Header Ads

KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI YAPATA JAJI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, umempanga Jaji Agustine Mwarija kuendelea usikiliza kesi ya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi Ukanda wa Tanzania inayowakabili raia 36 wa kigeni maarufu kama ‘kesi ya samaki wa Magufuli’.


Hatua ya kupangwa kwa jaji Mwarija kusikiliza kesi hiyo kunatokana na uamuzi uliotolewa Machi 3 mwaka huu, na Jaji Razia Sheikh wa kujitoa ambapo alisema anajitoa kusikiliza shauri hilo si kwasababu ya hoja zilizowasilishwa na wakili wa washtakiwa John Mapinduzi na Ibrahim Bendera kwamba hawana imani naye, bali anajitoa ili haki ionekane inatendeka na kwamba jalada la kesi hiyo analipeleka kwa Jaji Mfawidhi Semistocles Kaijage ili aweze kumpanga jaji mwingine.

Kwa mujibu wa hati ya wito ya mahakama hiyo inayoihalifu ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP),Eliezer Feleshi na mawakili wa utetezi , mahakama hiyo imezitaka pande hizo mbili kufika mahakamani Mei 5 mwaka huu, mbele ya jaji Mwarija ambapo kesi hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima jana wakili wa washtakiwa John Mapinduzi alithibitisha kupokea wito huo na kwamba siku hiyo watafika mahakamani hapo bila kukosa wao pamoja na wateja wao.

Februali 25 mwaka huu, washtakiwa hao kupitia wakili wao Mapinduzi walimwomba jaji huyo ajitoe ikiwa ni saa chache tu baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha makosa yanayowakabili yanadhamana kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ila akasema kwa mazingira ya kesi hiyo mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana.

Machi 9 mwaka 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uvivu haramu katika kina kirefu cha habahari ya Hindi Ukanda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuharibu mazingira ya ukanda huo.Hadi sasa washtakiwa wanaendelea kusota rumande kwa kukosa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 28 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.