Header Ads

MAHABUSU WATOROKA CHINI YA ULINZI MAHAKAMA YA KISUTU

Na Happiness Katabazi

MAHABUSU wawili wanaokabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Na. 253/2010 , Shida Luanda na Samuel Oyugi, wametoroka wakiwa katika harakati za kufungwa pingu na askari Maregeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jiji Dar es Salaam.


Tukio hilo la aina yake lilitokea jana saa 3.30 asubuhi mahakamani hapo, ikiwa ni muda mfupi baada ya mahabusu hao wakiwa na wenzao wengine wawili Hakimu Mkazi Sundi Fimbo kuarisha kesi yao.Washitakiwa hao ambao walitoroka kwa kuruka ukuta wa mahakama hiyo, hata hivyo askari wanaolinda mahakama hiyo walifanikiwa kumkamata Luanda, nje ya eneohilo na Oyugi alifanikiwa kutoroka moja kwa moja hajapatikana hadi saa tisa alasiri wakati gazeti hili linaondoka mahakamani hapo.

Wanausalama hao baada ya kufanikiwa kumkamata Luanda walimpandisha kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mustapher Siyani na kufunguliwa kesi mpya ya kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Magereza.

Wakili wa serikali Zuberi Mkakuti ndiye aliyesoma hati mpya ya dhidi ya mshtakiwa huyo ambapo alidai Luanda anakabiliwa na kosa la kutoroka chini ulinzi wa askari Magereza Rashid Gwakisa na Ibrahim na kwamba kosa hilo alilitenda jana saa tatu asubuhi mahakamani hapo.

Mshitakiwa huyo ambaye shati lake alilokuwa amelivaa mwilini lilikuwa limechanika kwa nyuma na hivyo kumfanya kulifunga huku akiwa hana viatu mguuni, alikana shtaka hilo ambapo Wakili Mkakatu alidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na jana hiyo akamsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo.

Katika maelezo hayo, inadaiwa Luanda , Oyugi, Ismail Shabani na Hati Jawadu, walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Fimbo, kusomewa mashitaka katika kesi ya jinai Na. 253/2010.Mkakatu alidai baada ya washitakiwa hao kutoka kwa Hakimu Fimbo, wakiwa kwenye ‘korido’ la mahakama chini ya ulinzi wa askari hao ambao walikuwa wanawafunga pingu, Luanda na Oyugi walitumia nguvu na kujinasua kutoka kwenye pingu.

Ilidaiwa washitakiwa hao walimpiga kifuani askari Rashid na kukimbia ambapo katika harakati za askari hao kuwafukuza, waliruka ukuta wa mahakama ya Kisutu na kurukia upande wa pili ambao ni jingo la Maktaba ya Taifa. Mkakatu alidai askari walifanikiwa kumkamata Luanda nje ya eneo hilo na kufikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kutoroka akiwa chini ya ulinzi.

Katika maelezo hayo ya awali aliyosomewa, Luanda alikubali kuwa jina na umri ni vyake. Upande wa mashitaka ulidai una mashahidi watatu ambao ni askari waliotorokwa na washitakiwa.Luanda na Oyugi walitoroka mahakamani hapo kwa kupanda katika vyuma vilivyofungwa na mafundi wanaofanya ukarabati ndani ya ofisi za mahakama hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 12 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.