Header Ads

SIRI ZA RICHMOND ZAZIDI KUFICHUKA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa tatu wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC, Injinia Simon Jilima ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa hafahamu kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo aliyepo Marekani Mohamed Gile amewahi kulalamika kuwa mshtakiwa Naeem Gile ameghushi hati ya nguvu ya kisheria ya kampuni yake kufanyakazi hapa nchini chini ya mshtakiwa huyo.


Jilima ambaye ni Mhandishi wa Shirika la Umeme(TANESCO) alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema wakati akihojiwa na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa ikiwa ni muda mfupi naada ya shahidi huyo kumaliza kuongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Mkuu wa Serikali Fredrick Manyanda ambapo pia shahidi huyo alidai kuwa hamfahamu ni nani aliyekuwa akiiwakilisha kampuni ya Richmond hapa nchini licha yeye aliteuliwa na Meneja Mkuu wa Idara ya Uzalishaji ya shirika hilo kuwa mhandishi msimamizi wa mradi wa kufunga mashine za kuzalisha umeme zilizoletwa na kampuni ya Richmond nchini.

“Namfahamu Mohamed Gile kupitia makabrasha kwamba yeye ndiye mkurugenzi wa Richmond yenye makao makuu nchini Marekani lakini sijawahi kuonana naye ana kwa ana...na sifahamu kuwa hiyo kampuni kama ilikuwa na mwakilishi wake hapa nchini”alidai mhandisi Jilima.

Awali akihojiwa na wakili mkuu wa serikali Manyanda, shahidi huyo Jilima alieleza mahakama kuwa mwaka 2006 alikuwa ni mhandisi katika katika kitengo cha uzalishaji umeme Tanesco na kwamba majukumu yake yalikjuwa ni kusimamia mitambo ya kuzalisha umeme na kwamba anaifahamu Richmond.

Jilima alieleza kuwa kwa mara ya kwanza aliifahamu kampuni hiyo wakati akiwa mjumbe wa kamati ya tathimini ya makampuni Machi 2006.Kwani kampuni hiyo ni miongoni mwa makampuni nane yaliyoleta maombi kwenye kamati hiyo ambaye naye alikuwa ni mjumbe na kwamba kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 12 ilianzishwa na Bodi ya Manunuzi ya shirika hilo na hatimaye kamati hiyo ilibaini hakuna kampuni iliyotimiza vigezo na matokeo yao hayo waliyafikishwa kwenye bodi ya Tanesco.

“Baada ya Bodi kupokea taarifa yetu hiyo bodi hiyo iliagiza tena kamati yetu iangalie upya kampuni hiyo na kweli kamati yetu kwa mara ya pili ikaya tathimini tena makampuni yale na ikabaini tena kuwa makampuni hayo hayakuwa yametimiza vigezo walivyokuwa wakivitaka na kamati hiyo ikaandika tena ripoti yake kwa bodi na baada ya hapo kilichoendelea huko mbele sikufahamu”alidai Jilima.

Aidha alidai baada ya hapo aliteuliwa na Meneja Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa Shirika hilo Steven Babaga kusimamia mradi wa kufunga mashine za kufua umeme zilizoletwa na kampuni ya Richmond na akapewa mkataba wa kufunga mitambo hiyo na kwamba mkataba ulikuwa ni baina ya Tanesco na Richmond wa mwaka 2006 na kwamba majukumu yake yalikuwa kusimamia ufungaji mitambo licha mitambo hiyo ililetwa na Richmond ikiwa imechelewa.

‘Na awali nilikuwa nimeelezwa kwamba mitambo hiyo italetwa na Richmond kupitia kampuni ya Tratt-Whirtacy lakini baadaye kutokana na mabadiliko ambayo nilikuwa kuarifiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha ambaye ni miongoni mwa mawaziri waliojiuzulu kutokana na kashfa ya mkataba huo kwamba kampuni Tratt-Whirtacy haitaileta mitambo hiyo na kwamba mitambo hiyo italetwa na kampuni nyingine iitwayo GE Electric na kweli mitambo hiyo yenye megawati 100 ililetwa na tukaifunga”alidai shahidi huyo.

Kesi hiyo ambayo ilipangwa kuzisilikizwa mfululizo kwa siku tatu, kuanzia juzi na kwamba ingemalizika leo, katika hali isiyotarajiwa Wakili Mkuu wa Serikali Manyanda aliyaambia mahakama kuwa itawawia vigumu kuwapata mashahidi wengine hivyo akaiomba mahakama iarishe kesi hiyo jana hadi tarehe nyingine ambapo Hakimu Lema aliarisha shauri hilo hadi Mei 9-10 mwaka huu, na akautaka upande wa Jamhuri uakikishe unawaleta mashahidi wengi kadri iwezekanavyo.

Februali 2009 ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa (Naeem) alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.Aidha, alidai katika shitaka la tano mshtakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka 2006 iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni, Hemed Gile ambaye ni kaka yake kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Aprili 13 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.