiyo kuwa na manung’uniko ya uonevu, ubambikiaji kesi kama kipindi hiki.

Kwa namna ya pekee wakati mwingine tunaona Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, nayo imekuwa ikituhumiwa chini chini kuwa imebaki kuwa kituo cha kupitisha maamuzi ya mashtaka yaliyokwisha chukuliwa na ngazi za juu serikalini badala ya maamuzi hayo kuchukuwaliwa kwa misingi ya kitaaaluma.

Tumeona jinsi baadhi ya waliokuwa watuhumiwa wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania(BoT), walivyoshughulikiwa kwani kuna wengine walipewa msamaha kabla ya kushtakiwa eti kwasababu walirudisha fedha na wengine wakaburuzwa pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Sasa kwa mktadha huo kuna uchaguzi wa nani ashtakiwe na nani asishtakiwe wakati wote walituhumiwa kuvunja sheria za nchi kama hao walioshtakiwa mahakamani.

Kamwe hakutufanyi tuheshimu baadhi ya taasisi zetu za seriakali kwa kuwa inaonyesha wazi zimehusika katika udhalimu huo.

Fukuto la Jamii linahitimisha kwa kusema kama tuhuma hizo zilizotandazwa kwenye mtandao huo, na zile zinazotolewa na baadhi ya mawakili wa kujitegemea na maofisa wengine wa serikali kwamba kuna baadhi ya kesi zinafunguliwa kwaajili ya vigogo fulani kulipiza kisasi na kwamba katika kesi hizo ofisi ya DPP na baadhi ya majaji na mahakimu waoga wanakuwa wanashindwa kutenda haki kwa ajili ya kuogopa vitisho.

Basi makundi hayo yote hayana budi kuondokana na udhalimu huo kwani wakumbuke vyeo ni dhamana na walipokuwa vyuoni wanasoma sheria hawakufundishwa kuonea watu kwa ajili ya kuwafurahisha waliowateua au kupokea rushwa.

Licha baadhi ya mawakili wa kujitegema kuwa miongoni mwao nao wamekuwa wakilalamikiwa na baadhi ya mawakili wa serikali kuwa wamekuwa wakikwamisha kesi zinazofunguliwa na Jamhuri kwa makusudi kwa kuwasilisha pingamizi mahakamani kila kukicha ili waweze kukata ngebe ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi na Takukuru kwa madai kwamba ofisi hizo zimekuwa zikitumiwa na serikali kuwabambikizia kesi baadhi ya wateja wao ili serikali ionekane haifanyi kazi.

Lakini kwa kufanya hivyo ni kuendelea kuwachochea baadhi ya wananchi waendelee kuichukia serikali yao na mahakama.

Na ikumbukwe kuwa mwananchi yoyote anayeamini amedhurumiwa haki yake kimbilio lake ni mahakamani.

Lakini kwa watu wenye akili timamu huwa tunajiuliza hivi huo udhalimu wote unaofanywa na baadhi ya wanataaluma ya sheria na wapelelezi una tija gani kwa taifa hili?

Binafsi naona hauna tija kwa taifa letu hata kidogo zaidi ni kujenga taifa la wananchi wenye wenye moyo wa visasi na kuleteana umaskini kwenye familia.

Kila mwanataaluma atimize wajibu wake kwa mujibu wa maadili ya kazi yake na asikubali kutumiwa vibaya kwani vitabu vya dini vinatueleza kuwa Mungu yupo; na kesho kwa Mungu kuna moto kwa wale wote wanaokwenda kinyume na matakwa yake.

Hivyo mhimili wa mahakama nao hauna budi kujiondoa katika kashfa za tuhuma hizo kwani ningali nikikumbuka wosia uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete, katika Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 2 mwaka huu katika Viwanja vya Mahakama Kuu, aliitaka mahakama ijisafishe kwani ndani ya mhimili huo kuna baadhi ya mahakimu na majaji wanatuhumiwa kukiuka maadili ya kazi yao na viapo vyao.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.